
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange (kulia), Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Samuel Ndomba (katikati) na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Raphael Muhuga wakisoma kitabu cha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2014/15, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi.
Dodoma. Vijana wasiopungua 45,000 watakaomaliza
kidato cha sita watajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria
na watakaokwepa mafunzo hayo ya miezi mitatu, watashtakiwa.
Mpango huo wa kupitisha JKT wahitimu wa kidato cha sita na vyuo,
ambao ulifutwa mwanzoni mwa miaka ya 90 kutokana na matatizo ya kifedha na
kurejeshwa bila mafanikio ya miaka ya hivi karibuni, ulilenga kujenga uzalendo
kwa vijana na kuongeza ukakamavu.
Jana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Dk Hussein Mwinyi
alisema utaratibu huo ni wa kisheria na si hiari, hivyo wahitimu wa kidato cha
sita watambue kuwa ni kosa kukaidi wito wa kujiunga na JKT.
Dk Mwinyi, aliyekuwa anawasilisha bungeni makadirio ya mapato na
matumizi ya wizara yake, alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015, vijana
watakaojiunga na jeshi watafanya hivyo kwa awamu tatu.
Alisema awamu ya kwanza itahusisha vijana 20,000 ambao wataingia
katika mafunzo hayo Juni hadi Septemba 2014 na kufuatiwa na wa awamu ya pili
itakayochukua vijana 14,450 kuanzia Oktoba hadi Januari 2015 wakati awamu ya
tatu ya vijana 10,550 itaanza Januari hadi Aprili 2015.
Hata hivyo, kumekuwepo na mwingiliano wa muda wa kujiunga na
jeshi hilo na wa kujiunga na masomo ya juu. Kati ya vijana 15,000 waliotakiwa
kujiunga na jeshi hilo kati ya Oktoba 2013 na Januari 2014, waliojiunga
walikuwa 1,002 tu.
Alipoulizwa kuhusu mwingiliano huo, naibu waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama alisema atatoa ufafanuzi huo leo.
Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, mbunge wa viti maalumu (CCM),
Esther Bulaya alitaka mafunzo ya JKT kwa wabunge yafanyike kwa miezi miwili
hadi mitatu badala ya wiki mbili.
Bulaya, ambaye alipitia mafunzo hayo pamoja na wabunge wenzake
wakati mpango huo uliporejeshwa mapema mwaka jana, alisema kuwa hali hiyo
itawafanya wabunge hao kujifunza mambo mengi zaidi.
Bulaya aliwataja baadhi ya wabunge vijana wanaotakiwa kujiunga
na mafunzo hayo kuwa ni John Mnyika (Chadema-Ubungo) na Catherine Magige (viti
maalumu-CCM).
“Mheshimiwa Spika naomba uwaruhusu wabunge kwenda kwenye mafunzo
kwa miezi miwili hadi mitatu,” alisema na Bulaya na kuongeza:
“Katika kambi za JKT kuna tatizo la vifaa vya afya, hivyo wizara
iliangalie hilo ili wanaokwenda katika mafunzo hayo wapate tiba sahihi na kwa
wakati. Wataka muda uongezwe
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na
Usalama kuhusu wizara hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Vita Kawawa alipendekeza
muda wa JKT uongezwe hadi miezi sita.
Kawawa alisema ingawa Serikali inasema kuongeza muda huo
kunashindikana kutokana na mabadiliko ya mihula ya masomo vyuoni, bado
wanasisitiza umuhimu wa kuongeza muda wa mafunzo.
Kamati hiyo imeshauri vijana wote wanaomaliza kidato cha sita
kujiunga na JKT na wale ambao hawataripoti kwa mafunzo bila sababu za msingi,
Serikali iwachukulie hatua za kisheria.
Bajeti ya Wizara
Kuhusu bajeti, Dk Mwinyi alisema wizara yake itatumia Sh1.26
trilioni kwa mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali,
zikiwamo kununua ndege za kivita.
Dk Mwinyi aliliambia bunge kuwa kati ya Sh1.26 trilioni, Sh1.0
trilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati kiasi cha Sh249
bilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa
na wizara hiyo ni pamoja na kununua vifaa na zana za kijeshi, ikiwamo vifaa vya
uhandisi wa medani na ndege za kivita.
Pia,alisema wizara itaanza ujenzi wa gati katika Kamandi ya
Jeshi la Wanamaji Kigamboni, kuboresha mifumo ya mawasiliano ya ndani na nje ya
vikosi vya kambi za jeshi na kuendelea na ujenzi wa nyumba 6,064 za makazi ya
wanajeshi.
Dk Mwinyi alizitaja shughuli nyingine zitakazofanywa kuwa ni
kukamilisha ujenzi wa shule ya mafunzo ya awali ya kijeshi (RTS), eneo la
Kihangaiko, Pwani na Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC), Tengeru Arusha.
Pia,wizara itaanza ujenzi wa hospitali kuu ya jeshi eneo la
Mataya mkoani Pwani, kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine duniani katika
nyanja za kijeshi na pia kulipa madeni ya kimkataba.
Hata hivyo, Dk Mwinyi alisema kuwa pamoja na bunge kuidhinishia
wizara hiyo Sh1.1 trilioni kwa mwaka unaoishia Juni 30 mwaka huu, hadi Machi
ilikuwa imepokea Sh768.4 bilioni, sawa na asilimia 69.7.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment