Pages

Pages

Pages

Thursday 6 November 2014

RAIA 12 WA IRAN KORTINI KWA DAWA ZA KULEVYA KILOGRAMU 41



Na Tausi Ally, Mwananchi
Dar es Salaam. Raia 12 wa Iran wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakituhumiwa kuingiza nchini dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye thamani ya zaidi ya Sh2 bilioni.
Wakili wa Serikali, Hellen Mushi akishirikiana na Janeth Kitali aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Mansoor Raisi (24), Kheri Mohamed (32), Rasul Baksh (50), Gulam Rezar (42), Nawab Bari (40) na Nazir Pack (39).
Wengine Mohamed Rafiq (25), Rahim Baksh(49), Salim Kosal (43), Yari Muhamad (35), Razar Raisi (32) na Allan Nuru Jawi (35).
Akisoma hati ya mashtaka inayowakabili, Mushi alidai kuwa Oktoba 30, mwaka huu washtakiwa hao walikamatwa wakiingiza nchini kilo 41.7 za dawa hizo.
Mushi alidai washtakiwa hao walikamatwa eneo la Bandari ya Dar es Salaam sehemu ambayo meli kutoka nje ya nchi hutia nanga.
Alidai kuwa washtakiwa hao, walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 16(b) cha sheria ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi haujakamilika na Hakimu Kaluyenda aliamuru washtakiwa kupelekwa rumande hadi Novemba 18 mwaka huu.
Wakati huohuo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imeshindwa kumsomea maelezo ya awali, Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee (35) na wenzake wanane wanaokabiliwa na mashtaka mawili ya kukataa kutii amri halali ya Jeshi la Polisi kufanya mkusanyiko usio halali baada ya upande wa mashtaka kubaini upungufu kwenye maelezo ya kesi.
Wakili wa Serikali, Hellen Mushi akishirikiana na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Jackson Chidunda walisema kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Baada ya Mushi kueleza hayo, Chidunda aliwakumbusha washtakiwa hao mashtaka yanayowakabili kuwa Oktoba 4, mwaka huu katika Mtaa wa Ufipa, bila kuwa na uhalali walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi (SP) Emmanuel Tillf kwa niaba ya Jeshi la Polisi.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment