Jana, Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani akisindikizwa na polisi waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi, huku wafuasi wake wakizuiwa nje ya uzio wa Mahakama hiyo kwa sababu za kiusalama.PICHA|MAKTABA.
Morogoro. Kiongozi wa Taasisi ya Kiislamu
Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda ameendelea kusota rumande baada ya kesi yake
kuahirishwa kwa mara nyingine kwa kuwa jalada la kesi yake, halijarudi kutoka
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam lilikoitishwa kwa ajili ya mapitio.
Kesi hiyo
iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro mwaka
jana, iko mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mary Moyo na imekuwa
ikitajwa kwa zaidi ya miezi sita, huku Sheikh Ponda akiendelea kusota rumande
baada ya kunyimwa dhamana.
Sheikh
Ponda anakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kutotii amri halali iliyotolewa
na Mahakama ya Kisutu ya kutokutoa maneno yenye kuharibu imani za dini na
kushawishi watu kutenda kosa ambayo anadaiwa kuyatenda Agosti 10, 2013 jioni katika
eneo la Kiwanja cha Ndege, Morogoro.
Jana,
Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani akisindikizwa na polisi waliokuwa na silaha
za moto na mabomu ya machozi, huku wafuasi wake wakizuiwa nje ya uzio wa
Mahakama hiyo kwa sababu za kiusalama.
Mara baada
ya kutajwa kwa kesi hiyo, Hakimu Moyo alisema jalada la kesi hiyo, bado
halijarudi kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, hivyo kuiahirisha kesi
hiyo hadi Mei 26, mwaka huu itakapotajwa tena.
Upande wa
mashtaka uliwasilisha ombi mahakamani hapo kutaka Sheikh Ponda kuhojiwa na
polisi kuhusiana na mashtaka yanayomkabili. Hakimu Moyo alikubali ombi hilo na
kumtaka Sheikh Ponda kuwa na imani na Mahakama hiyo, akisema itatenda haki kwa
mujibu wa sheria na si vinginevyo.
No comments:
Post a Comment