Waziri wa Fedha wa SMZ, Omar Yussuf Mzee.PICHA|MAKTABA
Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)
jana iliwasilisha bajeti yake ya Sh708.8 bilioni kwa mwaka 2014/2015 ambazo ni
pungufu mara 28 ya Bajeti ya Jamhuri ya Muungano ya Sh19.7 trilioni
inayotarajiwa kuwasilishwa mwishoni mwa Juni mwaka huu.
Sambamba na bajeti hiyo, SMZ imetangaza
mikakati ya kukusanya fedha hizo kwa kupandisha kodi za leseni za udereva na
ada ya usafiri wa anga kwa wasafiri wa ndani.
Waziri wa Fedha wa SMZ, Omar Yussuf Mzee
alitangaza mpango huo jana alipowasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Serikali katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani,
Unguja.
Waziri Mzee alisema ili kuimarisha uwezo
wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar na kutoa huduma bora, wasafiri wa
ndani watalazimika kulipa Sh3,000 badala ya 1,000 na mabadiliko hayo
hayatawahusu wasafiri wa nje ya nchi ili kutoathiri sekta ya utalii visiwani.
Pia ada za leseni ya udereva kwa miaka
miwili italipwa kwa Sh35,000, miaka mitatu Sh45,000 na kwa miaka mitano kwa
Sh60,000.
Alisema SMZ imeamua kufuta utaratibu wa
kila mwaka kwa madereva kulipia leseni ili kuwaondolea usumbufu na sasa kuweka
utaratibu wa kukata leseni za muda mrefu na utekelezaji wake utaanza mwaka huu
wa fedha.
EFD zaingia Zanzibar
Pia Waziri Omar alisema ili kudhibiti
ukwepaji kodi, SMZ inatarajia kuanzisha utaratibu wa stakabadhi kutolewa kwa
mashine maalumu za (EFD) na wafanyabiashara wote watalazimika kuwa na mashine
hizo kwenye maduka yao ambazo zitasaidia biashara kufanyika kisasa na kudhibiti
mapato ya Serikali.
Hata hivyo, alisema bajeti ya mwaka huu
ina nakisi ya Sh36 bilioni na kwamba Serikali itaziba pengo hilo kupitia mapato
yatakayokusanywa kutokana na Kodi ya Wafanyakazi (Paye) wa Muungano walioko
Zanzibar na Sh21 bilioni zitakusanywa kutoka vyanzo hivyo na Sh15 bilioni zitatokana
na mikopo ili kuleta uwiano wa bajeti, mapato na matumizi yake.
Pia alisema Pato la Taifa limekua kutoka
Sh1,342.6 bilioni mwaka 2012 hadi kufikia Sh1, 442.8 bilioni wakati pato la mtu
binafsi limekua kwa asilimia 4.6 kutoka Dola za Marekani 656 hadi Dola 667
mwaka 2013.
Kuhusu deni la Taifa, Waziri Mzee
aliwaeleza wajumbe wa Baraza hilo kwamba limeongezeka na kufikia Sh294.90
bilioni sawa na ongezeko la asilimia 17.0 ikilinganishwa na deni la Sh252.3
bilioni lilikuwapo hadi Machi mwaka jana.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment