Bondia Francis Cheka
Dar es Salaam. Pambano la bondia Francis
Cheka la kuwania ubingwa wa dunia unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Dunia
(WBF), sasa litafanyika Juni 6 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es
Salaam.
Cheka, ambaye awali alipangwa kuzichapa
na Varely Brudov wa Urusi, amebadilishiwa mpinzani na sasa atazichapa na bondia
kutoka Uingereza.
Akizungumzia pambano hilo, Cheka alisema
tayari ameanza kambi ya wazi jijini Dar es Salaam kujiwinda na pambano hilo na
kusisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha anatwaa tena ubingwa huo aliovuliwa
mwishoni mwa mwaka jana.
“Nategemea wiki ijayo kwenda Morogoro
kujifua milimani kwa ajili ya kujenga pumzi, lakini pia natarajia kuweka kambi
nje ya nchi kujiwinda na pambano hilo,” alisema Cheka.
Wakati
huohuo, kocha mkuu wa timu ya taifa ya judo
iliyoweka kambi nchini Uturuki kujiandaa na Michezo ya Jumuiya ya Madola, Hamis
Zaid amesema kikosi chake hivi sasa kimekubaliwa kujifua na timu ya taifa ya
nchi hiyo baada ya kuonekana kufikia viwango.
Zaid alisema awali walipowasili nchini
humo hawakukubaliwa kuanza mazoezi na timu ya taifa kutokana na kiwango chao na
kukabidhiwa timu ya vijana ya nchi hiyo kabla ya kufuzu hatua ya awali na
kupewa nafasi ya kujifua na timu ya taifa ya nchi hiyo.
“Wenzetu wana programu ya muda mrefu
ambayo hivi sasa tunajitahidi kwenda nayo pamoja na mwelekeo wetu hivi sasa ni
mzuri.”
Kocha huyo aliyeambatana na wachezaji
Andrew Thomas, Abubakar Nzinge na Mbarouk Selemani alisema programu hiyo
itafanyika hadi Juni 29 ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa michezo hiyo.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment