Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.
MBUNGE wa jimbo la Vunjo ,James Mbatia (TLP) ameshinda kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia chama cha Tanzania Labour (TLP) Augustine Lyatonga Mrema .
Mbatia ameshinda kesi hiyo baada ya upande wa mlalamikaji (Mrema) kuamua kufuta shauri hilo kwa hati maalumu iliyowasilishwa katika mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi huku akikiri kumtambua Mbatia kama mbunge halali wa jimbo hilo.
Mbali na utambuzi huo Mrema pia amekanusha maelezo pamoja na ushahidi wake aliowasilisha mahakamani hapo dhidi ya Mbatia,wananchi wa jimbo la Vunjo pamoja na taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini ambazo zilitajwa mahakamani hapo wakati wa ushahidi wake.
Ukiwasilisha hoja mahakamani hapo mbele ya Jaji wa mahakama kuu Lugano Mwandambo , upande wa mlalamikaji ukiongozwa na wakili January Mkobogho ulieleza kuwa pande mbili katika shauri hilo wamefikia makubaliano nje ya mahakama.
Wakili Mkobogho aliiomba mahakama kuona makubaliano hayo ambayo yako katika maandishi kama alama kwa mujibu wa makubalinao waliyoafikiana baada ya kuingizwa na kupokelewa mahakamani hapo kama madai.
Alisema kwa kuwa kesi hiyo ya uchaguzi ikiwa na maslahi mapana ya umma na kwa kuwa mlalamikiwa wa pili na watatu waliunganishwa kwenye shauri hili kwa mujibu wa sheria aliomba kila upande ubebe gharama zao.
Wakili Mkobogho alieleza kuwa kutokana na pande zilizokuwa zinakwaruzana wameamua kukaa na kumalizana wenyewe na kwamba haoni sababu za mlalamikiwa wa pili na watatu kutokubeba gharama zao wenyewe.
Jopo la mawakili sita wa upande wa utetezi ukiongozwa na wakili , Mohamed Tibanyendera uliileza mahakama hiyo kwamba wanaungana na mtoa maombi kwa maslahi ya umma na kwamba wanakubali kila upande kubeba gharama zake.
Wakili mkuu wa serikali Mark Muluambo akisaidiana na wakili wa serikali Grayson Orcado , alisema wamesikia pande zote na wameafiki kuhusiana na uamuzi huo kutokana na kesi hiyo kuwa na maslahi kwa umma.
Alisema upande wao hauna pingamizi na maamuzi hayo na kwamba wamekili kupokea nakala na wataisoma na kuipitia vizuri, na kutokana na mlalamikiwa wa pili na watatu walitumia gharama katika kesi hiyo waliiomba mahakama walipwe nusu ya gharama hizo.
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande hizo mbili Jaji Mwandambo alieleza kupata maelezo kuwa mlalamikaji amekiri kwamba kesi hiyo hainafaida yeyote kwa wana Vunjo na kwamba amekubali kuwa tuhuma zake zote alizokuwa nazo juu Mbatia na watu wote aliokuwa anawahusisha na kesi hiyo kuwa amezitengua .
Jaji Mwandambo alieleza kuwa mlalamikaji pamoja na yote aliyoyasema pia amekiri kuwa mbunge wa sasa wa jimbo la Vunjo ,James Mbatia alichaguliwa kwa kura halali na alipata kura nyingi dhidi yake.
Nje ya mahakama Wakili Tibanyendera alisema haikuwa kazi rahisi kufikia maridhiano haya na kwamba ushawishi mkubwa umefanyika baada ya Wakili anyemtetea Mrema kumueleza ukweli mwenendo wa shauri hilo.
“Tumefanya kazi ya kuwashawishi wateja wetu ,Mrema amekiri katika maandishi yaliyosajiliwa leo mahakamani baada ya kuona kwamba kesi hii haina faida kwa wana vunjo,amekiri na kutengua tuhuma zake zote alizotoa dhidi ya Mbatia,wafuasi wake na taasisi nyingine.”alisema Tibanyendera.
“Hoja kubwa ilikuwa ni kupinga matokeo ya Ubunge,Mrema kwa maandishi amekiri kwamba Mbatia alichaguliwa kihalali na akapata kura nyingi kihalali,hayo yamo katika amri wa mahakama,”alisema Tibanyendera.
Akizungumza mara baada ya kufikiwa kwa uamuzi huo Mbunge wa jimbo la Vunjo,James Mbatia alisema Chama chake kina aamini katika itikadi za utu na kwamba amemsamehe na hata dai gharama za kesi hiyo.
“Tungeweza kumdai Mrema gharama kubwa,tangu kuletwa kwa kesi hiyo mahakamani,mimi sitamdai Mrema hata senti moja,nimemsamehe Mrema kwa sababu ni mpiga kura wa jimbo la Vunjo,nisingependa kuona anadidimia zaidi lazima ni mlee vizuri mzee wngu Mrema,”alisema Mbatia.
“Gharama za mawakili talipia asilimia 50 za mawakili wa upande wetu,Mrema amekubali kulipa sehemu ndogo ya malipo ya mawakili wetu, tungeendelea tungeweza kuuza hata nyumba zake, sasa atalipa Milioni 40 na tayari kwa hatua ya kwanza mawakili watapewa Mil 15 ambazo tayari ziko mahakamani,mwezi ujao atalipa Mil 15 na kabla ya mwezzi wa sita atalipa Mil 10 “aliongeza Mbatia.
Mbatia aliyekuwa amengozana na mawakili wake pamoja na baadhi ya wafuasi wa chama cha NCCR-Mageuzi alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa jimbo la Vunjo waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo .
“Niwashukuru wananchi wa jimbo la Vunjo kwa ushirikiano na muda mwingi uliopotea kwa ajili ya kufuatilia kesi hii ,yapo mengi ambayo tulitakiwa kuanza kuyafanya lakini muda mwingi tulitumia katika kushughulikia shauri hili “alisema Mbatia.
Upande wa utetezi katika shauri hilo ulikuwa ukiongozwa na Mawakili Mohamed Tibanyendra, Faith Sadala ,Youngsevior Msuya na Mike Kavala huku Mawakili wa serikali wakiwa ni Mark Mluambo Helen Mwajage na Lilian Machange.
Katika uchaguzi huo Mbatia alitangazwa mshindi kwa kupata kura 60,187 huku Mrema akiambulia kura 6,416, na mgombea wa CCM, Innocent Shirima, kura 16,097.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment