UPANDE wa utetezi katika kesi ya mauaji inayowakabili raia wawili wa Kenya na Mtanzania mmoja wanaotuhumiwa kumuua askari wa Jeshi la Polisi, Ex. PC Michael Milanzi, aliyeuawa kwa kupigwa risasi Julai 11, mwaka 2007 katika Benki ya NMB Tawi la Mwanga, umedai hakuna aliyeshuhudia askari huyo akiuawa.
Akichambua ushahidi wa mashahidi watatu kati ya 18 walioitwa na upande wa mashitaka mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Kasusulo Sambo, Wakili wa washitakiwa hao, Majura Magafu, alidai hata askari aliyekuwa katika lindo na marehemu hakushuhudia mwenzake akiuawa.
Washitakiwa hao, Samwel Gitau Saitoti na Michel Kimani, pamoja na Mtanzania, Kalist Joseph Kanje, wanashitakiwa kwa kosa la kumuua kwa makusudi Milanzi kwa kumpiga risasi wakati askari huyo akiwa lindoni kwenye benki hiyo.
Katika tukio hilo, sh milioni 239 kiliporwa pamoja na bunduki aina ya SMG, mali ya Jeshi la Polisi nchini pamoja na magazini iliyokuwa na risasi 30 ambapo kabla ya uporaji huo majambazi hao walimteka aliyekuwa meneja wa benki hiyo,Robert Marandu.
Wakili Magafu alidai hata PC .Naftari aliyekuwa lindoni siku ya tukio pamoja na marehemu, katika ushahidi wake alidai baada ya kuvamiwa palitokea purukushani na baadaye alimuona mwenzake akiwa ameanguka chini huku akitokwa damu kichwani.
Alidai hata aliyekuwa meneja wa benki hiyo, Robert Marandu, naye hakushuhudia wala kuona mtu aliyemuua askari huyo na kwamba hawafahamu hata aina ya silaha iliyotumika kumuua.
Magafu alidai upo utata juu ya silaha iliyotumika katika mauaji hayo kutokana na kutofautiana kwa namba za silaha aina ya SMG inayodaiwa kumuua marehemu kwa madai kuwa bunduki iliyopelekwa kwa mtaalamu wa silaha ilikuwa tofauti na silaha inayodaiwa kukamatwa kwa washitakiwa Gitau na Kimani eneo la Njiro, jijini Arusha.
CHANZO: TANZANIADAIMA
No comments:
Post a Comment