Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 8 May 2015

RAIS KIKWETE KUJITOSA KUHIFADHI WANYAMAPORI

Miongoni mwa matatizo hayo ni lile lililoelezwa kuwa katika kipindi cha mwaka 1966 na 1992 walitoweka mbwamwitu wengi katika hifadhi hiyo na wengine wakihamia  Hifadhi ya Ngorongoro na Maasai Mara nchini Kenya. 
Na Anthony Mayunga, Mwananchi
Mbwamwitu ni miongoni mwa  wanyamapori waliopo kwenye mkakati wa kuokolewa kutokana na hatari ya kutoweka kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kubainika kuteketea kwa wanyama hao kuliibua utata kuhusu kilichosababisha tatizo hilo.
Miongoni mwa matatizo hayo ni lile lililoelezwa kuwa katika kipindi cha mwaka 1966 na 1992 walitoweka mbwamwitu wengi katika hifadhi hiyo na wengine wakihamia  Hifadhi ya Ngorongoro na Maasai Mara nchini Kenya.
Hata hivyo, watafiti wa mambo ya wanyamapori wakasema kuhama huko siyo sababu kuu inayoweza kutumika kama kigezo cha kupungua kwa mbwamwitu katika Mbuga ya Serengeti.
Sababu nyingine zikaelezwa ni magonjwa kwa wanyama walao nyama kama vile simba, dumu na chui.
Sababu nyingine ikatajwa ni kuwapo kwa mabadiliko ya tabianchi na uoto wa asili na misitu kwa ujumla inapotea na matokeo yake wanyama wanashindwa kupata hifadhi pamoja na chakula.
Sababu nyingine zinazozungumziwa ni huenda kumekuwapo kwa hujuma kutoka kwa watafiti wa nje wa wanyama hao. Hii ni kutokana na maelezo kuwa ongezeko la watafiti linakwenda sanjari na kupungua kwa wanyama hao.
Hata hivyo, ripoti za karibuni zinaonyesha chanzo ni migogoro kati ya jamii ya wafugaji na wanyama hao katika maeneo ya Loliondo.
Mbwamwitu walikuwa wanaelekea kuisha katika hifadhi hii, waliokuwa eneo la Loliondo walianza kuuawa kwa sumu kutokana na migogoro na wafugaji.
Sababu za kuwaua zinaelezwa kuwa ni kutokana na wanyama hao kushambulia na kuua mifugo kama vile mbuzi na kondoo.
Hakukuwapo na jumuisho la moja kwa moja la sababu lakini Taifa likaona kuna umuhimu wa kukoa kizazi cha wanyama hao.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa Allan Kijazi anasema kutokana na umuhimu wa wanyama hao shirika limekuwa likijitahidi kuwakamata na kuwahifadhi eneo maalumu ili waendelea kuzaliana.
Miongoni mwa wadau waliojitokeza kwenye mpango huo wa kukabiliana na kupungua kwa mbwamwitu ni Rais Jakaya Kikwete.
“Ni aibu wanyama hawa muhimu kwa utalii kutoweka kisha baadaye tuwatafute kwa gharama kubwa… Mimi niko tayari kusaidia wanyama hawa wasipotee,” anasema Rais Kikwete.
Anasema ili kufanikisha kazi hiyo, sasa wanatakiwa kuanzisha mfuko maalumu wa uhifadhi ambao utachangiwa na watu wa ndani na nje ya nchi, lengo ni kulinda wanyama walio katika hatari ya kutoweka na yeye atasimamia hilo.
Katika kuunga mkono juhudi hizo za Kikwete, Kijazi anasema kuwa Tanapa ipo tayari kuchangia mfuko huo ili kuunga mkono juhudi za Rais Kikwete ili kuongeza wanyama hawa maana walikuwa katika hatari ya kutoweka.
Kijazi anasema kupungua kwa fisi siyo tu kwa Hifadhi ya Serengeti bali hata maeneo mengine, yakiwamo mapori ya akiba.
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Ernest Manongi anasema mradi huo umesaidia ongezeko kubwa la wanyama hao na utakuwa endelevu ili kuhakikisha historia ya wanyama hao inajirudia.
JK akistaafu kusaidia uhifadhi
Rais Kikwete anasema licha ya sasa kujitosa katika kuongeza nguvu ili kukoa mbwamwitu wasiteketee katika hifadhi za wanyama pori, hata baada ya kustaafu ana mpango wa kuendeleza juhudi hizo.
“Kazi niliyoamua kufanya sasa na baada ya kuacha urais ni kusaidia uhifadhi,” anabainisha Rais Kikwete, huku akiahidi kumhimiza rais ajaye kuweka msisitizo wa kipekee katika kulinda uhifadhi.
Isitoshe anasema hata wahisani mbalimbali wa nje wako tayari kusaidia juhudi za kulinda uhai wa wanyamapori, hivyo akasema Watanzania hawana budi nao kuonyesha juhudi zao katika kulinda rasilimali hii muhimu kwa Taifa.
“Ukibebwa, shikilia usijilegeze, tunahitaji kupambana kweli kuokoa wanyama hawa,” anasisitiza Rais Kikwete ambaye anatarajia kumaliza kipindi chake cha miaka 10, cha kuiongoza nchi, Oktoba mwaka huu.
Rais Kikwete anasema sekta hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Taifa na vizazi vijavyo, hivyo kuyataka mashirika makubwa kama Tanapa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuanza kuchangia mfuko huo.
Mradi rejesha mbwamwitu
“Mwaka 2005 Tawiri kwa kushirikiana na Serengeti Wild Dog Conservation Project na Frankfurt Zoological Society, tulianzisha mradi wa kuwakamata mbwamwitu huko Loliondo na kuwahifadhi ili waweze kuongezeka katika Ikolojia ya Serengeti,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk Saimoni Mduma.
Anasema walianzisha mradi wa kuongeza idadi ya mbwamwitu mbugani, lengo lilikuwa ni kuwakama kwa awamu ili kuwahifadhi maeneo maalumu.
“Tayari tumefikisha kundi la tano, idadi tuliyokuwa tumepanga kwa makundi sita ya kuhifadhi na baadaye kuwaachia.
“Mradi utaendelea kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ikiwemo wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro,” anasisitiza.
Mtafiti wa Wanyama Taasisi ya Wanyamapori Tanzania (Tawiri), Joseph Masenga anaongoza mradi wa kurejesha mbwamwitu maeneo yanaoonekana wamepungua. Yeye anasema jitihada za kuwarudisha mbwamwitu, ambao ni muhimu katika sekta ya Utalii na uhifadhi, zinafanywa na wadau mbalimbali, akiwamo Rais Kikwete.
Mratibu wa mradi huo Dk Ernest Mjingo anasema miongoni mwa makundi yaliyokuwa yamehifadhiwa, tayari yamerejeshwa na kuanza kuonyesha uhai wa wanyama hao mbugani.
Anataja miongoni mwa yale yaliyorejesha uhai wa idadi ya mbwamwitu mbugani ni kundi lililokuwa linahifadhiwa na Rais Kikwete na baadaye kuachiwa.
Kundi hilo maarufu kama Kikwete Pack liliachiwa Desemba 23, 2012, wakiwa 15 na hadi sasa limezaliana mara tatu.
Baada ya kuachiwa, kundi hilo linaelezewa liligawanyika makundi mawili, lingine likienda Makoma Hill, Sopa Valley, Moru, Nyaruboro hill hadi maeneo ya Simiyu. Kundi lingine lenye Mbwamwitu watano lilitoka Kusini Mashariki, Osinoni, Kakesiohadi katika Pori la Akiba la Maswa.
Tabia za mbwamwitu
Wataalamu wa hifadhi za wanyama pori wanasema unapomhifadhi fisi unakabiliwa na changamoto nyingi mbali na gharama za kumlisha.
Wanasema ukiwakaribia hukutishia kukung’atana wakati mwingine hubweka usiku kucha. Hatari huwa kubwa zaidi wakati wamezaa kwa kuwa huwa wakali, hasa dume ambalo wakati huo hulisha jike. Mbwamwitu hubeba mimba kwa miezi mitatu na huzaa watoto kuanzia 10 hadi 12. Chakula chake kikuu ni ni nyama kilo tatu hadi nne kwa siku.
Wakati mwingine hula majani kama dawa. Wanyama hawa ni mhimili katika uhifadhi kwa kuwa ni rasilimali ya nchi.
Wawapo mbugani, hutembea kifamilia na wana uwezo wa kuwinda kwa kushirikiana na hata kukabiliana na adui kwa umbali mrefu. Hufanya hivyo kwa mtindo wa askari wawapo vitani.
Hivyo jamii inatakiwa kushirikiana na wahifadhi kuwadhibiti wanapokula mifugo na siyo kuwaua kwa kuwa gharama za kuwatunza ni kubwa.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment