Pages

Pages

Pages

Saturday 14 March 2015

MABOMU YARINDIMA JIJINI MWANZA

Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), wakilinda Mtaa wa Makoroboi, jijini Mwanza jana,  baada ya kudhibiti vurugu. Picha na Ngollo John 
Na Ngollo John, Mwananchi
Mwanza. Hali ya amani katikati ya Jiji la Mwanza jana ilichafuka kwa takriban saa mbili kutokana polisi kupambana na wananchi, waliokuwa wakipinga hatua ya madhehebu ya Kihindi ya Swaminarayan kufunga Mtaa wa Makoroboi.
Hatua ya wananchi ilikuja baada ya uongozi wa Hekalu la Swaminarayan kujenga nguzo makutano ya Mtaa wa Lumumba na Makoroboi, ili kuzuia watu kukatisha eneo hilo kwenda Makoroboi.
Awali, eneo hilo lilikuwa lilikuwa likitumiwa na wamachinga, lakini viongozi wa hekalu hilo walimuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kuwaondoa kwa sababu walikuwa wakiwabughudhi wakati wa ibada zao.
Wamachinga 169 waliondolewa na kupewa eneo la Tanganyika ambako wanaendesha biashara zao, sehemu hiyo ilibaki wazi huku wananchi wanaotaka kwenda Makoroboi ambako kuna shughuli nyingi za jamii wakiendelea kukatisha hapo.
Jana saa 3:00 asubuhi, hali ilibadilika ghafla baada ya wananchi kuvamia nguzo za zege zilizojengwa usiku na kuanza kuzing’oa, hali iliyosababisha kuitwa polisi ambao bila kuuliza kilichokuwa kikiendelea walianza kutupa mabomu ya machozi.
Vurugu hizo zilidumu hadi saa 5:30 asubuhi na kusababisha shughuli za uzalishaji katikati ya mji kusitishwa, huku maeneo ya Msikiti wa Ijumaa, Kituo cha Daladala, Mtaa wa Lumumba na Barabara ya Nyerere yakitawaliwa na moshi wa mabomu ya machozi.
Mfanyabiasha wa eneo hilo, Raphael Kinje alisema wamechoshwa na mabomu ya mara kwa mara ambayo yanasababishwa na watu wachache wenye fedha.
Kinje alisema eneo hilo ni njia ya umma ambayo inatumiwa  na wananchi wengi, hivyo kitendo cha kuweka geti kingezuia matumizi ya njia hiyo ya muda mrefu.
Mfanyabiashara wa duka la Gupta Autos Ltd, Jiddavy Hazaa alisema Serikali inatakiwa kuchukua hatua za kisheria ili kuzuia vurugu hizo zinazotokea mara kwa mara, kwani zinaathiri akili na afya za wakazi wake.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema wanawashikilia vijana 12 waliokuwa wanafanya fujo.
“Tulichofanya tumedhibiti wafanya fujo na sasa tunachunguza iwapo ujenzi huo ulikuwa na kibali,” alisema Mlowola.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment