Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 22 August 2015

WAJUE WAGOMBEA URAIS 8 UCHAGUZI MKUU 2015!

Edward Lowassa - Ukawa
 Dk. John Magufuli - CCM


Na Daniel Mbega wa brotherdannyblog
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekwishawatangaza wagombea urais wa mwaka huu 2015 ambapo idadi imepungua kuliko ilivyokuwa mwaka 2005.
Jumla yao wapo nane waliokidhi vigezo, huku wanne wengine wakienguliwa kwa kushindwa kutimiza vigezo vinavyotakiwa.
Waliotemwa na NEC ni Mchungaji Christopher Mtikila wa DP, Godfrey Malisa wa CCK na John Lifa Chipaka wa Ada-Tadea ambao fomu zao zilikuwa na kasoro, wakati ambapo mgombea wa chama cha AFP, Omari Sombi, yeye hakurudisha kabisa fomu.
Waliopitishwa, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa NEC Jaji mstaafu Damian Lubuva, ambao sasa tutaanza kushuhudia sarakasi zao majukwaani ni mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Joseph Magufuli, mgombea wa Ukawa Edward Ngoyayi Lowassa, Fahmi Nassoro Dovutwa wa UPDP, Macmillan Lyimo wa TLP, Chifu Lutasola Yemba wa ADC, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Hashimu Rungwe wa Chauma na Malik Kasambala wa NRA.
Ufuatao ni wasifu wa wagombea hao:

FAHMI NASSORO DOVUTWA (UPDP)
Fahmi Dovutwa akiwa na fomu za urais

Huyu ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP). Alizaliwa Kisarawe mkoani Pwani Februari 27, 1957. Rekodi zake za elimu zinaoneysha kwamba alianza elimu yake ya msingi mwaka 1967 katika shule ya msingi Zanaki hadi alipohitimu mwaka 1974 na kuendelea na masomo ya sekondari katika shule ya Azania jijini Dar es Salaam ambako alihitimu mwaka 1977.
Mwaka 2014, alikuwa miongoni mwa Watanzania waliopata fursa ya kuteuliwa na Rais wa Tanzania kupitia kundi la vyama vya siasa, na kuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba lililofanya kazi yake mjini Dodoma na kukamilisha Katiba Inayopendekezwa.
Hakuna rekodi zozote zinazoonyesha harakati zake za siasa hasa kwa kipindi cha miaka 10 kushuka chini, lakini itakumbukwa kwamba mwaka 2010 alijitosa katika mbio za urais kupitia chama chake cha UPDP.
Siku chache kabla ya uchaguzi, Dovutwa alitangaza kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho, lakini licha ya kujitoa huku jina lake likiwa limekosewa, bado aliweza kupigiwa kura na Watanzania na akashika nafasi ya mwisho kati ya wagombea saba waliojitokeza akipata asilimia 0.16 ya kura zote. Wagombea wengine walikuwa Jakaya Mrisho Kikwete wa CCM (asilimia 62.83), Willibroad Slaa wa Chadema (asilimia 27.5), Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (asilimia 8.28), Peter Kuga Mziray wa APPT (asilimia 1.15), Hashim Rungwe wa NCCR (asilimia 0.31), na Mutamwega Bhatt wa TLP (asilimia 0.21).
Mwanasiasa huyu ana mikogo ya aina yake; kuanzia uvaaji wake ambao humtofautisha na wagombea wengine. Lakini tatizo kubwa ni kwamba, anapenda kudandia hoja ambazo hazina mashiko. Halafu ameshindwa kabisa kukitapa uhai chama chake ambacho kipo kama hakipo tu.
Ni miongoni mwa wagombea ambao wataleta nakshi kwenye kampeni za mwaka huu kutokana na mbwembwe zake, ingawa ana changamoto kubwa sana katika siasa za mageuzi.

EDWARD NGOYAI LOWASSA (UKAWA)
Lowassa alipokabidhiwa fomu za urais Chadema

Alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa. Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967. Akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 - 1971, baadaye akaenda Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora alikohitimu  kidato cha sita katika mwaka 1972–1973.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) na baadaye Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.
Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.
Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge kupitia kundi la Vijana ndani ya CCM na akashikilia nafasi hiyo kati ya mwaka 1990 hadi 1995. Mwaka 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.
Mwaka 1995 wakatiwa Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi, Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3. Alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili. Mwaka 1997–2000, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umasikini).
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mifugo hadi mwaka 2005.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.
Uwaziri mkuu wa Lowassa ulikoma Februari 8, 2008, alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond. Kamati Maalumu ya Bunge ya watu watano iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ilisisitiza kuwa wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu ndizo zinazopaswa kubeba lawama ya uingiaji wa mkataba mbovu na Richmond, kampuni ambayo uchunguzi ulionyesha kuwa ni ya mfukoni mwa watu huku Serikali ikilazimika kulipa mabilioni ya fedha katika mkataba ambao una upungufu makubwa.
Baada ya kujiuzulu, Lowassa aligombea ubunge kwa mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na kupata asilimia 90.93 ya kura zote na hadi sasa ndiye mbunge wa jimbo hili japokuwa amekwishaaga kwamba hatagombea tena kiti hicho.
Lowassa alikuwa miongoni mwa wana CCM 17 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 1995 lakini aliyepitishwa ni Mkapa. Mwaka 2005, hakugombea urais ila alikuwa na mipango ya muda mrefu ya kumsaidia rafiki yake, Kikwete na inadaiwa kuwa makubaliano ya Kikwete na Lowassa yalikuwa kwamba mwenzake akishaongoza nchi kwa miaka 10 (yaani 2005 – 2015) atamtengenezea njia 2015 – 2025.
Katika kampeni za ndani ya CCM mwaka huu alikuwa miongoni mwa wanachama 42 waliochukua fomu, lakini akaenguliwa katika hatua za mwanzo tu na kushindwa kuingia tano bora. Ndipo akaamua kujiunga na Chadema na sasa ndiye anaakilisha Ukawa kwenye mbio za urais.
Umaarufu wake na nguvu ya fedha ndivyo vinavyomfanya awe na wafuasi wengi hata kwenye mikutano yake.
Udhaifu wa kwanza wa Lowassa ni kuwa karibu mno na watu wenye majina yenye taswira zinazotia shaka, ndiyo maana anahusishwa na tuhuma za ufisadi hata kama hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa kuhusika kwake. Waingereza wanasema; Ndege wenye mabawa yanayofanana, huruka pamoja. Marafiki wakubwa wa Lowassa ni watu wenye pesa na matajiri, hilo linaweza kumkwamisha katika harakati zake.
Ndiyo maana jamii imegawanyika mno juu yake, wengine wakimuona kama mtu mwenye mipango mingi ya kifedha na mfanyabiashara zaidi kuliko kiongozi wa nchi huku wengine wakimuona kama kiongozi anayethubutu.
Lakini udhaifu wake mwingine ni kwamba hana uwezo wa kuendesha mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kwa sababu wengi kati ya rafiki zake ndio hao wanaotuhumiwa pamoja naye. Atawezaje kuwanyooshea kidole huku akitangaza hadharani kwamba anawapenda?

JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI (CCM)
Magufuli alipoteuliwa na CCM

Alizaliwa tarehe Oktoba 29, 1959 huko wilayani Chato mkoani Kagera (sasa ni wilaya ndani ya Mkoa wa Geita). Alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato mwaka 1967 na akahitimu mwaka 1974. Alifaulu na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke, Biharamulo ambako alisoma Kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 - 1977, akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza ambako alisoma kidato cha Tatu na Nne mwaka 1977 - 1978.
Masomo ya kidato cha Tano na Sita aliyapata mkoani Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981. Baadaye akarudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu; hii ilikuwa mwaka 1981 – 1982.
Baadaye akaenda kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati. Ajira hii aliifanya kati ya mwaka 1982 na 1983, kisha akajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), na kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).
Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988.
Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya shahada ya uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009 ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa shahada ya udaktari. Dk Magufuli ana mke, watoto na familia imara.
Dk. Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alipojitosa katika jimbo la Chato kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda wakati akiwa na miaka 36. Rais Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu.
Uchaguzi wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk. Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na akakaa hapo hadi kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipomalizika.
Mwaka 2005 aligombea  jimboni kwake na akaingia kwenye orodha ya wabunge waliopita bila kupingwa. Rais Jakaya Kikwete akamteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 wana CCM wa Chato hawakuchoka kumpa ridhaa Dk Magufuli, hii ikiwa mara ya nne. Mara hii hakupita bila kupingwa, alipambana na mgombea kutoka Chadema, Rukumbuza Vedastus Albogast ambaye alifanikiwa kumtoa jasho Magufuli.
Katika uchaguzi ule alipata ushindi wa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mgombea wa Chadema. Na baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne, Rais Kikwete akamrudisha katika Wizara ya Ujenzi ambako yuko hadi hivi sasa.
Dk. Magufuli pamoja na kazi nzuri aliyoifanya akiwa waziri katika wizara alizoziongoza, lakini si maarufu katika ‘mitandao’ ya CCM na hata uchukuaji na urejeshaji wa fomu ndani ya chama hicho haukuwa na mbwembwe kama wagombea wengine. Alipoulizwa na wanahabari, yeye alijibu kwamba anasubiri kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Kushinda kwake kulikuwa kama ‘ndondokela’ baada ya kukatwa kwa Lowassa na kupitishwa kwa jina la Bernard Membe – mgombea ambaye alikuwa na ushindani mkubwa na Lowassa. Wajumbe wa NEC, wengi wakidaiwa kuwa wa upande wa Lowassa, wakampa kura nyingi zilizomvusha hadi tatu bora na kuwaengua Membe na January Makamba.
Huku akapambana na wanamama wa shoka, Dk. Asha-Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali, lakini akashinda kwa ‘mafuriko’.
Magufuli ana uwezo wake wa kielimu. Lakini jambo lingine linalompa nguvu, ni kukaa kwa muda mrefu katika wizara zake. Amekuwa Naibu Waziri wa Miundombinu kwa miaka mitano na pia Waziri wa Miundombinu wakati wa Mkapa; akaongoza wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa miaka mitatu kabla ya kuongoza ile ya Uvuvi na Mifugo kwa miaka miwili. Lakini pia tangu mwaka 2010 hadi hivi leo ameiongoza Wizara ya Miundombinu bila kuhamishwa. Jambo hili hulikuti kwa mawaziri wengi sana, hasa katika serikali ya Kikwete. Hii ina maana kwamba anaaminiwa kutokana na utendaji wake. Anafaa!
Huyu jamaa ni makini na ana uwezo wa kusoma na kuchambua nyaraka. Yeye husoma kila jambo na kwamba anatumia muda mwingi sana kusoma kila taarifa na hadi anaweka mistari na michoro kwenye taarifa.
Mhandisi mmoja ambaye amewahi kufungiwa leseni na Magufuli anasema kuwa kosa moja kubwa alilofanya ni kumwandikia Magufuli taarifa ndefu lakini yenye uongo kwenye aya moja. Anasema kuwa aya hiyo ilikuwa iko ukurasa wa 20 lakini ndani ya muda mfupi “Magufuli aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi”. Utendaji huu wa kufuatilia hadi vilivyomo kwenye maandishi ndani kabisa, umewashinda wanasiasa na viongozi wengi, Magufuli anabebwa na jambo hilo.
Tatizo ni moja tu kwa Dk. Magufuli; kufanya maamuzi ya haraka. Mgombea mwenza wake ni Samia Suluhu Hassan na endapo CCM itashinda, itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kuwa na Makamu wa Rais mwanamke.

ANNA MGHWIRA (ACT-WAZALENDO)
Anna Mghwira

Anna Mghwira ni mwenyekiti wa taifa wa chama cha ACT – Wazalendo. Alizaliwa Januari 23, 1959 katika hospitali ya mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao Manispaa ya Singida Mjini. Baba yake mzazi alikuwa diwani na kiongozi wa TANU kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo na ufugaji na wazazi hawa kwa ujumla walijipatia watoto tisa, akiwemo Bi. Anna.
Bi. Anna alianza safari ya kielimu katika shule ya msingi “Nyerere Road” mwaka 1968 – 1974 akaendelea na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka 1975 – 1978 kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya Sekondari (Kidato cha V na VI) Lutheran Junior Seminary kati ya mwaka 1979 – 1981.
Aliendelea na masomo ya Chuo Kikuu mwaka 1982 baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Theolojia (Chuo Kikuu cha Tumaini) na kuhitimu shahada ya Theolojia mwaka 1986.
Mwaka huohuo 1986 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam akitafuta shahada ya Sheria na akaimaliza na kutunukiwa mwaka 1986.
Kati ya mwaka 1987 – 1998, Bi Anna aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, akifanya kazi ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu mkubwa.
Safari ya Elimu ya Bi. Anna ilikamilikia Chuo Kikuu cha Essex nchini Uingereza ambako alianza shahada ya uzamili ya sheria (LLM) mwaka 1999 na kutunukiwa mwaka 2000.
Licha ya kuwa mwanasheria na mtheologia aliyebobea, pia amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu katika uendeshaji wa serikali za mitaa, uzoefu wa utumishi katika mashirika ya kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo amejihusisha na masuala ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za binadamu.
Anna ana historia ya kupenda siasa, masuala ya jamii na michakato ya maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko yake mbalimbali katika majarida na magazeti ya hapa ndani ya nchi.
Alianza siasa tangu wakati wa TANU akiwa ni mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na ushiriki wa juu katika TANU lakini baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza ushiriki wake ili ajipe muda katika masomo na baadaye ndoa na malezi ya watoto.
Kwa kipindi kirefu hakuwa anajihusisha na siasa hadi alivyoamua kujiunga na Chadema mwaka 2009 ambako alishika nafasi mbili tu za Uenyekiti wa Baraza la Wanawake ngazi ya Wilaya na Katibu wa Baraza la Wanawake Mkoa.
Mwezi Machi 2015 alijiunga rasmi na chama cha ACT – Wazalendo na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, yeye ndiye akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza wa ACT.
Bi. Anna aliolewa na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na walibahatika kupata watoto 3 wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha. Hata hivyo kwa bahati mbaya, mume wake hivi sasa ni marehemu.
Bi. Anna Mghwira alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza mwezi Januari 2012 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kifo cha Solomon Sumari.
Anna alishiriki kura ya maoni ndani ya Chadema akihitaji kupewa ridhaa, hata hivyo chama hicho kilimpitisha Joshua Nassari na Bi. Anna alikuwa na kazi ya kuendelea kumuunga mkono hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama hicho.
Pia, amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kupitia Chadema japokuwa hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.
Ndiye mwanamke pekee anayegombea urais safari hii na mgombea mwenza wake ni Hamad Mussa Yusuph. Hata hivyo, mgombea mwenza wa CCM pia ni mwanamke, Samia Suluhu Hassan.

HASHIM RUNGWE SPUNDA (CHAUMA)
Hashim Rungwe

Hashim Rungweni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania akifanya kazi zake kama wakili binafsi. Alizaliwa Januari Mosi, 1949 katika eneo la Ujiji, mkoani Kigoma.
Alianza elimu ya msingi katika shule ya msingi Kipampa iliyoko mkoani Kigoma kati ya mwaka 1959 – 1966 na akajiunga na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Chuo Kikuu cha Cambridge kati ya mwaka 1967 – 1969 na kuhitimu kidato cha nne, kabla ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita hapa hapa Tanzania.
Mwaka 1975 alisoma ngazi ya Cheti katika Taasisi ya Kukuza Mauzo ya Dar es Salaam, mwaka 1977 alisoma Lugha ya Kifaransa kwa ngazi ya cheti katika taasisi ya “Alliance Francais” ya jijini Dar es Salaam na kisha akasoma lugha ya Kiarabu na elimu ya dini ya Kiislamu kwa ngazi ya shahada katika Chuo Kikuu cha Mfalme Abdul kilichoko Saudi Arabia kati ya mwaka 1979 – 1982.
Mwaka 1989 alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ngazi ya Cheti, akichukua masomo ya Usimamizi wa Umma lakini pia mwaka 1991 alisoma ngazi ya cheti hapo hapo Chuo Kikuu, akijikita katika eneo la Historia ya Afrika na Falsafa ya Historia na Masuala ya Maendeleo.
Hashim aliendelea zaidi kielimu alipoamua kubobea katika sheria, alijiunga na Chuo Kikuu Huria Tanzania na kusoma shahada ya sheria kuanzia mwaka 1996 na kuhitimu mwaka 2003 na mwaka huohuo 2003 akasajiliwa kuwa wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa upande wa ajira, Hashim amefanya kazi na mashirika mbalimbali ya ndani ya nchi. Kwa mfano, kuanzia mwaka 1969 hadi 1973 amekuwa ni Ofisa aliyeajiriwa serikalini na kufanya kazi katika idara mbalimbali za sekta ya umma.
Pia, mwaka 1982 hadi leo amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Udalali ya Bahari, lakini pia kuanzia mwaka 1990 hadi leo amejiajiri katika kampuni ya Bahari Motors inayojishughuliza na uuzaji wa magari akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji
Kisiasa, Hashim aliwahi kuwa mwanachama imara wa TANU kati ya mwaka 1966- 1977 na kisha CCM kati ya mwaka 1977 – 1995. Ndiyo kusema kuwa wakati mfumo vyama vingi unaanzishwa mwaka 1992 yeye alikuwa mwanachama wa CCM kwa miaka mitatu zaidi kabla ya kuhamia NCCR Mageuzi mwaka 1996.
Alipokuwa NCCR alishiriki hatua mbalimbali za chama hicho katika kupigania mabadiliko, lakini alijiondoa NCCR mwaka 2012 na kuanzisha chama cha siasa kinachojulikana kama Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na baada ya kuanzisha chama hicho alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mwaka 2014. Ameoa na ana watoto watano.
Mwaka 1995 aligombea ubunge katika Jimbo la Kawe kupitia CCM, lakini akashindwa na Zainudin Adamjee. Mwaka 1996 akahamia NCCR-Mageuzi na mwaka 2005 akagombea ubunge Jimbo la Kinondoni na kushindwa na Iddi Azan wa CCM. Mwaka 2010 akagombea urais kupitia NCCR-Mageuzi akashika nafasi ya tano kati ya wagombea saba na kupata kura 29,638 sawa na asilimia 0.31.

MACMILLAN ELIFATIO LYIMO (TLP)
Macmillan Lyimo

Huyu alizaliwa Januari 29, 1964 katika kijiji cha Kondeni Matala Wilaya ya Moshi Vijijini, katika jimbo la Vunjo, akiwa mtoto wa nne kati ya watoto sita wa familia ya Mwalimu Elifatio Lyimo na mama Elingisongoya.
Alianza elimu msingi katika shule za msingi Kondeni na Kirua kati ya mwaka 1975 na 1978 (darasa la kwanza hadi la nne). Kisha, mwaka 1978 hadi 1979 alisoma katika Shule ya Msingi Sanya Juu katika Wilaya ya Hai. Baadaye akajiunga na Shule ya Msingi Karoro kati ya mwaka 1980 – 1981 alikomalizia darasa la saba.
Macmillan alikuwa mwanafunzi pekee aliyefaulu kutoka kwenye shule zote za Kata ya Mwika Kusini. Baada ya ufaulu huo wa “upweke” alichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Same mkoani Kilimanjaro akafanikiwa kuhitimu mwaka 1985 akipata Daraja la Kwanza (Division I) na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya juu ya sekondari katika mchepuo wa ECA (Uchumi, Biashara na Uhasibu). Masomo haya ya juu ya sekondari (kidato cha tano na cha sita) aliyapata katika Shule ya Sekondari Umbwe iliyoko Moshi Vijijini (1985 - 1988) ambako nako alipata daraja la kwanza (Division I).
Baada ya hapo alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika kambi za Mgambo na baadaye Maramba zote za mkoani Tanga, kisha akahamishiwa makao makuu ya JKT eneo la Mlalakuwa jijini Dar es Salaam mmwaka 1988 – 1989 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia mwaka 1989 alikohitimu Shahada ya Biashara (BCom) mwaka 1993. Katika kujiendeleza kitaaluma, Macmillan alijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) mwaka 1999 – 2004 alikosoma na kutunukiwa Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara (MBA). Tangu mwaka 2013 amekuwa akiendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu Huria Tanzania na hivi sasa yuko katika hatua ya utafiti akitarajia kuhitimu shahada hiyo ya falsafa miaka michache ijayo.
Tangu ahitimu shahada yake ya Biashara, Macmillan hajawahi kuajiriwa serikalini na haamini katika “kuajiriwa na serikali”. Amefanya shughuli za biashara ndogo ndogo kabla ya kufungua kampuni yake binafsi inayojihusisha na masuala ya madini na raslimali za nchi.
Mwaka 2000 aligombea ubunge katika Jimbo la Temeke, Dar es Salaam na akashindwa na Abbas Zuberi Mtemvu wa CCM, mwaka 2010 aligombea ubunge Arusha Mjini lakini akashindwa na Godbless Lema wa Chadema, yeye akishika nafasi ya mwisho akiwa na kura 179 (0.18%)
Mwaka 2010 aliomba ridhaa ya TLP kugombea urais, lakini akashindwa na kada maarufu wa chama hicho Muttamwega Bhatt Mganywa ambaye alipitishwa, akagombea urais na kupata kura 17,482 (0.21%).
Lakini safari hii bahati ilikuwa yake, kwani Aprili 23, 2015 alipitishwa na TLP kuwa mgombea Urais na akawa mgombea wa kwanza kutangazwa na chama cha siasa kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu.

CHIFU LUTASOLA YEMBA (ADC)
Chifu Lutasola Yemba

Huyu hafahamiki katika siasa za Tanzania, lakini ndiye aliyepitishwa na chama chaAlliance fo Democratic Change (ADC) kilichoanzishwa na aliyekuwa Mbunge wa Wawi kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Rashid Mohammed, ambaye alijitoa mwaka 2014.
Hamad, ambaye aliwahi kuwa Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa Bunge la Tisa, yeye anagombea Zanzibar akichuana na Maalim Seif Sharrif Hamad wa CUF na Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM.
Hata hivyo, mgombea mwenza wa Chifu Yemba ni Said Miraji Abdullah, kada maarufu wa zamani wa CUF aliyejiengua pamoja na Hamad.

JANKEN MALIK KASAMBALA (NRA)
Mwanasiasa huyu si maarufu sana katika siasa za Tanzania, hususan za vyama vingi. 
Mwaka 2005 aligombea ubunge katika Jimbo la Ukonga kupitia chama hicho, lakini akashika nafasi ya tano kwa kupata kura 1,186. Mshindi alikuwa Dk. Milton Makongoro Mahanga aliyepata kura 126,955.Lakini chama cha kimemuona anafaa kugombea nafasi ya urais. Tusubiri tuone.

Imeandaliwa na www.brotherdanny.com kwa msaada wa makala za Julius Mtatiro zilizochapishwa kwenye gazeti la Mwananchi.



No comments:

Post a Comment