Pages

Pages

Pages

Thursday 11 December 2014

TAIFA STARS ILIPOLALA TENA KWA BURUNDI


Na Imani Makongoro, Mwananchi
Dar es Salaam. Tanzania imeendeleza uteja wake kwa Burundi baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa, Taifa Stars ikiwakilishwa na wachezaji wengi wa majaribio.
Katika mchezo huo wa kusherekea miaka 53 ya uhuru wa Tanganyika, Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Yusuph Rashid, lakini Burundi walisawazisha kupitia Nininagazwe Fabrice kabla ya Niyonkuru Nassor kupachika bao la ushindi kwa wageni hao.
Hicho ni kipigo cha tatu mfululizo kwa Stars mbele ya Burundi. Mara ya kwanza ilifungwa mabao 3-0 katika mechi ya kusherekea miaka 50 ya Muungano, wakanyukwa tena 2-0 jijini Bunjumbura mwezi Septemba.
Taifa Stars ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika 11, lililofungwa na Rashid akimalizia krosi ya Michael Gadiel.
Burundi walijibu mapigo dakika 21, baada ya shuti la Nininagazwe Fabrice kupanguliwa na ustadi mkubwa na kipa Stars, Aishi Manula na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Nininagazwe alisawazishia Burundi dakika 24, baada ya kuchukua mpira umbali wa mita 40 na kuwatoka mabeki wa Stars kabla ya kugongeana na mwenzake ndani ya eneo la penalti 18 na kuubetua mpira juu ya Manula.
Burundi waliwatoa Nshimiriman Abbas na Mavugo Laudit na kuwaingiza Nahiman Nassiri na Mubango Tresor, wakati Stars iliwatoa Moshi Hussein na Friday na kuwaingiza Shiza Emmanuel na Mohamed Abubakari.
Burundi ilihitimisha ushindi katika dakika 78 wakati Mubango alipopiga krosi ya chini nyuma ya ukuta wa Stars na kumkuta Niyonkuru aliyemalizia kirahisi.
Taifa Stars: Manula Aishi, Adam Miraji, Michael Gadiel, Mgeveke Joram, Andrew Vicent, Mbonde Salum, Yusuph Rashid,  Hassan Banda, Green Atupele, Kelvin Friday, Moshi Hussen.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment