Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 11 December 2014

NYERERE ADAI KUTISHIWA KUUAWA

Vincent Kiboko Nyerere, Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema)

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Musoma Mjini, mkoani Mara, Jacob Nkomola, anadaiwa kuhamasisha wafuasi wa chama hicho kufanya mauaji dhidi ya Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere. 


Nkomola anadaiwa kutoa maelekezo hayo kwenye mkutano wa hadhara eneo la Nyasho Stendi mjini humo katika kampeni za kuwania uongozi wa serikali za vitongoji, vijiji na mitaa zinazoendelea kote nchini. Akizungumzia tukio hilo, Nyerere ambaye ni Mbunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita saa tano asubuhi.

“Kwanza kabisa alivamia eneo letu ambalo ratiba ilionyesha kuwa tulitakiwa kufanya mkutano kuanzia saa tano asubuhi, lakini yeye (Nkomola) akafunga vyombo kuanzia saa 12 alfajiri na kuanza kutangaza hadharani kwamba ili wawe salama, ni lazima Mbunge wa Musoma Mjini auawe, jambo ambalo lilipelekea kuzuka kwa vurugu,” alisema Nyerere na kuendelea:

“Kutokana na kauli hiyo na mazingira yenyewe yalivyokuwa, polisi waliamuru kusiwepo na mkutano kwenye eneo hilo ili kuepusha hatari ambayo ingeweza kutokea, kutokana na kauli hiyo ya katibu wa CCM.”

Nyerere alisema kuwa tayari ameliripoti tukio katika ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Musoma Mjini (OCD) na kuandikisha maelezo kuhusu kauli hiyo ambayo alidai inamnyima usingizi akihofia kuuawa wakati wowote.

Alipoulizwa OCD Juma Majata, kuhusiana na tukio hilo, alithibitisha na kusema kwamba  wameanza kuzifuatilia tuhuma hizo ili kujua kama zina ukweli ili sheria ichukue mkondo wake.

“Tumezijua baada ya mheshimiwa Mbunge kuja hapa ofisi kutoa taarifa, hivyo sasa tunazifuatilia ikiwa ni pamoja na kumuita mtuhumiwa aje ajieleze ili kujua undani wake,” alisema Kamanda Majata.

Hata hivyo, NIPASHE ilipomuuliza Nkomola kuhusu tuhuma hizo, alikana na kusema kuwa hajawahi kutoa kauli hiyo na kama kuna ushahidi wa tepu, uwekwe hadharani ili wananchi wajue kama kweli ametamka maneno hayo.

“Kilichotokea ni kwamba mkurugenzi wa halmashauri alitugonganisha katika ratiba ya mikutano ya kampeni na kujikuta tuko eneo moja, hali ambayo ilisababisha vurugu kidogo, lakini polisi walikuja na kuzimaliza,” alisema Nkomola.

Katibu huyo alisema kuwa kinachofanywa na Chadema sasa ni kutaka kura za huruma kutoka kwa wananchi kwa mtindo wa  kukizushia Chama Cha Mapinduzi tuhuma ambazo hazina ukweli.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment