Pages

Pages

Pages

Thursday 11 December 2014

MFANYABIASHARA MAARUFU MOSHI, ARUSHA AJIUA KWA RISASI

Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro, Godfrey Kamwela

Mfanyabiashara maarufu katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, Agustin Malya (40), amejiua kwa kujipiga risasi mjini Moshi.


Mfanyabiashara huyo wa madini na samani za ndani mkoani Kilimanjaro, amejiua kwa kujipiga risasi kifuani na kufariki dunia papo hapo.

Mfanya biashara huyo mkazi wa kata ya Karanga, Manispaa ya Moshi, alijipiga Risasi juzi Jumanne, majira ya saa 11:00 alifajiri, nyumbani kwake baada kuugua maradhi ya tumbo kwa muda mrefu.

Akizungunza na NIPASHE, mke wa marehemu, Elizabeth Mallya (32), alisema alibaini kufariki kwa mume wake baada ya kusikia mlio wa risasi sebuleni muda mfupi baada ya kuamka na kuanza kujiandaa kwenda kanisani.

“Alfajiri, mume wangu aliamka na kwenda bafuni kwa ajili ya kuoga ili aweze kwenda kanisani. Mara nikasikia mlio mzito wa risasi, nilipofika nilikuta amejipiga risasi ya kifuani na kupoteza maisha papo hapo,” alisema Elizabeth na kuongeza:

“Mume  wangu alikuwa akisumbuliwa na tumbo kwa muda mrefu licha ya kutibiwa nchini India pamoja na hospitali mbalimbali hapa nchini bila mafanikio. Alitakiwa India Desemba 12 (kesho) kwa ajili ya upasuaji wa kile kilichodaiwa kuwa ni kansa.”

Elizabeth alisema mumewe alitumia silaha aliyokuwa akimiliki kihalali  aina ya bastola Browing iliyosajiwa kwa namba za usajili TZ CAR 96682 yenye risasi nane.
Marehemu ameacha mke na watoto wanne na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya K.C.M.C, mjini Moshi.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro, Godfrey Kamwela, alipotafutwa na NIPASHE, hakupokea simu licha ya kupigiwa zaidi ya mara 10 na kutumiwa ujumbe mfupi  wa maneno (SMS) bila majibu yoyote.

NIPASHE ilipokwenda kituo kikuu cha polisi mkoani hapa, polisi walisema hawajapata taarifa.

Baadhi ya wananchi mkoani Kilimanjaro, wameiomba serikali pamoja na mashirika binafsi kuingilia kati  matukio ya watu kujipiga risasi hasa matajiri mkoani Kilimanjaro.

 “Ifike mahali serikali pamoja na taasisi mbalimbali zikiwamo za dini kuliangalia suala hili la matajiri kujitoa uhai wao pasipokuwa na sababu za msingi, yawezekana  wanafanya biashara bila hofu ya Mungu,” alisema Denis Ngowi mkazi wa Manispaa Moshi.

Akizungumzia tukio hilo, Mchungaji wa Kipentekoste wa Kanisa la Mailisita, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema yawezekana watu hao  wamekuwa wakifanya biashara kwa njia za ushirikina au kutokuwa na hofu ya Mungu.

Tukio hili ni la pili baada ya Mei 27, mwaka huu aliyekuwa mfanyabiashara  maarufu Werasimba Lema (74) mkazi wa  Msasani Mailisita, kata ya Kindi,  wilaya ya Moshi,  kujipiga risasi baada ya kugungulika kuwa na saratani ya koo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment