Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 13 September 2016

WAKURUGENZI WAPYA WAASWA KUSIMAMIA MAPATO YA NDANI YA HALMASHAURI




Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene akizungumza katika hafla ya kuwaapisha Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji, Manispaa na Wilaya 13 walioteuliwa hivi karibuni. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora Angella Kairuki, Naibu Waziri Selemani Jafo, baadhi ya wakurugenzi, wafanyakazi kutoka OR-TAMISEMI pamoja na waandishi wa habari.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki akiongea Wakurugenzi wapya mara baada ya kuapishwa leo mjini Dodoma. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene. Kushoto kwa Simbachawene ni  Mkurugenzi mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilimanjaro Bi. Butamo Nuru Ndalahwa.
 Baadhi ya Wakurugenzi  wa halmashauri  wakisaini hati ya kiapo cha maadili ya utumishi wa umma pamoja na ahadi ya kuwa waaminifu na wazalendo kwa nchi yao leo katika ofisi za TAMISEMI mjini Dodoma mbele ya Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Ofisi ya Kanda ya Kati Cathlex Makawia.



Na Nasra Mwangamilo- Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI)  Mhe. George Simbachawene amewaasa Wakurugenzi wapya kusimamia mapato ya ndani katika halmashauri zao ili waweze kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwahudumia wananchi.
Waziri Simbachawene amesema hayo leo mjini Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha Wakurugenzi wapya 13 walioteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika katika jengo la Mkapa, Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa mjini Dodoma. Pamoja na kuapishwa, Wakurugenzi hao walikula kiapo cha maadili ya utumishi wa umma pamoja na ahadi ya kuwa waaminifu na wazalendo kwa nchi yao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Simbachawene alisema Wakurugenzi hao wanawajibu wa kusimamia mikataba iliyopo, iliyopita na itakayoingiwa na halmashauri zao  ikiwa ni pamoja na kuzingatia masharti ya mikataba hiyo wakati wa utekelezaji wake. Aidha, aliwahimiza kuwa wawajibikaji kwa mamlaka waliyonayo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kikatiba.
“Kuanzia leo mnaitwa viongozi, unapokuwa kiongozi unalazimika kuishi kwa namna tofauti kabla ya kuapishwa kuwa kiongozi, eneo mnaloenda kufanya kazi ni muhimu na mnaenda kuongoza taasisi na mnaenda kuwahudumia wananchi moja kwa moja” alisema Simbachawene.
Waziri Simbachawene amewaeleza Wakurugenzi hao kuwa unapozungumzia kuondoa umasikini wa wananchi, Mkurugenzi ndiye anayebeba bendera na dhamana ya kusimamia sekta zote ndani ya halmashauri ikiwemo afya, kilimo, elimu, maji, uvuvi ambazo zitawaletea hali bora ya maisha ya wanachi hao.
Katika kuyatekeleza majukumu hayo, Waziri Simbachawene amewahimiza wakurugenzi hao kufanya kazi na Wizara zote kwa kufutata sera mbalimbali na miongozo inayotolewa na viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Simbachawene amewataka Wakurugenzi hao kutembelea maeneo yao katika halmashauri zao badala ya kukaa ofisini kuanzia tarehe 1 hadi 30 kila mwezi ili kujionea changamoto zinazowakabili wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
“Tokeni ofisini na tembeleeni maeneo yenu, mna mambo mengi ya kufanya, ni lazima uwajue wananchi, viongozi unaofanya nao kazi, taasisi na watumishi wako kwa takwimu ikiwezekana kwa majina” alisisitiza Waziri Simbachawene.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Angellah Kairuki amewataka Wakurugenzi hao wafuatilie na kusimamia miradi ya maendeleo iliyopo ndani ya halmashauri zao kwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kuhusu watumishi hewa, Waziri Kairuki amesema kuwa hadi sasa wamebainika watumishi hewa 17,102 tangu kuanzishwa zoezi hilo Machi mosi mwaka huu na kuwaasa wakurugenzi hao kufuatilia watumishi ndani ya halmashauri zao ili kuondokana na dhana ya kuwa na watumishi hewa ndani ya halmashauri zao.
Ili kuwa na taarifa sahihi, Waziri Kairuki amewataka Wakurugenzi hao watumie mifumo sahihi ili kutoa taarifa sahihi za watumishi na kuondoa dhana ya watumishi hewa ndani ya halmashauri zao.
Kwa upande wao Mkurugenzi  mpya wa halmashauri ya wilaya ya Bukoba Mwantumu Dau na Frank Bahati wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe wamemshukuru Rais kwa kuwateua na kuhahidi kutomuangusha ambapo na watawatumikia wananchi kwa nguvu zao zote katika kuwaletea maendeleo.
Wakurugenzi 13 wa Halmashauri za Manispaa, Mji na Wilaya walioapishwa na Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Vingozi wa Umma, Ofisi ya Kanda ya Kati Cathlex Makawia ni pamoja na Godwin Emmanuel Kunambi Manispaa ya Dodoma, Elias R. Ntiruhungwa Mji waTarime, Mwantumu Dau Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Frank Bahati Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Hudson Stanley Kamoga Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Mwailwa Smith Pangani Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Godfrey Sanga                              Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na Yusuf Daudi Semuguruka Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.
Wakurugenzi wengine ni Bakari Kasinyo Mohamed Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Juma Ally Mnweke Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Butamo Nuru Ndalahwa          Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Waziri Mourice Halmashauri ya Wilaya ya Karatu na  Fatma Omar Latu Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.




No comments:

Post a Comment