Baadhi ya meno ya tembo yaliyokamatwa Uchina.
Meno ya tembo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya vielelezo mahakamani yalitoweka katika Kituo cha Polisi cha Kilwa mkoani Lindi.
Tukio hilo limenukuliwa
katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
ikisema meno makubwa 108 ya tembo na kilo 20 za meno mengine ya tembo
yaliyokuwa yamehifadhiwa kama kielelezo cha kesi za uhujumu uchumi,
yamebainika kutoweka kinyemela.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni juzi,
imebainisha kuwa meno mengine makubwa ya tembo yaliyokuwa na uzito wa
kilo 498.3 yamebadilishwa kinyemela na meno madogo, hivyo kusababisha
hasara ya kilo 203.66 za meno ya tembo ambazo thamani yake
haikufahamika.
CAG Ludovick Utouh katika ripoti hiyo ya mwaka ulioishia
Juni 30, 2013, amebainisha kuwa kumbukumbu katika Pori Tengefu la
Miguruwe zilionyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Juni 5 hadi Juni 8,
2012 meno makubwa 108 yalikuwa miongoni mwa vielelezo kituoni hapo.
Kati
ya meno hayo 108 yaliyokamatwa katika matukio ya ujangili, 74
yalitoweka katika kituo cha polisi wakati 34 yalibadilishwa na meno
madogo, tofauti na yale yaliyokuwa yamekamatwa yakihusishwa na kesi ya
ujangili Na. 3/2009 na kesi nyingine ya uhujumu uchumi Na. 2/2010 ambazo
zilikuwa zikiendelea mahakamani mkoani Lindi.
Pia ilibainika
kuwa kilo 20 za meno ya tembo ambayo yalikamatwa na kuhifadhiwa kama
kielelezo cha majalada KLM/IR/184/2009, KLM/IR/235/2009 na
KLM/IR/567/2010 yalitoweka.
Gari la ujangili latowekaUkaguzi
huo pia ulibaini kuwa gari lililokamatwa likiwa kielelezo baada ya
kukutwa na kilo 26 za meno ya tembo yenye thamani ya Sh135 milioni
liliondolewa kinyemela katika Kituo cha Polisi Kilwa.
CAG katika ukaguzi
huo alibaini upungufu katika usimamizi wa meno ya tembo na nyara
nyingine za taifa katika chumba cha meno hayo Dar es Salaam na vituo vya
mikoani.
CAG katika taarifa yake hiyo amesema kutokana na kukosekana kwa
kumbukumbu sahihi, meno ya tembo yanaweza kuibwa au kupotea bila
menejimenti kuwa na taarifa yoyote, hivyo ameishauri Serikali
kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa kutosha katika usimamizi wa nyara za
Serikali nchi nzima.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment