Pages

Pages

Pages

Sunday 2 November 2014

NAHODHA AFAGILIA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR

Waziri Kiongozi Mstaafu wa awamu ya sita, Shamsi Vuai Nahodha. PICHA|MAKTABA YA MWANANCHI
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar: Wakati Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ikitimiza miaka minne, Waziri Kiongozi Mstaafu wa awamu ya sita, Shamsi Vuai Nahodha amesema ipo haja ya kuendelea kuwa na umoja huo kwa vile sababu zilizofanya kuundwa kwa Serikali shirikishi ya vyama vya CCM na CUF bado zipo.
Nahodha anaeleza hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika nyumbani kwake Chukwani, Zanzibar na kusema kuwa faida za serikali za SUK ni nyingi na zimeleta manufaa kwa wananchi.
Alisema ni vyema watu watathmini manufaa ya mfumo huo wa serikali, waangalie faida zake kwa serikali yenyewe na hata kwa wananchi.
“Zanzibar imepita kwenye misukosuko mingi ya kisiasa tokea mwaka 1957 hadi 2010, matatizo yamekuwa yakiongezeka kila unapofanyika uchaguzi kutokana na ushindani mkubwa wa kisiasa uliopo.”
Alisema matokeo ya chaguzi kuu tangu mwaka 1995 yameonyesha hakuna tofauti kubwa ya ushindi kati ya CCM na CUF, pamoja na kuwa katika chaguzi zote 1995, 2000, 2005 na 2010 CCM ilishinda lakini tofauti ya mshindi na mpinzani wake haikuwa kubwa sana.
Alisema ingawa CCM kiliendelea kushinda kwa asilimia 51, 52, na 54, hali hiyo inaonyesha kuwa chama cha upinzani CUF pia kina nafasi kubwa tu ya kushinda kwa sababu hupigiwa kura na takriban nusu ya Wazanzibari.
Nahodha alisema iko haja ya kutambua kuwa ushindani huu unahitaji kuangaliwa kwa umakini mkubwa kwa vile wataalamu wa mambo ya siasa wanasema mahali kwenye ushindani wa nguvu msipokuwa na utaratibu mzuri wa kugawana madaraka, hapatakuwa na utulivu utakaosaidia kuwaletea maendeleo wananchi mnaokusudia kuwaongoza.
Waziri huyo Kiongozi mstaafu Zanzibar alitoa mfano wa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron wa Chama cha Liberal kwamba pamoja na kuwa yeye na chama chake walipata ushindi, alilazimika kukikaribisha chama cha Conservative ili kuunda serikali ya pamoja kwa nia ya kuwaletea maendeleo wananchi wao na kuziba nyufa na makovu yatokanayo na mitafaruku ya uchaguzi.
Alisema kwa asili na historia ya Zanzibar, siasa zake zimekuwa na matatizo hata kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Alisema vyama vya siasa vilivyokuwapo kabla ya Mapinduzi mara kadhaa viliunganisha nguvu ili vipate ushindi kwani mara zote uchaguzi ulitoa ushindi mwembamba kiasi cha chama kimoja kushindwa kuunda serikali peke yake.
Jambo ambalo hatalisahau
Kuhusu jambo ambalo hatalisahau, Nahodha alisema ni mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar katika kipindi cha miaka 10 yeye akiwa Waziri Kiongozi chini ya Rais Dk Amani Karume kabla ya kuibuliwa mpango wa kuanzisha mazungumzo ya kusaka upatanishi uliozaa mwelekeo wa kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Akielezea hisia zake anasema wakati mwingi moyo wake ulikuwa ukisononeka hasa alipoona vyombo vya dola vinatumia nguvu kupambana na ghasia zilizokuwa zikijitokeza ili kuhakikisha vinaweka mazingira ya utulivu. Alisema matokeo ya vurugu na mapambano ya kutafuta amani ndiyo yaliyomsononesha kwa sababu wengi walioathirika kwa njia moja ama nyingine ni wananchi wa kawaida.
“Sitasahau katika maisha yangu ya uongozi misukosuko ya kisiasa iliyojitokeza wakati ule kwa miaka 10 chini ya uongozi wetu, hata hivyo Rais Karume alikuwa akitumia busara sana kukabiliana na kila hatua hatarishi, moyo wangu haukuwa ukipenda yatokee mazonge na hasama,” anasimulia Nahodha.
Aidha, Nahodha anamsifu Rais Jakaya Kikwete kwa kuibua wazo la kuanzishwa kwa mazungummzo ya kusaka upatanishi wa kisiasa kati ya CCM na CUF na vilevile, hatamsahau Rais Karume kwa kuyasimamia mazungumzo hayo na kuyafanikisha kwa njia za kiungwana.
Kuhusu Katiba Inayopendekezwa
Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa kupingwa na baadhi ya makundi vikiwamo baadhi ya vyama vya siasa, Nahodha alisema Katiba kupingwa katika taifa lolote ni jambo la kawaida na hakuna katiba hata moja duniani iliyoandikwa, kurekebishwa au kuandikwa upya ikapata kuungwa mkono na makundi yote kama mapokeo ya vitabu vya Mungu.
Alieleza kuwa kutokana na historia ya jambo hilo, hakatishwi tamaa au kushtushwa kuona watu wakinyoosheana vidole na kusema wanaipinga katiba hiyo na kwamba jambo pekee muhimu ni suala hilo liungwe mkono na wengi ili kuwashinda wachache kwa nguvu ya hoja na uamuzi.
“Dunia itatushangaa sana ikiwa Katiba iliyoandikwa kwa kutumia kodi kubwa ya fedha za wananchi ikikwamishwa na kundi la wachache kwa kutetea masilahi binafsi, panapo majaaliwa naamini Katiba inayopendekezwa itapita na kupatikana kwa asilimia 50 Bara na Zanzibar.”
Nahodha aliyataja mambo matano ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa muda mrefu na Wazanzibari na kusema kuwa sasa yamepatiwa majibu katika Katiba Inayopendekezwa ikiwamo uwezo wa kimamlaka kwa Zanzibar kuweza kujiunga na jumuiya za kikanda na kimataifa.
Rais wake kuwa sehemu ya itifaki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, suala la mafuta na gesi asilia kuondolewa katika mambo ya Muungano na kukopa katika taasisi za fedha za nje.
Nahodha anaitaja ibara ya 76(2)(3) ya Katiba Inayopendekezwa inasema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itakuwa na mamlaka na haki juu ya mamabo yanayohusu Zanzibar, uwezo wa kuanzisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa na Serikali ya Muungano itapaswa kufanikisha.
Kadhalika alisema kuanzishwa kwa Tume ya Usimamizi na Kuratibu Mapato yatokanayo na vyanzo vya Muungano na kuweka taratibu za mgawo wake sasa ukitajwa kikatiba na kisheria ikiwamo uchangiaji wa uendeshaji wa shughuli za Muungano ni mambo yanayofungua ukurasa mpya katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amelitaja jambo lingine ambalo limekuwa kilio kwa Zanzibar ni suala la mafuta na gesi asilia ambalo lilileta mjadala mkubwa na serikali ya awamu ya sita pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakitaka suala hilo liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano, sasa dai hilo limesikilizwa na kutekelezwa kisheria na kikatiba.
“Ikiwa Katiba Inayopendekezwa haitapita, Zanzibar ndiyo itakayopoteza fursa zake na si Tanzania Bara, kupita kwa katiba hii ni kufanikiwa kwa Zanzibar katika dhana ya kusukuma mbele maendeleo yake hasa ya kiuchumi na kuikwamisha ni kutupa fursa hizo,” alieleza Nahodha.
Ukawa
Kuhusu Muungano wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF chini ya mwamvuli wa Ukawa, Nahodha alisema mtu mwenye nguvu za kutosha na kujiamini huwa hahitaji msaada au ushirika na kueleza ana wasiwasi mkubwa wa kudumu kwa umoja huo kutokana na tofauti za kisera, kifalsafa na kimsimamo.
Alisema vyama vyote vilivyounda Ukawa vinafahamika sera zao, itikadi zao za kisiasa, mitazamo na misimamo ya viongozi wao, hivyo wana kazi ngumu kufikia malengo yao, ugumu wake ni sawa na kumpitisha ngamia kwenye tundu la sindano.
“Sina hakika ya kudumu kwao kama hakutakumbwa na dhoruba,” alisema Nahodha.
Alisema anakumbuka kuanzishwa kwa aina ya miungano kama hiyo huko nyuma ukiwamo ule wa kamati ya kwanza kabla ya vyama vingi iliyoitwa NCCR chini ya Mwenyekiti Chifu Abdallah Fundikira na baadaye ukaja Umoja wa Demokrasia Tanzania (UDETA ) chini ya Mabere Marando, lakini miungano yote hiyo haikufika popote na kujikuta wakivurugana.
“Hata Chadema na CUF waliingia katika mvutano mkubwa tukiwa bungeni pale Dodoma, Chadema wakakihusisha CUF kuwa ni chama chenye itikadi ya uliberali (Liberal International) ambao wanaunga mkono masuala ya ushoga na kujikuta wakisuguana na kuhasimiana.
Pia alieleza kuwa wakati CUF ikiunda serikali kivuli tangu mwaka 1995 wakiwa bungeni, ilikataa kuvishirikisha vyama vingine na kuviita ni vichanga jambo ambalo pia lilikuja kujitokeza kwa Chadema kuviacha NCCR-Mageuzi na CUF katika Bunge la 2010 huku Chadema wakikilaumu CUF kuwa kina ushirika na CCM huko Zanzibar na mara kadhaa walikiita ‘CCM B.’
“Sitaki kuwavunja moyo mapema, tunahitaji muda jambo hilo kuliona linafikia wapi, lazima tujipe maswali ya akiba, je, falsafa, itikadi na sera zao zinafanana? Je, wako tayari kuvunja vyama vyao na kuunda kimoja ili kushindana na CCM? Nafikiri huwezi kuwa na nia ya kushuka ngazi na mwenzako mkiwa mmeshikana mikono wakati mmoja anataka kupanda na mwingine anateremka,” alisema Nahodha.
Kuhusu mawaziri kutoka CUF waliounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kuamua kuungana na Ukawa, Nahodha alisema jambo hilo linaweza kuiteteresha Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar iwapo atatokea kiongozi mmoja akaamua kutekeleza majukumu yake kinyume na katiba na sheria.
Nahodha alisema kwa kuwa mawaziri wa SMZ hawakuwa na msimamo wa serikali kuhusiana na uundwaji wa katiba, kususia kwao Bunge haikuwa tatizo kwani waliondoka kama wabunge wa Bunge la Katiba walioamua kujitoa na hivyo haikuwa taathira kulingana na idadi ya wabunge waliobaki bungeni.
Alisema kwa bahati mbaya sana wakati uamuzi huo wa Ukawa wa kujitoa bungeni ulipochukuliwa waliangalia kipengele cha muundo wa Muungano tu, wakati rasimu hiyo ilikuwa na sura 16 na vifungu 157 ambavyo vyote kimsingi vilikuwa na umuhimu wa wao kushiriki, kuchangia, kushauri, kuongeza jambo au kupunguza na halikuwa jambo la kuwafanya wakimbie.
Wagombea urais
Kuhusu wanaojitokeza au wanaotangaza kutaka kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nahodha alisema makada wa CCM waliojitokeza na kutangaza nia hawajafanya kosa kwa vile ni nafasi pekee kwa wananchi kuanza kuwachambua, kuwapima na kuwatathmini mapema.
“Ni wazi kuwa wananchi watakuwa wamepata fursa ya kuwaona, kuwatambua na hata kugundua upungufu au kasoro au hitilafu za kimaadili ama kinidhamu walizonazo na kujua kama wana uwezo au sifa za kushika nafasi hiyo ya juu.
Waziri Kiongozi huyo mstaafu alisema jambo la msingi ni chama na wanachama kuwa makini na kumteua mgombea anayeuzika kwenye soko la wapiga kura ambaye atakuwa na uwezo, ushawishi, anayeaminika kiutendaji, mwenye historia ya uchapakazi na anayezijua siasa za Muungano na mzalendo wa vitendo na muonekano wake.
“Hata marehemu Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema ni vyema mgombea anayetaka nafasi ya uongozi wa juu akajitangaza mapema ili wenzake wampime, wamchambue ili kuona kama ana viwango vya uadilifu, nidhamu na heshima inayostahili mbele ya jamii. Kwa hiyo waliofanya hivyo sifikirii kama wana kosa na wanaweza kubanwa na hatia,” alisema Nahodha.
Alisema hata makada walioadhibiwa na kuwekwa katika vifungo vya maadili, hawakuadhibiwa kwa kutangaza kwao nia ila walifungiwa kwa tuhuma za kuanza kampeni mapema na kushawishi kwa kutumia bakhshishi jambo ambalo alisema ndani ya CCM hilo halikubali na halitaachiwa lichukue nafasi.
Hata hivyo, alisema CCM ina nafasi ya kushinda Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015 Zanzibar na Tanzania Bara kutokana na chama hicho mizizi yake kufika mbali katika maeneo ya Jamhuri ya Muungano ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa ilani yake katika maeneo ya ujenzi wa miundombimu, nishati, elimu, afya na kilimo.
Kuhusu kugombea urais wa Zanzibar
Nahodha alisema CCM imeweka utamaduni wake maalumu ambao ni wa kistaarabu, kwani anapotokea kiongozi mmoja akipata nafasi ya kuwa Rais anatakiwa amalize vipindi vyake viwili hivyo hana fikra wala mpango wa kuchukua fomu ya kuwania urais Zanzibar kwa wakati huu.
Alisema pamoja na utaratibu huo kukosa mashiko ya kikatiba, lakini yeye anausifu kwa kuwa unasaidia kujenga umoja, kuaminiana na kuheshimiana.
“Sitakuwa mjinga wa kukiuka utaratibu uliowekwa na chama changu, sina fikira wala mpango wa kuwania urais wa Zanzibar, tunachokihitaji kwa sasa ni kumsadia Rais Dk Ali Mohamed Shein amalize ngwe yake kwa salama na kuiletea Zanzibar maendeleo yanayotarajiwa,” alisema Nahodha.
Alisema kuwa awamu zote za uongozi toka 1964 kila moja imefanya wajibu wake na kuhakikisha yale aliyoyaamini hayati Mzee Abeid Karume katika kupiga vita ujinga, maradhi na umasikini, yanasimamiwa kwa umakini licha ya chati ya kiuchumi kupanda na kushuka kwa vipindi tofauti lakini la muhimu nu kuwa malengo ya Mapinduzi yanasimamia kwa nidhamu kama yalivyoasisiwa.
Nahodha alisema pamoja na elimu kuwa bila ya malipo na kila mtoto akifaidika na matunda hayo, ipo haja na ulazima wa kuangaliwa ubora wa elimu inayotolewa.
Kuhusu vichocheo vya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar Nahodha ameishauri serikali ihakikishe inakuwapo bandari huru huku maeneo huru ya kiuchumi yakipewa kipaumbele. Kadhalika amezungumzia kuendeleza shughuli za utalii, kuboresha usafiri wa anga ili kuifanya Zanzibar iwe ni eneo linalofikika kwa urahisi.
Maadili ya viongozi
Kuhusu kushuka kwa viwango vya maadili ya viongozi, Nahodha alisema serikali lazima iweke rasilimali fedha za kutosha na wataalamu wa mambo ya uchunguzi ili Tume ya Maadili iweze kufanya kazi zake za kuchunguza watendaji na viongozi wanaovunja na kukiuka miiiko ya uongozi na kuhakikisha lengo la kuimarisha misingi ya utawala bora inafikiwa.
Alisema kulingana na ukubwa wa nchi, Tume hiyo inashindwa kuwafuatilia kwa undani na kutaka Tume hiyo ipewe uzito kulingana na umuhimu wa kazi zake na kueleza tatizo la rushwa na uhujumu uchumi kwamba haliwezi kuondoka bila ya kuwa na nia au utashi wa kupambana na mambo hayo kwa vitendo.
“Rushwa si jambo jepesi, unapotaka kupambana na jambo hilo uwe tayari kuongeza maadui.”
Aidha alisema tatizo la kuingia mikataba mibovu kama vile IPTL litaondoka kwa kuwa na utaratibu wa kikatiba na kisheria na kulipa Bunge mamlaka ya kupitisha mikataba husika baada ya kuisoma na kujiridhisha kama ina tija na maslahi kwa umma.
‘Hatua hiyo ikifikiwa itajenga na kutanua uwazi, kuaminiana na uzalendo lakini pia kutapunguza kutuhumiana na kunyoosheana vidole visivyo na ushahidi, alisema Nahodha.
Kujiuzulu uwaziri
Akijibu swali la kujiuzulu kwake katika nafasi ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alisema aliwajibika kwa lengo la kuheshimu utendaji wa pamoja baada ya waliokuwa chini yake kukabiliwa na shutuma, ingawaje yeye hakuwa mhusika na mshiriki wa jambo lililodaiwa kufanyika.
“Kama Wizara ikifanya mambo mazuri sifa huwa ni za Waziri, yanapofanyika mambo mabaya unalazimika pia kukubali kuwa mambo hayakuwa mazuri, kuondoka kwako kwa aina hiyo kunatoa nafasi ya wenzako na vyombo vingine kukuchunguza na kujiridhisha, unapobaki unaweza kuwatia shaka wenzako na hushindwa kukupekua na kujiridhisha,” alisema Nahodha.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment