Pages

Pages

Pages

Wednesday 8 April 2015

MITI 300,000 KUPANDWA MLIMA KILIMANJARO


Na Rehema Matowo, Mwananch
Moshi. Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utunzaji wa mazingira mkoani Kilimanjaro (Teaca) limelenga kupanda miti zaidi ya 300,000 katika maeneo yanayozunguka mlima Kilimanjaro, lengo likiwa ni kurudisha uoto wa asili uliopotea.
Makamu Mwenyekiti wa shirika hilo, Adoncome Mcharo alisema hayo wakati wa Uzinduzi wa upandaji miti katika Halmashauri ya Moshi Vijijini, kiwilaya wamepanda miti katika Kijiji cha Lole Marera, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mcharo alisema miti hiyo inatarajiwa kupandwa katika maeneo ya msitu, mingine ikipandwa katika mabonde, vilima na makazi ya watu na kwamba upandaji huo ni kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama za kutunza mazingira.
Alisema katika kuhakikisha uoto wa asili wa mlima huo unarudi kwenye hali yake ya awali, shirika hilo limeunda mtandao wa vijiji 39 vinavyozunguka mlima huo na kutunga sheria zitakazozuia uharibifu wa mazingira.
Akizungumza na waliojitokeza kupanda miti, Meneja mradi wa shirika hilo, Charles Njau alisema lipo kwenye mchakato wa kuomba kibali kwa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Aliwataka wananchi kutambua kuwa msitu huo ni mali ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro hivyo ni vyema wakaheshimu uamuzi kuepuka shughuli za kibinadamu ndani yake.
Diwani wa Kata ya Mwika Kaskazini, Meja Jesse Makundi alisema, lengo la vijiji hivyo ni kupanda miti katika msitu huo ili kunusuru theluji ya mlima huo ambayo iko hatarini kutoweka.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment