Pages

Pages

Pages

Thursday 1 January 2015

MTUHUMIWA WA DAWA ZA KULEVYA WA SIERRA LEONE AUAWA NA ASKARI MAGEREZA KWEUPEEE


Na Thobias Mwanakatwe, Dar es Salaam
Mtuhumiwa wa kesi ya dawa za kulevya, raia wa Sierra Leone (33), Abdul Koroma, amepigwa risasi na kufa baada ya kujaribu kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Magereza, jijini Dar es Salaam.

Mtuhumiwa huyo alipigwa risasi jana asubuhi, wakati akitaka kukimbia kwa kuruka uzio wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kuzua taharuki kubwa mahakamani hapo.

Askari Magereza mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa kuwa si msemaji wa jeshi hilo, aliiambia NIPASHE kuwa Koroma alifikishwa katika mahakama hiyo akitokea katika Gereza la Keko.

Koroma alikuwa akikabiliwa na shtaka la kuingiza nchini dawa za kulevya aina ya cocaine gram 1,229 zenye thamani ya Sh. milioni 61.4.

Alikamatwa Desemba 2, mwaka 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na dawa hizo.

Kesi hiyo namba PI 21/2013, ilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo,  Augustina Mmbando, na baadaye ilihamishiwa kwa Hakimu Warialwande Lema, ambaye alikuwa akiendelea kuisikiliza.

Kesi hiyo ilikuja jana katika mahakama hiyo kwa ajili ya  kutajwa.

Hadi marehemu anataka kutoroka, upelelezi wa kesi dhidi yake ulikuwa bado haujakamilika.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa muda mfupi baada ya kufikishwa katika mahakama hiyo, mtuhumiwa huyo aliomba kwenda chooni kujisaidia na kusindikizwa na askari.

Askari aliyekuwapo eneo la tukio, alisema kuwa mtuhumiwa baada ya kumaliza kujisaidia, alivua suruali yake aina ya jeans na kubaki na kaptura huku suruali hiyo akiishika mkononi.

Muda mfupi baadaye, Koroma (mtuhumiwa), alijirusha kutoka katika choo hicho chenye vioo ambacho ni maalum kwa ajili ya mahabusu na kujeruhiwa na vioo ambavyo vilimkatakata katika maeneo kadhaa ya mwili wake.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kuruka kutoka katika choo hicho licha ya kujeruhiwa, alianza kutimua mbio na ndipo askari walipoanza kumfukuza wakiwa na silaha za moto.

Askari hao wakati wakiwa katika harakati za kumfukuza, walianza kupiga kelele kuwaomba walinzi wa mahakama hiyo kufunga geti la kuingia na kutoka ili mtuhumiwa huyo asitoke nje ya uzio wa mahakama.

Mtuhumiwa huyo baada ya kuona geti limefungwa, alibadili uelekeo na kwenda kwenye ukuta wa mahakama ambao ulikuwa na nondo na kujaribu kuruka.

Askari waliokuwa wakimfukuza waliwaeleza wenzao kwamba wasimpige risasi kwanza kuepuka kuwajeruhi au kuwadhuru watu wengine wasiokuwa na hatia na kwamba wasubiri hadi afike eneo zuri.

Kutokana na mtuhumiwa huyo kukaidi amri ya kutakiwa kusimama, askari mmoja alipiga risasi mbili hewani, lakini marehemu hakujali na kuendelea kuparamia ukuta wenye nondo.

Hata hivyo, wakati anajaribu kuruka, fulana yake ilinasa kwenye nondo na ndipo mlinzi mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Mwakasisi, alifanikiwa kumshika mguu mtuhumiwa huyo ndipo Askari Magereza alipofyatua risasi zilizompata mtuhumiwa.

Risasi hiyo zilimpata mtuhumiwa huyo kwapani na kutokea kichwani na hivyo kunasa juu ya nondo za uzio wa mahakama hiyo.

Baadaye, yalifika magari matatu ya Jeshi la Polisi na askari wawili walipanda kwenye uzio huo na kumnasua mtuhumiwa huyo huku akivuja damu nyingi na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alithibitisha kupigwa risasi kwa mtuhumiwa huyo ambaye alifariki dunia kabla ya kufikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kamanda Kova alisema Jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini sababu iliyosababisha mtuhumiwa huyo kukimbia akiwa chini ya ulinzi.

Aliwatahadharisha watuhumiwa kuondokana na majaribio kama hayo kwani yanaweza kuwaathiri raia wasio na hatia wakati wa kuwakamata.

Naye Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa ya Muhumbili, Doris Ishenda, alithibitisha kupokea mwili wa marehemu saa 2:47 na kwamba umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment