Chopa iliyodondoka juzi
SIKU moja baada ya viongozi waandamizi wa serikali kunusurika kufa katika ajali ya helikopta iliyoanguka juzi wakati ikijaribu kuruka, viongozi hao wamesema hawajui waliponaje.
Viongozi hao ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, ambao wote kwa nyakati tofauti wamesema ni muujiza wa Mungu ndio uliowaokoa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk. Magufuli alisema wakati ajali hiyo inatokea kabla ya kufanikiwa kutoka nje ya helikopta hiyo, alijua kwamba mwisho wa maisha yake umefika.
“Sijui tumeponaje na siamini kama bado niko hai. Nilipata mshituko mkubwa baada ya kusikia kishindo kikubwa kilichotokea wakati helikopta hiyo inaanguka, hapo nilijua tumekufa,” alisema Waziri Magufuli.
Akifafanua zaidi, waziri huyo alisema kuwa wakati helikopta hiyo inaanguka, alichokumbuka ni kusali, kumuomba Mungu awanusuru na kifo kilichokuwa mbele yao.
“Kwa kweli nilishindwa kuamini, sikutambua nini kingenikuta, leo hii yangekuwa mambo mengine wala tusingekuwa pamoja, lakini kutokana na maombi niliyoyafanya baada ya kuona kifo kinatukaribia, naamini yalisaidia na hatimaye tukatoka tukiwa wazima licha ya kupata maumivu ya kawaida,” alisema Magufuli.
Dk. Magufuli alisema chanzo cha ajali hiyo ni helikopta kupata hitilafu wakati ilipotaka kuruka katika Uwanja wa Ndege wa Jeshi (Airwing) Ukonga, Dar es Salaam na hatimaye kurudi chini ghafla.
Kova ataka muda zaidi wa kupumzika
Kwa upande wake, Kamishna Kova alisema kama inawezekana alitaka apewe muda wa kupumzika ili kutafakari kilichotokea kwani haamini kama wamepona.
“Lile tukio ni kubwa na limehusisha viongozi wa kitaifa na mimi nikiwa sehemu yao. Binafsi ningependa kupata muda wa kupumzika kabla ya kuongea jambo lolote zaidi kuhusiana na ajali hiyo,” alisema Kamishna Kova.
Sadick: Sijui shukrani gani zinamtosha Mungu
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, akizungumzia ajali hiyo, alisema anamshukuru Mungu kumnusuru katika ajali hiyo ya kutisha.
“Jambo la kushukuru ni kwamba helikopta hiyo haikuwa imeruka juu sana kabla ya kupata hitilafu, hata hivyo bado kwa umbali ule, ni vigumu kuamini kama tumepona,” alisema.
Akiongeza kuwa haoni shukrani gani zinatosha kumpa Mwenyezi Mungu kwa kuwaepusha katika ajali hiyo aliyosema itabaki katika kumbukumbu ya historia ya maisha yake.
“Sijui nifanye dua gani ambayo inaweza kulingana na mapenzi haya ya Mwenyezi Mungu kutuacha hai, hatukuwa na ujanja wowote wa sisi kujiokoa. Sijui ni shukrani gani nitoe ya kumtosha Mwenyezi Mungu,” alisema Sadick.
Viongozi hao walinusurika katika ajali hiyo juzi baada ya helikopta waliyotaka kutumia kwa ajili ya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na mafuriko jijini Dar es Salaam kuanguka ikiwa ni mita chache baada ya kuruka.
Katika ajali hiyo iliyohusisha helikopta ya Jeshi la Wananachi wa Tanzania (JWTZ), mbali ya viongozi hao pia walikuwamo waandishi wa habari wawili, marubani wawili, walinzi wa makamu wa rais wawili na ofisa mwingine kutoka Ikulu.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment