KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ameng'olewa! Ndiyo unaweza kusema baada ya kiongozi huyo kuondolewa na Rais John Magufuli kumteua Balozi Injinia John William Kijazi kushika wadhifa huo.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, imeeleza kwamba Balozi Sefue atapangiwa kazi nyingine!
Hata hivyo, kuondolewa kwa Balozi Sefue kumekuja takriban wiki mbili baada ya gazeti la Dira ya Mtanzania kuandika mfululizo wa makala zikimtaja kiongozi huyo kwa ufisadi mbalimbali.
Uchapishaji wa makala hizo ulisababisha Idara ya Habari (MAELEZO) kutoa taarifa kwa kulitaka gazeti hilo litoe ushahidi wa ushiriki wa Balozi Sefue ama liombe radhi mara moja kwa ukubwa ule ule vinginevyo hatua za kisheria zingechukuliwa dhidi yao.
Taarifa ya MALEZO ni hii hapa chini:
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
IDARA YA HABARI - MAELEZO
P.O. Box 8031, Dar es Salaam,
Tel: 2110585, 2122771/3,
Fax: 2113814,
e-mail: maelezo@habari.go.tz
Tarehe: 01/03/2016
Gazeti la Dira ya Mtanzania, Toleo Na.404 la Februari, 29 – Machi 6, 2016 liliandika taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho “Uchafu wa Ombeni Sefue Ikulu”. Taarifa
hiyo, ambayo ni muendelezo wa makala nyingine kwenye toleo la gazeti
hilo la wiki iliyopita, ilimtuhumu Katibu Mkuu Kiongozi kushawishi juu
ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD pamoja na Kampuni za “CRJE” na “UGG”
kupewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, Daraja la Kigamboni na
Reli ya Dar es Salaam - Kigali. Taarifa zote hizi ni za uongo na za
kupotosha wananchi.
Kuhusu uteuzi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD,
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,
hakuhusika kwa namna yoyote kushawishi uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa
MSD. Uteuzi huo ulitekelezwa kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa.
Nafasi hiyo ilitangazwa na Bodi tarehe 20 Novemba, 2013. Usaili
ulifanywa na kampuni huru iliyopewa jukumu hilo na Bodi. Mapendekezo ya
majina matatu yalipelekwa kwa Mhe. Rais na Waziri wa Afya, kwa ajili ya
uteuzi.Balozi Sefue alikuwa hamjui aliyeteuliwa na wala hakuwahi kuwa na uhusiano naye.
Alichofanya Balozi Sefue ni
kutangaza tu uteuzi baada ya Rais kuteua. Gazeti hilo pia limeandika
uwongo kuwa MSD haijawahi kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu asiye Mfamasia.
Tangu MSD ianzishwe mwaka 1993 hadi sasa, ni Mkurugenzi Mkuu mmoja tu,
Rino Meyers (1996-1999), ndiye alikuwa Mfamasia. Wakurugenzi wengine
kama Peter Mellon (1993-1995), Jay Drosin (2001-2004) na Joseph Mgaya
(2004-2013) hawakuwa Wafamasia.
Kuhusu Kampuni ya CRJE kuhusishwa na Balozi Ombeni Y. Sefue
Suala la
kumhusisha Katibu Mkuu Kiongozi na kampuni hii nalo ni uzushi na uongo
wa kupindukia. Wakati kampuni hii ikipewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu
cha Dodoma mwezi Oktoba 2007, Balozi Ombeni Y. Sefuehakuwa Katibu
Mkuu Kiongozi; alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani. Kadhalika
mchakato wa kumpata mkandarasi wa daraja la Kigamboni, ulipoanza mwezi
Machi, 2011, Balozi Sefuehakuwa Katibu Mkuu Kiongozi; alikuwa
Balozi wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, New York. Hata mkataba wa ujenzi
wa Daraja hilo uliposainiwa tarehe 9 Januari, 2012, Balozi Sefue alikuwa na wiki moja tu ya kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kufuatia kuteuliwa tarehe 30 Disemba, 2011. Aidha, Kampuni iliyoshinda tenda hiyo wala siyo CRJE kama ilivyoandikwa na gazeti hilo bali ni China Major Bridges Engineering Company (BCEC) kwakushirikiana na Kampuni ya China Railway Construction (CRCEG).
Kuhusu tuhuma kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Chapuo Kampuni ya UGG:
Katibu Mkuu
Kiongozi hajawahi kuipigia chapuo kampuni yoyote ile pahala popote.
Isitoshe, hakuna kampuni yenye jina la “UGG” iliyowahi kuonesha nia ya
kujenga reli ya kati. Hii ni moja ya uthibitisho kwamba gazeti hili
linatoa taarifa za kuokoteza zisizo na ukweli kama vile walivyopotosha
kuhusu jina la Katibu Mkuu Kiongozi kwenye makala yao ya pili kwenye
ukurasa wa tisa wa gazeti hilo yenye kichwa cha habari “Magufuli anaishi na jipu Ikulu” ambapo walimpachika Katibu Mkuu Kiongozi jina la Sifuni, jina ambalo hajawahi kuwa nalo. Balozi Sefue hajahusika,
hahusiki na wala hatahusika katika kuchagua wa kupewa tenda hiyo kwa
sababu yeye si sehemu ya wenye mamlaka ya kutoa tenda.
Kuhusu Eliachim Maswi:
Gazeti la Dira ya Mtanzania limeandika kuwa moja ya “madudu” aliyofanya Balozi Sefue ni walichoita kumsafisha Bwana Eliachim Maswi. Wanadai hivyo wakati wamekiri kuwa alichofanya Balozi Sefue ni kusoma matokeo ya uchunguzi, ambao hakuufanya yeye. Waliomsafisha Maswi ni
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali; Sekretarieti ya Maadili ya Umma;
na hatimaye kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu.
Kwa hiyo, kwa maoni ya gazeti hili, Balozi Sefue asingepaswa kusoma matokeo ya uchunguzi uliofanywa na vyombo hivyo huru. Kwa maoni yao kusoma taarifa ya uchunguzi ni “madudu”.
Habari hizo
hazina chembe yoyote ya ukweli, na wao wenyewe ndani ya gazeti wamekiri
hawana ushahidi, ni wazi kuwa habari hizo ni za kubuni na zimetungwa.
Kwa sababu hiyo, Serikali inalitaka Gazeti la Dira ya Mtanzania kukanusha uongo na uzushi wao na kumuomba radhi Balozi Ombeni Sefue,
kuiomba radhi Serikali na kuwaomba radhi wote walioumizwa na uzushi
huo kwa uzito ule ule uliotumika kuchapisha taarifa hiyo.
Vinginevyo iwapo
gazeti la Dira ya Mtanzania lina ushahidi wa huo “uchafu” wa Katibu Mkuu
Kiongozi, waupeleke mara moja kwenye vyombo vinavyohusika ikiwamo
Sekretarieti ya Maadili na TAKUKURU.Vinginevyo, hatua zikichukuliwa dhidi yao wasiseme Serikali inavibana vyombo vya habari.
Aidha Serikali inashauri wenye
vyombo vya habari, wachapishaji, wahariri na waandishi wa habari
wajikite kwenye weledi na ukweli, wafanye utafiti na kuandika mambo
waliyo na uhakika nayo, na kamwe wasikubali kutumiwa kuendeleza agenda
za watu wengine.
MWISHO



No comments:
Post a Comment