Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 11 December 2014

ESCROW YAITOKEA PUANI CHADEMA

VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) wilayani Kahama, mkoani Shinyanga wametekwa na kushambuliwa na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi, huku wakihoji ni kwa nini wameshindwa kuwawajibisha viongozi waliochota fedha za umma kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Tukio hilo lilitokea juzi usiku mjini Kahama wakati viongozi hao wakitokea kwenye mkutano. Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, baada ya msafara wa viongozi hao kutekwa ilitolewa amri ya kuwataka kusimama na kuzima taa za magari na muziki.

Kisha majambazi hayo yaliwaambia kwamba hawawezi kuwadhuru kwani CHADEMA ni chama cha makamanda, lakini itabidi watoe fedha na simu kwa sababu ya kushindwa kuwawajibisha viongozi walionufaika na fedha za umma kutoka akaunti ya Escrow.

“Tupo kazini tunawaomba msitulaumu, muwalaumu viongozi waliokula pesa za Escrow, bila hivyo tusingefanya kazi hii... tunawalaumu mmeshindwa kuwawajibisha wezi wa fedha za umma,” alisema Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Kahama, Juma Protasi, wakati akieleza yaliyojiri siku ya tukio kwa waandishi wa habari.

Protasi, aliwaambia waandishi wa habari juzi ofisini kwake kuwa majambazi hao baada ya kuwateka, walianza kuwapiga huku wakihoji ni kwa nini wameshindwa kuwawajibisha watuhumiwa wa Escrow.

Alisema wakiwa wanatoka katika mkutano wa kampeni walitekwa na kundi la majambazi kwenye mbuga iliyopo katikati ya vijiji vya Kalagwa na Nyambula, vilivyopo Kata za Ntobo na Ngogwa.

Alisema walikuwa na magari mawili yaliyobeba viongozi wa Chadema wa wilaya. Protasi alisema wakati wanafika eneo hilo la daraja walikuta magari mengine matatu yakiwa yamesimama pembeni ambayo nayo yalikuwa yametekwa.

Alitaja magari hayo kuwa ni basi moja lililokuwa linatoka mkoani Geita, lori aina ya Fuso na gari moja dogo la Kampuni ya Bia Tanzania (TBL). Alisema waliokuwa kwenye magari hayo tayari walikuwa wameporwa.

Mwenyekiti huyo aliwataja viongozi wengine aliokuwa kwenye msafara huo ni Mratibu wa Kanda ya Ziwa Mashariki, Renatus Mzemo na Mwenyekiti wa Kamati ya Rasilimali Kanda ya Ziwa Magharibi, Emmanuel Mbise. Alisema viongozi hao walikuwa wamepanda gari aina ya Toyota Prado namba. T 707 BBP.

“Tuliporwa fedha zaidi ya sh.900,000 na simu 11 ambazo thamani yake haikufahamika mara moja.” Alisema magari yote yaliyotekwa yalivunjwa vioo.

“Kulikuwa na magari mengi tuliyoyakuta yametekwa na abiria walinyangíanywa simu na fedha zao, pia kulikuwa na Mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Lunguya ambaye naye alitekwa akiwa na pikipiki yake aina ya Sanlg,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw.Justus Kamugisha alipoulizwa kwa simu yake ya kiganjani juu ya tukio hilo alisema kuna watu wasiofahamika usiku wa siku hiyo waliyarushia magogo magari hayo katika barabara itokayo wilayani Kahama kwenda mkoani Geita na kusababisha uharibifu kwenye baadhi ya magari hayo.

Mwandishi wa habari wa gezeti la Tanzania Daima wilayani hapa aliyekuwa katika msafara huo, Ally Lityawi, alisema majambazi hayo yakiwa na silaha waliwateka Jumanne saa 3.30 usiku wakati wakitoka katika kapeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika kata ya Bulyanhulu jimbo la Msalala, wilayani Kahama.

Wakati huo huo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dkt.Martin Shao, amemshauri Rais Jakaya Kikwete, kutumia ujasiri kuwaondoa madarakani viongozi wanaotuhumiwa kuchotewa fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.

Askofu Shao, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Karatu, kwenye uzinduzi wa jengo la Kanisa Usharika wa Karatu mkoani Arusha.

Alimshauri Rais Kikwete, kutumia haki bila kuwaangalia nyuso zao ili kuwachukulia hatua viongozi wabovu na wabinafsi bila kuangalia itikadi zao. Askofu Shao alisema ni aibu kwa Taifa watu kujichukulia mabilioni ya fedha za wananchi, huku Rais wa nchi akikaa kimya bila kuwachukulia hatua za kisheria.

“Viongozi wanatakiwa kuwa waadilifu katika kazi zao za kila siku, hivyo viongozi wenye uroho wa pesa si viongozi wanaostahili kukaa madarakani, bali wanaliingiza taifa kwenye matatizo,” alisema Askofu Shao.

Aliendelea kusema kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi, lakini rasilimali hizo haziwanufaishi Watanzania bali zinawanufaisha watu wachache wenye uroho wa madaraka kwa masilahi binafsi.

Aliwataka wananchi kuwachagua viongozi waadilifu wasio na roho ya ubinafsi wenye uwezo wa kuongoza bila kuangalia vyama wanavyotoka katika uchaguzi wa Serikali za mitaa

Askofu Shao alisema kuna viongozi ambao wanatumia nyumba za ibada kwa kufanya kampeni, hivyo aliwataka kutotumia nyumba za ibada kwa kuomba kura, bali wapende nyumba za ibada.

Akisoma risala, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Kanisa hilo, Jublet Mnyenye, alisema ujenzi wa kanisa hilo umegharimu sh. bilioni 1.5 zilizotokana na michango ya washarika wa Karatu.

CREDIT: MAJIRA

No comments:

Post a Comment