Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 4 August 2015

LOWASSA RAIS, JUMA DUNI HAJI MAKAMU!

Juma Duni Haji - mgombea mwenza wa Ukawa

Hatimaye kitendawili cha mgombea mwenza wa Ukawa kimeteguliwa baada ya umoja huo kuridhia kwamba Edward Lowassa ndiye atakayekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Hata hivyo, badala ya mchumi Prof. Nguyulu Ibrahim Haruna Lipumba kuwa mgombea mwenza, umoja huo umemteua Juma Duni Haji wa Chama cha Wananchi (CUF) na kuondoa utata kwamba huenda Wazanzibari wangesahaulika.

Juma Duni Haji ndiye makamu wa mwenyekiti wa CUF Zanzibar na ni Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar. Alizaliwa Novemba 26, 1950, Zanzibar.
Alianza elimu katika Shule ya Msingi Mkwajuni mwaka 1959 hadi 1965 kisha akajiunga na Shule ya Sekondari Gamal Abdel Nassar (siku hizi inaitwa “Beit el Ras”) mwaka 1966 na kuhitimu mwaka 1969.
Duni aliendelea na sekondari ya juu (kidato cha tano na sita) katika Chuo cha Lumumba, Zanzibar kati ya mwaka 1970–1971. Wakati akisoma Sekondari ya Beit el-Ras na Sekondari ya Lumumba, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa ASP.
Duni alidahiliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma Shahada ya Sayansi katika Elimu (BSC Education) kati ya mwaka 1972 hadi 1975.
Baada ya kuhitimu shahada ya kwanza, aliajiriwa kama mwalimu wa Sekondari ya Beit Al Ras, wakati huo ikiitwa Gamal Abdil Nassir (jina la Rais wa zamani wa Misri), na baada ya mwaka mmoja akahamishiwa Sekondari ya Lumumba na kufundisha kidato cha tano na sita na baadhi ya wanafunzi wake ni “magwiji” wa siasa za Zanzibar; Ismail Jussa, Thuwayba Kisasi na wengineo.
Mwaka 1978–1979, Duni alikwenda masomoni Uingereza, akasoma na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Reading na aliporejea alihamishiwa Ofisi Kuu ya Wizara ya Elimu na kupewa wadhifa wa Ofisa Mipango ya Elimu.
Duni alipata mafunzo mengine muhimu ya kitaaluma nchini Nigeria mwaka 1980 juu ya Mipango ya Elimu na mwaka 1982 alipelekwa Japan kujifunza kwa kina Mipango ya Kiuchumi.
Pia, Mwaka 1980 Rais Aboud Jumbe, alimteua Juma Duni kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango (Zanzibar) na baadaye kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango (Executive Secretary Planning Commission).
Duni alianza safari ya kisiasa kwa “kulazimishwa” mwaka 1984, baada ya serikali ya Muungano kutoa Waraka wa Serikali (white paper) na kutakiwa wananchi watoe maoni yao juu ya hali na matatizo ya Muungano.
Makatibu wakuu wa Serikali ya Zanzibar ya wakati huo akiwemo yeye walitoa maoni dhidi ya muungano, uhuru huo wa kitaalamu uligeuzwa kuwa mchungu kwani walisingiziwa kwamba wamefanya kinyume na walivyoagizwa na baadhi yao wakapewa onyo kali na wengine wakateremshwa vyeo.
Duni aliteremshwa cheo kutoka wadhifa wa Katibu Mkuu hadi mwalimu wa kawaida kwa Tangazo la Rais, akatakiwa kwenda kufundisha Shule ya Mikunguni.
Mwaka mmoja tangu aanze kufundisha Mikunguni akaambiwa anashiriki siasa hapo shuleni na kuwatia kasumba chafu wanafunzi wa shule hiyo na hivyo akahamishiwa Shule ya Lumumba.
Baada ya muda mfupi huko Lumumba nako akahamishwa na kurudishwa Ofisi Kuu ya Elimu kama Ofisa Mipango wa Elimu. Akiwa Ofisa Mipango alituhumiwa kuwa anakwenda nyumbani kwa Maalim Seif Sharrif usiku wa manane kufanya siasa na ikaipasa serikali imhamishie Idara ya Ukaguzi.
Kwenye idara ya ukaguzi nako akaambiwa anafanya siasa kwa kutoka saa za kazi na kukaa kwenye vibaraza (vijiwe), akarejeshwa tena Ofisi Kuu na huko akaambiwa kwamba anaondoka kwenda Dar es Salaam bila kuaga kwa wakubwa zake na mara nyingi ameonekana usiku akifanya siasa na Marehemu Abrahman Babu (ambaye wala hakuwepo Zanzibar wakati huo).
Wizara ilipomchoka na kukosa cha kumfanya ikamrejesha kwa Mkurugenzi Mkuu wa Utumishi ambaye hakuwa na kazi ya kumpa, sana sana alimwambia abaki nyumbani bila kazi kwa zaidi ya miezi sita.
Baadaye, mkurugenzi wa utumishi akamrejesha tena Wizara ya Elimu baada ya Duni kuwauliza kosa lake na kushindwa kumueleza.
Duni alipoona visa hivyo vinamuumiza na vinamchosha aliomba ruhusa ya likizo bila malipo kwenda kusoma, ombi ambalo nalo pia lilikataliwa na ndiyo akaamua mwenyewe kuondoka na kwenda kujisomesha kwa fedha zake Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza na kuhitimu stashahada ya Juu ya Biashara kati ya mwaka 1993-1994.
Wakati alipofika Uingereza akatumiwa barua ya kuachishwa kazi na kupoteza haki zake zote za miaka 18 ya utumishi serikalini. Mwaka huo 1994 akiwa bado nchini Uingereza, akaunganisha tena kwa shahada ya uzamili/umahiri akibobea kwenye usimamizi wa Rasilimali Watu na kabla hajaihitimu akarejea nchini ili kusaidia upinzani kujipanga kiuchaguzi.
Moja kwa moja akajiunga na vuguvugu la uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi. Chama Cha Wananchi (CUF) kikamteua kuwa Mgombea mwenza wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba wakati bado hajakamlisha shahada yake ya pili ya uongozi na utawala.
Tangu ajiunge CUF ameshika nyadhifa mbalimbali kwa nyakati tofauti, amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar na Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha CUF Taifa mwaka 1999–2003, amekuwa Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha CUF kati ya mwaka 1997-2010, amekuwa Naibu Katibu Mkuu CUF (Zanzibar) kuanzia mwaka 1999-2010, Amekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa CUF Taifa kati ya mwaka 1999-2014.
Hivi sasa yeye ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, nafasi aliyochaguliwa mwaka 2014 na analazimika kuishikia hadi uchaguzi mwingine wa ndani ya chama chake utakapofanyika, mwaka 2019.
*Nyongeza ya makala haya chanzo ni gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment