
Waombolezaji wakibeba jeneza lenye mwili wa Daktari Gilbert Buberwa wa Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kuagwa. Daktari huyo, aliyefariki kwa kuugua homa ya dengue, anatarajiwa kuzikwa leo jijini Dar es Salaam. Picha na Rafael Lubava.
Dar/Dodoma. Wakati taharuki iliyosababishwa na
mlipuko wa homa ya dengue ikiendelea kutikisa kila kona ya jiji, imebainika
kwamba gharama za vipimo katika hospitali mbalimbali zinafikia Sh50,000, ikiwa
ni tofauti kubwa na Sh1,000 kwa kipimo cha malaria.
Ugonjwa huo unazidi kusambaa jijini Dar
es salaam na baadhi ya mikoa, kiasi cha mamlaka kuagiza mabasi yote yaendayo
mikoani yafanyiwe usafi wa kunyunyizia dawa za kuua wadudu kudhibiti usienee
zaidi mikoani. Pia wananchi wameshauriwa kuvaa nguo ndefu ili kudhibiti mbu
wanaoeneza ugonjwa huo mchana tofauti na mbu wa malaria.
Timu ya waandishi wa Mwananchi ilipita
katika baadhi ya hospitali kubwa binafsi na za Serikali jijini Dar es Salaam na
kubaini kuwa gharama ya kupima homa hiyo ni kubwa zaidi katika hospitali na
vituo binafsi vya afya, lakini wagonjwa wanaokwenda katika hospitali za
Serikali hulazimika kulipa kati ya Sh25,000 na Sh30,000. Pamoja na homa hiyo
kufananishwa na malaria kwa dalili na kuenezwa na mbu, gharama za vipimo vyake
ni tofauti kwani mgonjwa wa malaria hutozwa kati ya Sh1,000 na 2,000.
Hata hivyo, jambo la kutia moyo ni
kwamba baada ya mgonjwa kupata majibu na kubainika anaumwa homa ya dengue,
gharama za tiba huwa ndogo kati ya Sh200 na 500 za kununulia dozi ya dawa za
kutuliza maumivu aina ya panadol.
Wanaopima waongezeka
Mchunguzi wa magonjwa katika maabara ya
kimataifa ya Lancet, Kanda ya Tanzania, Mohamed Abdulai alisema idadi kubwa ya
watu wanakwenda katika maabara hiyo kupima homa ya dengue tangu ugojwa huo
uenee kwa kasi kati ya Machi na Aprili mwaka huu.
Alisema kwa siku wagonjwa zaidi ya 40
hupima dengue na katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja, wagonjwa 53
waligundulika kuwa na homa hiyo.
Abdulai alisema gharama za kipimo cha
dengue katika kituo hicho ni Sh50,000.
Katika Hospitali ya Aga Khan, Mkurugenzi
wa Tiba, Dk Jaffer Dharsee alisema kipimo cha homa ya dengue ni kati ya
Sh35,000 hadi Sh40,000 kutokana na mchakato wa upimaji wake.
“Ni lazima tunapompima mtu dengue pia
tumpime na maradhi mengine kwanza kama homa ya matumbo, malaria na maradhi
mengine ambayo tunahisi anayo na ndiyo gharama inakuwa kubwa,” alisema Dk
Dharsee.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Hindu Mandal,
Dk Kaushik Ramaiya alisema katika hospitali hiyo kipimo cha homa ya dengue ni
Sh30,000. “Tunatumia vipimo vitatu, kile kitakachoangalia iwapo chembe hai
nyeupe za damu zimepungua, malaria na kiwango cha sumu kinachotokana na virusi
vya dengue,” alisema.
Dk Ramaiya alisema tangu vyombo vya
habari vianze kuripoti ugonjwa huu, watu wamejawa hofu na hufika hospitali kwa
wingi wakitaka kupima maradhi hayo ili kujua kama wapo salama.
Dk Kebwe alisema Serikali imeanza
utaratibu wa kupuliza dawa ya kuua wadudu wakiwamo mbu kwenye mabasi na maeneo
yote yenye watu wanaoingia na kutoka Dar es Salaam, ili kuepuka ugonjwa wa dengue
kusambaa nchini.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutoa
kauli ya mawaziri bungeni kuhusu ugonjwa huo, Dk Kebwe alisema hatua hiyo
inafanywa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa
kushirikiana na wizara yake.
“Mkoa wa Dar es Salaam, umeanza zoezi la
kupulizia viatilifu vya kuua mbu katika mabasi yanayoingia na kutoka Dar es
Salaam,” alisema Dk Kebwe, kauli ambayo iliungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Said Meck Sadiki.
Awali, Dk Kebwe alisema wananchi
wanatakiwa kuvaa nguo ndefu, kutumia vyandarua vyenye dawa na kuweka nyavu
kwenye madirisha na milango ya nyumba ili kujikinga na ugonjwa huo.
Alisema mbu huyo anayeishi katika
mazingira ya binadamu huuma mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye
vivuli, hususan majira ya asubuhi na jioni kabla jua halijazama.
Temeke wamuaga Dk Buberwa
Jana wafanyakazi wa Hospitali ya Temeke
waliuaga mwili wa Dk Gilbert Buberwa aliyefariki dunia Jumapili kutokana na
homa ya dengue.
Sadiki, aliyeongoza wafanyakazi hao,
alisema: “Tumepoteza nguvu kazi muhimu katika sekta ya afya, tena kwenye
Kitengo cha Magonjwa ya Akili. Alikuwa kijana mdogo na alitegemewa sana.”
Mwili wa Dk Buberwa ulihifadhiwa
hospitalini hapo tangu alipofariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
alipokuwa amepelekwa kwa dharura baada ya hali yake kuwa mbaya.
Baada ya wafanyakazi kuuaga mwili huo
kwa majonzi na vilio, ulipelekwa nyumbani kwa marehemu, Tabata Kinyerezi
kusubiri taratibu nyingine za mazishi leo jioni.
Imeandikwa na Florence Majani, Andrew
Msechu, Julius Mathias, Beatrice Moses na Sharon Sauwa.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment