Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 4 July 2015

UONGOZI CCM NI 'ZABUNI', HUNA FEDHA KAFIE MBELE!


Na Daniel Mbega
“RUSHWA ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa!” Hii ni ahadi namba 6 miongoni mwa Ahadi 10 za Mwana-TANU ambazo zilirithiwa na Chama cha Mapinduzi inayosisitiza kwamba mtu yeyote anayepewa uongozi hapaswi kuutumia kwa maslahi yake binafsi bali kwa maslahi ya wote.
Ahadi hii na nyinginezo zilikuwa zikiimbwa kila mahali kuanzia shule ya msingi, sekondari na vyuo vikuu ambako somo la Siasa lilianzishwa na serikali ya TANU na kuendelezwa na CCM kabla ya kufutwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Vijitabu vingi vya TANU na Azimio la Arusha vilikuwa vimesambazwa ambapo kila mjumbe wa nyumba kumi kumi alikuwa navyo vya kutosha kuwagawia wananchi wake ili waweze kuelewa wajibu wao na siasa kwa ujumla na kuhamasisha Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo sasa imezikwa na wajanja wachache walioamua kuukumbatia ubepari kwa kisingizio cha Soko Huria, ambalo limekuwa soko holela!
Kabla ya kujiunga na Chama (TANU na baadaye CCM) ulitakiwa kuziimba na kuziahidi kwa dhai ahadi hizi ili utakapotenda kinyume cha hapo ujipime mwenyewe na itakapobidi uchukuliwe hatua stahiki.
Hizi zilijenga misingi imara ya uongozi, utii, uadilifu na uzalendo kwa Taifa letu. Ndiyo maana watu waliokula kiapo hiki walikuwa na uzalendo wa kweli na walilipenda Taifa na watu wake na walijitolea kwa dhati kulitumikia. 

Hebu ziangalie mwenyewe ahadi hizi: 
i. Binadamu wote ni ndugu zangu na Dunia ni moja 
ii. Nitaitumikia nchi yangu na binadamu wenzangu wote kwa unyenyekevu na moyo wa upendo na huruma 
iii. Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, maradhi, na dhuluma hapa nchini na duniani pote. 
iv. Rushwa ni adui wa haki, sitatatoa wala kupokea Rushwa. 
v. Cheo ni dhamana. Sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu. 
vi. Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote. 
vii. Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu na dunia yenye haki na amani. 
viii. Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. 
ix. Nitakuwa raia mwema wa Tanzania, Afrika na Dunia nzima. 
x. Nitakuwa mtii kwa Raisi na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania. 

TANU (na baadaye CCM) iliamini binadamu wote ni sawa na kusisitiza raia wote kwa pamoja wamiliki utajiri wa asili wa nchi hii ukiwa kama dhamana kwa vizazi vyao; na Kwamba ni wajibu wa Serikali, ambayo ni watu wenyewe, kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi ya Taifa ili kuhakikisha usitawi wa raia wote na kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine na kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani na siasa ya watu wote kuwa sawa.
Tunaelezwa bayana kwamba TANU (sasa CCM) ni chama cha wakulima na wafanyakazi (Jembe la Mkulima na Nyundo ya Mfanyakazi) na ikasisitiza katika katiba yake kwamba, Serikali lazima itumie mali yote ya nchi yetu kwa kuondoshea umaskini; ujinga na maradhi;
Kuona kwamba Serikali inaondoa kila namna ya dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa na upotofu; na Kuona kwamba Serikali ya nchi yetu inasimamia barabara njia kuu za kuzalisha mali na inafuata siasa ambayo itarahisisha njia ya kumiliki kwa jumla mali za nchi yetu.
Njia kuu za uchumi ambazo zinapaswa kuwa chini ya wakulima na wafanyakazi ni pamoja na ardhi, misitu, madini, maji, mafuta na nguvu za umeme; njia za habari, njia za usafirishaji; benki, na bima; biashara na nchi za kigeni na biashara za jumla; viwanda vya chuma, mashini, silaha, magari, simenti, mbolea; nguo, na kiwanda chochote kikubwa ambacho kinategemewa na sehemu kubwa ya watu katika kupata riziki zao au kinachotegemewa na viwanda vingine; mashamba makubwa na hasa yale yanayotoa mazao ya lazima katika viwanda vikubwa.
Suala la mgawanyo wa mali za umma limekuwa kitendawili kigumu kuteguliwa hasa baada ya kushuhudia namna viongozi wa chama na serikali wanavyozitafuna mali za umma, wakijali zaidi matumbo yao kuliko ya Watanzania licha ya kuwepo kwa maadili ya uongozi ambayo nayo yameendelea kubaki kwenye makaratasi na kufungiwa kabatini huku agizo la kutenganisha biashara na siasa likiwa ni shairi lisilo na vina!
Viongozi hawa ambao wanaagizwa na chama kwamba ‘Cheo ni dhamana’, pamoja na kubadili mfumo wa siasa kutoka Ujamaa kuja kwenye Ubepari, bado wanashindwa kufuata maadili sahihi ya uongozi, yakiwemo kutojilimbikizia mali kwa kutumia vyeo vyao, kutaja mali zao kabla ya kuingia madarakani na baada ya kutoka, badala yake wanaendelea kuchota mali za umma kadiri wapendavyo huku wananchi wakiendelea kuogelea kwenye umaskini.
Kila kiongozi anayeingia madarakani kwa sasa anaangalia kwanza tumbo lake, na kadiri siku zinavyosonga hupata tamaa ya kuchota zaidi na zaidi na mwishowe huona kwamba ni haki yake kuwa tajiri huku wengine wakiendelea kupiga miayo bila kuwa na uhakika hata wa kipande cha muhogo kushibisha tumbo kwa mlo mmoja.
Chama hiki ambacho tulitegemea kingeleta na kuendeleza mapinduzi ya kweli kwa kila Mtanzania, leo hii si chama cha wakulima na wafanyakazi kama tulivyoelezwa enzi zile za Mwalimu.
Tangu tulipopata uhuru wetu Desemba 9, 1961 Serikali ya Awamu ya Kwanza ilihimiza lazima kusiwe na tabaka mbili: tabaka ya chini ya watu wanaoishi kwa kufanya kazi, na tabaka ya juu ya watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi.
Yale yaliyokatazwa, hasa ya kuweka matabaka baina ya matajiri na maskini, leo hii siyo jambo geni ndani ya CCM ambayo imefuta kabisa dhana ya mkulima na mfanyakazi kuwa muhimili wa chama.
CCM kimekuwa chama cha mabwanyenye ambao kila siku ama wanafikiria namna ya kuingia madarakani au jinsi ya kuendelea kuchota na kukalia madaraka hata kwa kuzivunja zile ahadi za chama, ikiwemo kutumia rushwa ingawa midomoni mwao wanaimba kuwa ‘rushwa ni adui wa haki’, tena wengine wanaongeza kwamba ‘ni dhambi’!
Watazame wagombea urais wa mwaka huu kupitia chama hicho! Wengi wameoza, wananuka uvundo wa rushwa na ufisadi. Hawatakati kwa kiwi wala sabuni!
Rushwa inanuka CCM. Wanachama nao wamelambishwa shubiri, hawaoni kama ni chungu, bali wanasema tamu kama asali. Matokeo yake wanatamba lazima mtu atoe kitu apate kitu!
Utiriri wa wagombea wote hawa unaonyesha kwamba chama kimesambaratika. Hakuna hata mmoja anayeweza kukijenga upya. Kila mtu anangalia kambi gani yenye maslahi. Akiingia huko ataimba mapambio bila kukoma. Hakika rushwa imelibomoa Taifa.
Kupata uongozi ndani ya chama hivi sasa watu hawaangalii sifa, wanaangalia uko kwenye ‘mtandao’ wa nani na umetenga fungu kiasi gani. Uongozi ndani ya CCM ni zabuni, hivyo mwenye fedha – hata kama hana sifa – ndiye atakayeshinda huku maskini wenye sifa za kuongoza wakitelekezwa.
Nani ajisumbue kuangalia maadili na uadilifu wa mtu? Nani anayeangalia mtu sahihi atakayewaongoza mamilioni ya Watanzania wavuke katika dimbwi la ufukara? Hakuna! Lakini kwa kuwa uongozi ndani ya chama hicho umekuwa kama ‘zabuni’, basi wanaangalia nani aliyetoa ofa kubwa ndiye anayeshinda.
Majuzi tu tumemsikia Balozi Amina Salum Ali, mmoja wa watia nia ya kuwania urais, akilalamika kwamba ameshindwa kutimiza idadi halisi ya wadhamini katika baadhi ya mikoa kwa sababu alipokwenda walimweleza wazi: “Wenzako wametoa kiasi Fulani, wewe unatoa kiasi gani?”
Hili lilimfanya mwanadiplomasia huyo wa kimataifa, ambaye namheshimu sana, alalamike kwamba tangu amekuwepo kwenye chama hicho kwa zaidi ya miaka 35 ndiyo kwanza anakumbana na kadhia hiyo. Ni aibu!
Hakuna mwenye ujasiri wa kumkemea mwenzake kwa sababu hata yeye naye aliingia kwa njia hizo hizo!
Wanapotokea watu wenye ujasiri wa kusema, kama ilivyo kwangu mimi, wapo baadhi, badala ya kuutambua ukweli na kujirekebisha, wanaanza kujenga chuki na kuwaona hao wanaosema kama ndio wabaya, wametumwa, wachochezi na mambo mengine kama hayo. Muungwana ukivuliwa nguo, chutama!
Kwa nini uwazi haupo sasa ndani ya CCM? Kwa nini watu wanaogopa kukosoana kwenye chama hiki kilichojenga misingi imara hata kwa vyama vingine vya ukombozi Kusini mwa Afrika? Kama wenyewe hawakubali kukosolewa, itawezekana vipi wakaenda kuwakosoa wengine nje ya nchi? Umakini ule umetoweka.
Ukitazama mchakato wa kura za maoni kwa mwaka 2010 ndani ya chama hicho utaamini kwamba CCM ni Chama cha Matajiri, si Chama cha Mapinduzi kama ambavyo tunaimba midomoni. Wengi ni wanafiki na wazandiki wakubwa na wameanza kuitumbua nchi mara tu baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kufariki dunia mwaka 1999.
Mtanisamehe sana kwa kutumia lugha kali na nitumie nafasi hii ku-declare interest. Nimezaliwa enzi za TANU, nikajifunza misingi ya TANU kabla hata ya kuanza shule, nikalelewa wakati wa CCM yenye hekima, ni mfuasi mkubwa wa falsafa za Mwalimu na ndiyo maana niliona fahari kupiga kwata la chipukizi kwa miezi mitatu kujiandaa na maadhimisho ya miaka 10 ya Chama pale Dodoma mwaka 1987.
Napata hasira ninapowaona wachache wakikiharibu Chama wapendavyo. Wamekuwa kama makambare ndani ya dimbwi la maji. Hujui baba ni nani; mama ni nani wala mtoto ni nani, maana kila mmoja ana ndevu!
Ukiwachungulia baadhi ya walioshinda kura za maoni 2010 na hatimaye Ubunge na Udiwani utakutana na majina ya watu ambao wanasifika ndani ya jamii yetu kwa mambo maovu, yakiwemo ya ujambazi na ukwepaji wa kodi kwenye biashara zao, nyingi zikiwa hazifahamiki sawasawa.
Kwa ujumla, utakutana na wafanyabiashara wengi ambao wanatajwa kwamba wamepata nafasi hiyo kutokana na ‘kushinda zabuni ya uongozi’ na ‘mchango wao kwa chama’, hasa fedha, bila kujali misingi iliyounda chama hicho kikongwe zaidi barani Afrika, na pekee ambacho kinaendelea kusimama imara ingawa kwa sasa kimeyumba.
Kuibuka kwa wagombea wengi mwaka 1995 kulimpagawisha Mwalimu Nyerere, ambaye aliamini hiyo haikuwa demokrasia tena bali chama kilikuwa kimevamiwa na kwamba kilikuwa na viongozi ‘wabaya’, ambao dhahiri aliwaona walikuwa na nguvu na wangeweza kupitishwa na chama kushika madaraka ya nchi.
Nyerere aliona chama kilikuwa kimevamiwa na watu wenye fedha, ambao walikuwa tayari kumsimika ‘mtu wao’ kwa kutumia fedha hizo ambazo Mwalimu aliziita ‘fedha za bhangi’, akimaanisha zilikuwa fedha chafu ambazo hata upatikanaji wake ulikuwa wa njia zisizo halali ndiyo maana walikuwa tayari kuzitumiza watakavyo ili kulinda ‘maslahi’ yao.
Akawaponda wagombea wengine waliokuwa kwenye mchakato huo akisema; “Mnakimbilia Ikulu, Ikulu kuna biashara gani pale? Mnataka kwenda kufanya nini Ikulu? Ikulu ni mahali patakatifu, si mahali pa mchezo mchezo pale. Ni mahali pa kuheshimika!”
Kusema ukweli, CCM ya sasa imebaki na katiba tu, ndani yake hakuna wanachama wenye katiba ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, kwa sababu misingi aliyoiacha imebomolewa na kuigeuza rushwa kuwa ni sehemu ya uamuzi ndani ya Chama hicho.
Watu wenye fedha, haijalishi kama ni za halali au za ‘bhangi’, ndio wenye sauti kwenye chama.
Leo hii mtu akipata ujasiri wa kuhoji ni wapi matajiri hawa ‘wanaoisaidia CCM’ ataonekana katumwa ama anatumiwa.
Kwa bahati nzuri, sisi tunapenda kuona Tanzania inaendelea na wananchi wananufaika na matunda ya rasilimali zao, hivyo hatuna budi kukikosoa chama ili kijirekebishe kwa kuwa kwa sasa ndicho kilicho madarakani na kinasimamia rasilimali zetu.
“Hiyo nitasema aaah, mwanaCCM weeeeeee......Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko!”

0656 331974


NB: MAKALA HAYA YAMEHARIRIWA, LAKINI YALICHAPISHWA KWA MARA YA KWANZA KATIKA GAZETI LA UCHUNGUZI LA ‘WAJIBIKA’ LA JUNI 29, 2015.

No comments:

Post a Comment