Na Daniel Mbega
BUNGE la Bajeti limeanza mjini
Dodoma, ambako tunaambiwa kwamba serikali imepanga kutumia kiasi cha trilioni
19 kwa shughuli za utawala na maendeleo.
Ingawa bajeti halisi
haijasomwa, lakini makadirio yaliyotangazwa awali yanaonyesha wazi kuna
ongezeko la bajeti hiyo ikilinganishwa kwa mwaka unaoishia Juni 30 mwaka huu.
Fedha hizi ni nyingi, ingawa
kwa uhalisi kushuka kwa thamani ya Shilingi nako kunaifanya bajeti hiyo
ionekane ndogo zaidi.
Hata hivyo, bajeti hii ni
muhimu sana kwa maendeleo ya taifa, hivyo hatutarajii kabisa kuona ngonjera,
majigambo, tambo na hata kususa kwa wabunge kwenye mijadala ya bajeti hiyo kama
ambavyo tumeshuhudia katika vikao vingi tu, likiwemo Bunge Maalum la Katiba.
Watanzania wametega masikio yao
huko Bungeni kuona wawakilishi wao wanajadili vipi bajeti ambayo inaweza
kuwakomboa, siyo ablakhadabla ambazo haziwasaidii chochote katika maisha yao ya
kila siku.
Tumemsikia wenyewe Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, akitangaza wakati wa
kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kwamba mishahara ya
wafanyakazi itaongezwa na pia kodi ile ya P.A.Y.E itapunguzwa ili kuwapunguzia
mzigo mkubwa wa makato.
Hata hivyo, hatujawahi kusikia
serikali ikitangaza unafuu kwa wananchi wa vijijini, hasa wakulima na
wajasiriamali wengine, ambao asilimia 83 iko huku vijijini.
Wananchi hawa wanalitazama
Bunge la Bajeti kama linaweza kuwaletea unafuu katika huduma mbalimbali za
maendeleo, zikiwemo afya, elimu na hasa kilimo ambacho ndicho kinachochukua
sehemu kubwa ya ajira ya Watanzania walio wengi.
Tumeshuhudia wenyewe serikali
ikizindua Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta kadhaa nchini,
lakini matokeo hayo hayawezi kuja bila kuwa na bejeti zinazoweza kuwakomboa
wananchi wa vijijini, vininevyo tutajidanganya kwa kutaka ‘Kuibadili Tanzania
iwe Singapore’!
Elimu yetu haiwezi kupanda
kiwango ikiwa mitaala yenyewe ni mibovu isiyokidhi viwango vya kimataifa, huku
shule zetu za msingi na zile za kata zikiwa hazina walimu, achilia mbali watoto
wetu kuendelea kuketi chini na walimu kulilia madai yao yasiyosikilizwa kwa
miaka mingi sasa.
Lakini taifa haliwezi kuwa na
wazalishaji imara ikiwa huduma za aya ni duni, huku wajawazito wakijifungua kwa
kutumia mwanga wa tochi na wanaobahatika kwenda hospitalini lazima wakodishe
ambulance za umma ambazo sehemu nyingine zimekuwa vitegauchumi vya wakubwa wa
halmashauri.
Hatuwezi kusema tunaleta
matokeo makubwa sasa ikiwa mkulima, ambaye ndiye mzalishaji mkuu nchini, anaendelea
kutumia jembe la mkono miaka 53 baada ya Uhuru. Huko ni kujidanganya.
Ikiwa leo hii ruzuku ya
pembejeo katika kijiji chenye wakulima 2,500 zinaletwa vocha 200, tunawezaje
kujidanganya kwamba tunaongeza uzalishaji? Zile fedha zetu walizorudisha wale
wezi wa EPA si tuliambiwa zinaelekezwa kwenye kilimo? Sasa zinafanya kazi gani?
Halafu zile chenji za Rada nazo
tuliambiwa zimeelekezwa kwenye elimu kwa ajili ya ununuzi wa vitabu, lakini
huko tumeshuhudia uhuni usio na kifani kwa darasa moja kuwa na vitabu zaidi ya
viwili vya somo moja. Kisa, soko huria ambalo limekuwa holela na lisilojali
maendeleo ya elimu.
Kwa mukhtadha huo basi,
Watanzania wanatamani sana kuona bajeti ya mwaka huu ikielekezwa katika maeneo
hayo matatu nyeti, huku kilimo kikipewa kipaumbele cha kutosha na kuwawekea
wakulima mazingira mazuri zaidi ya masoko ya bidhaa zao tofauti na sasa ambapo
mazao yao ama yanaozea shambani kwa kukosa soko au wanapunjwa kutokana na
kutokuwepo kwa mfumo mzuri.
Hakika, maendeleo ya Tanzania
yanategemea zaidi bajeti na kwa maana hiyo mjadala katika Bunge la Bajeti ni
muhimu mno ili uweze kuleta taswira njema ambayo itawanufaisha Watanzania wote.
Kelele za ‘Wanafiki waseme
Ndiyoooo’ zimewachosha Watanzania, lakini pia zile tabia za baadhi ya waunge,
hasa wa upinzani kususa vikao kama ‘watoto wa mwisho’ haziwasaidii Watanzania
na inabidi zikome mara moja.
Kama mambo hayaendi sawa ndani
ya Bunge, ni vyema wakakomaa humo humo ili tuweze kuona nani ni mkorofi
anayekwamisha maendeleo ya Watanzania, lakini wanapotoka nje ya Bunge mwisho wa
siku Watanzania watawaona kwamba wao ndio wakorofi.
Waheshimiwa hawa wakumbuke
kwamba, fedha zinazotolewa kama posho na mishahara yao ni kodi ya Watanzania
wanayokatwa kuanzia kwenye pipi mpaka kwenye bia. Yaani kila bidhaa ambayo
Mtanzania anainunua lazima akatwe kodi, na kodi hiyo ndiyo inayowaia jeuri
wengine wanafanya mambo ya ajabu Bungeni.
Hakika Watanzania wanataka
kuona bajeti inatoa vipaumbele kwenye afya, elimu na kilimo, sekta ambazo
zinabeba dhima kubwa ya maisha yao.
Kinyume chake, matokeo makubwa
sasa ni ndoto za mchana kama mkulima au mwananchi wa kijijini hajakombolewa.
Alamsiki.
No comments:
Post a Comment