Pages

Pages

Pages

Thursday 6 November 2014

KUMEKUCHA, SAKATA LA IPTL/ESCROW KUTINGA BUNGENI NOVEMBA 27!


Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Na Boniface Meena, Mwananchi
Dodoma. Ripoti ya ufisadi katika akaunti ya Escrow itawasilishwa bungeni Novemba 27, mwaka huu na kujadiliwa baada ya Kamati ya Uongozi ya Bunge kuridhia kwamba Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) inaweza kushughulikia suala hilo.
Taarifa zinaeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya baadhi ya wenyeviti wa kamati za Bunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Uongozi kutaka suala hilo lijadiliwe katika Bunge linaloendelea ili wanaopaswa kuwajibika kutokana na ufisadi huo wachukuliwe hatua.
Mjumbe mmoja wa kamati ya uongozi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema jana wamekubaliana kwamba hakuna haja ya kuundwa tume kama ilivyokuwa imeombwa awali na Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba bali, PAC ambayo ndiyo kamati husika inayoweza kuchunguza suala hilo na kuliwasilisha baada ya kupata ripoti ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hata hivyo, Naibu Spika, Job Ndugai ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi iliyokaa juzi jioni, hakutaka kuzungumzia suala hilo ambalo awali liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila akielekeza kuwa ratiba ya shughuli za Bunge ina mwongozo mzima wa nini kitafanyika. Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Novemba 27, PAC itatoa taarifa maalumu bungeni ambayo mwenyekiti wake, Zitto Kabwe alisema inahusu uchunguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba Bunge litajadili taarifa hiyo baada ya kamati kuiwasilisha.
“Ripoti inaweza kuiangusha Serikali kwa Waziri Mkuu kulazimishwa kujiuzulu. Iwapo ripoti ya CAG itaonyesha kuwa suala hilo siyo safi, basi Waziri Mkuu atatakiwa kujiuzulu kwa kuwa aliwahi kusema suala la Escrow liko sawa,” alisema Zitto.
Suala hilo lilizua mjadala bungeni juzi ambako Ndugai akitoa mwongozo ulioombwa na Kafulila kwamba hoja hiyo kuhusu lini Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atawasilisha ripoti hiyo baada ya uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na CAG kukamilika kwa kuwa ni ya haraka alisema; “Suala la Kafulila tutalishughulikia kwenye Kamati ya Uongozi kwa kuwa kiti hiki hakina mamlaka.”
Baada ya Kafulila kuomba mwongozo huo aliungwa mkono na wabunge wa upinzani na baadaye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama na kusema, “Ni kweli Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa Takukuru na CAG kufanya uchunguzi huo na kukabidhi ripoti kwake ili atoe taarifa bungeni, lakini kazi hiyo haijakamilika.”
Lukuvi alisema ukaguzi wa CAG bado unaendelea kwa kuwa unahusu mambo mengi na kwamba taarifa zinaeleza kuwa wako mbioni kukamilisha hivyo wakikabidhi kwa waziri mkuu itawasilishwa bungeni na kukabidhiwa kwa Spika kwa ajili ya utekelezaji.
Alisema taarifa hizo mbili hazijakabidhiwa kwake na kwamba Takukuru ikimaliza uchunguzi wake inaweza kuchukua hatua yenyewe lakini taarifa inayosubiriwa na Bunge ni ya CAG.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment