Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 10 May 2015

KUMBUKUMBU ZANGU: MISIMU MITANO YA KIHORO YA LIGI TANZANIA BARA

Mashabiki wa Yanga wakishangilia ushindi wa timu yao. (Picha kwa hisani ya Sufianimafoto)

NA DANIEL MBEGA
JAMVI la Ligi Kuu Tanzania Bara limekunjwa rasmi jana Jumamosi Mei 9, 2015 ambapo tayari mashabiki walikuwa wamejua nani bingwa pamoja na mwakilishi mwingine wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa.

Yanga ndiyo imeibuka bingwa msimu huu ikiipoka Azam FC, lakini pia ikitumia mbeleko yake kuibeba timu hiyo ya ‘Wana Lamba Lamba’ na kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika huku Simba ikibaki kushangaa.
Kabla ya mechi za mwisho, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Emil Malinzi alitoa tahadhari na kuwaagiza wasimamizi wa vituo vya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuhakikisha sheria na taratibu zote za mechi zinafuatwa.
Timu zote 14 zinazoshiriki ligi hiyo jana zilikuwa viwanjani kukunja jamvi hilo. Mabingwa wateule Yanga walikuwa ugenini wakicheza na Ndanda katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, JKT Ruvu zilipepetana na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Azam walikuwa nyumbani kwao Chamazi wakikamilisha ratiba na na Mgambo Shooting, Wapiga debe Stand United walikuwa wenyeji wa Ruvu Shooting pale kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Kagera Sugar waliwakaribisha maafande Tanzania Prisons katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Mbeya City na Polisi Morogoro ziliumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya, na Mtibwa Sugar na Coastal Union zikapambana kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Hofu iliyokuwepo ni kuhusu timu ambazo zilikuwa zinapigania kushuka daraja kwamba huenda zingepanga matokeo, jambo ambalo wakati mwingine hutokea, japokuwa siyo la kiungwana katika mchezo wa soka.
Yanga ilimaliza ngwe kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Ndanda, Simba ikaifunga JKT Ruvu 2-1, Azam ikatoka suluhu na Mgambo, Mtibwailiyoanza kuongoza ligi ikakubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Coastal, Mbeya City nayo ikaikanyaga Polisi bao 1-0, Stand United ikawachapa maafande wa Ruvu Shooting bao 1-0 na maafande wa Magereza, Prison wakawalazimisha suluhu Kagera Sugar.
 Kwa mantiki hiyo, Ruvu Shooting na Polisi Morogoro hazitashiriki Ligi Kuu msimu ujao baada ya kushuka daraja kwa kushika nafasi za mwisho.
Huu ulikuwa msimu mgumu, lakini si kama misimu mitano iliyopata kutokea huko nyuma.
Tuliwahi kushuhuria katika historia ya Ligi Tanzania Bara kwamba bingwa alishindwa kujulikana hadi siku ya mwisho, mara ya kwanza ikiwa mwaka 1986 wakati Tukuyu Stars ilipotwaa ubingwa kwa ngekewa kutokana na sare ya mabao 2-2 na Coastal Union mjini Tanga. Washukuru bao la kusawazisha la dakika ya 84 lililofungwa na John Alex.
Katika msimu wa 1987 ambao Yanga ilitwaa ubingwa wake wa 10, hadi ligi hiyo inafika ukingoni Septemba 19 bingwa alikuwa hajajulikana huku Yanga na Pamba zikifukuzana zote zikiwa na pointi 21 na ziliombeana mabaya kwa mmoja kupoteza.
Yanga ilicheza na Maji Maji mjini Songea na Abeid Mziba ‘Tekero’ akaipatia bao pekee la ushindi, wakati Pamba nayo iliikaribisha Nyota Nyekundu na kushinda bao 1-0 pia lililofungwa na Hamza Mponda. Zote zikafikisha pointi 23.
Ikabidi iangaliwe tofauti ya mabao ya kufunga na Yanga ikaibuka bingwa baada ya kuwa imefunga mabao 20 na kufungwa 10, wakati Pamba ilifunga mabao 18 na kufungwa 9.
Ni msimu uliokuwa mbaya kwa Simba ambayo ilinusurika kushuka daraja kama sis are yake ya ‘kupangwa’ ya mabao 5-5 na Tukuyu Stars kwenye Uwanja wa Taifa ambayo iliipa pointi na mabao muhimu zaidi kushika nafasi ya nne kutoka chini huku Nyota Nyekundu iliyokuwa na mabao 15 ya kufunga ikiteremka daraja licha ya kuwa zote zilikuwa na pointi 17. Simba ilifikisha mabao 19.
Msimu wa 1988 ambao ulikuwa na neema kwa timu za Tanga, nao ulikuwa na kihoro mwishoni kutokana na bingwa kutojulikana mapema. Coastal Union ilisubiri hadi jioni ya Julai 23 kufahamu kwamba kumbe ilikuwa imepata ubingwa wa kwanza, huku ikiwa inaugulia kwa kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa mahasimu wao African Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Wengi walisema hizi zilikuwa njama za Yanga, ambayo kihistoria inatajwa kuwa na uhusiano mzuri na African Sports, kutaka Coastal ifungwe na wao watwae ubingwa, lakini vijana wa Jangwani wakajikuta wakichapwa mabao 2-1 na Simba, ambayo kwa hakika kama si ushindi huo ulioelezwa kwamba ulikuwa wa ‘kulindana wazee’, ingeshuka daraja.
Simba ilimaliza msimu huo ikiwa ya tatu kutoka mkiani kwa pointi zake 20 ikizipisha Tukuyu Stars na Reli kushuka daraja.
Coastal ilitwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga, kwani ilikuwa na pointi 26 sawa na Yanga na African Sports, lakini ilipachika wavuni mabao 26, Yanga ilikuwa na mabao 24 na Sports mabao 23.
Mwaka 1991 nao ulikuwa mgumu ingawa Yanga ilifanikiwa kutwaa ubingwa, huku ikishinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Maji maji kwa mabao 3-1 mjini Dar es Salaam, na mabingwa watetezi, Simba wakilazimishwa sare ya 2-2 na Ushirika Septemba 21.
Mbaya zaidi ilikuwa kashfa ya ‘kupanga matokeo’ katika mechi hiyo ya mwisho ambapo Coastal Union, ikililia kucheza Ligi ya Muungano na kuipiku Reli ya Morogoro, iliamua kuishushia kipondo Mecco ya Mbeya cha mabao 9-2.
Mecco ilikuwa imeshuka daraja, na kwa uwezo wake ambao uliifanya ikaishinda Coastal mabao 2-0 katika mzunguko wa kwanza, Chama cha Soka Nchini (FAT) na wadau wengine waliona dhahiri kwamba hiyo ilikuwa ni njama. Matokeo hayo yakafutwa.
Tusubiri tuone msimu mpya utakuwa na matokeo ya aina gani.


No comments:

Post a Comment