Pages

Pages

Pages

Thursday 1 January 2015

ACT YADAI KUWATIMU PROFESA KITILA, MWIGAMBA

Katibu Mkuu wa chama cha ACT, Samson Mwigamba
Na Muhibu Said, Dar es Salaam
Chama cha ACT-Tanzania kimedai kutengua uongozi na uanachama wa Katibu Mkuu, Samson Mwigamba na Mshauri wa chama hicho, Prof. Kitila Mkumbo, kwa madai ya kuanzisha chama ndani ya chama na kula njama za kutaka kukikabidhi kwa mafisadi.


Mwenyekiti wa chama hicho, Kadawi Limbu, alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa na kamati kuu ya chama hicho katika kikao chake, kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Alisema kutokana na uamuzi huo, wanamtaka Mwigamba kwenda Dar es Salaam kukabidhi mara moja mali za chama.

“Tumeamua kwa dhati ili kutoa fundisho kwa wengine…waanzishe chama chao cha siasa. Tuliwakaribisha tukiwa tayari tumeshakianzisha chama. Hawana chembe ya uhalali wa uanzilishi wa chama chetu kama ambavyo wamekuwa wakitamba huko nyuma,” alisema Limbu.

Alidai pamoja na makosa makubwa yaliyofanywa na Prof. Mkumbo na Mwigamba siku za nyuma, kwa kushirikiana na baadhi ya watu ndani ya chama, wametiliana saini mkataba wa kimataifa na kampuni moja binafsi ya Senegal wa kukisaidia chama mamilioni ya shilingi, huku yeye kama mwenyekiti na viongozi wengine wakuu wa chama bila kuwa na taarifa zozote.

Alisema kitendo hicho hakina tofauti na kile kilichowahi kufanywa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, cha kutiliana saini mkataba kinyemela na wawekezaji kwa ajili ya kuchimba madini katika mgodi wa Buzwagi.

“Fedha zilizotaka kutumika kuendesha chama tumejiridhisha kuwa zimechotwa Escrow…Kama tunawalaani kina Karamagi kusaini mikataba kwa siri iweje katika chama?” alihoji Limbu, ingawa hakuonyesha mkataba huo wala kuthibitisha fedha anazodai kuwa zilichotwa kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.

Pia alidai wamebaini njama zilizokuwa zikifanywa na Prof; Mkumbo na Mwigamba za kutaka kuanzisha chama ndani ya chama, baada ya kuchukua katiba, ambayo hawajakubaliana na ‘kuichomeka’ kwa msajili wa vyama vya siasa.

Alidai ofisi ya msajili wa vyama vya siasa imeanza kutumika vibaya kukichafua chama hicho, hivyo, akamuomba msajili kutoridhia kitendo cha Prof. Mkumbo na Mwigamba ‘kuichomekea’ nyaraka ofisi yake.

MAJIBU YA PROF. KITILA
Alipoulizwa na NIPASHE jana, Prof. Mkumbo alisema majibu kuhusu madai hayo yatatolewa na mwanasheria wao.

Hata hivyo, alisema hakuna kamati kuu ya ACT-Tanzania iliyokutana kama inavyodaiwa na Limbu na pia hakuna mkataba wowote waliotia saini na ndiyo maana mwenyekiti huyo hakuweza kuuonyesha.

Alisema kamati kuu ya ACT-Tanzania itakutana Jumatatu wiki ijayo kwa ajili ya kupanga uchaguzi ndani ya chama.

Kwa mujibu wa Prof. Mkumbo, Limbu ni mwenyekiti wa muda katika chama, hivyo anaogopa kung’olewa na ndiyo maana ameanza kujihami.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment