Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 5 November 2014

MASWALI 10 KWA MBUNGE WA IRINGA MJINI, PETER MSIGWA


Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema)

1.Jackson Kiyeyeu,  Mkazi wa Mtaa wa Mshindo:
Ukosefu wa uelewa wa sheria umekuwa changamoto kubwa  kwa wananchi  wa Jimbo la Iringa Mjini, je, kwa nafasi yako ya ubunge umewasaidiaje wananchi katika kuwajengea uwezo kisheria?
Jibu: Katika kampeni zangu niliahidi kuwajengea uwezo wapiga kura kujua haki zao kwani niliwaambia usipojua haki yako, huna haki. Ahadi ya kuwawekea mwanasheria ilitekelezwa kama nilivyoahidi na wananchi wamekuwa wakipata ushauri wa kisheria bure na hii imewajengea ujasiri wa kudai haki zao.
2. Ahmed  Istambuli  mkazi wa Makorongoni:
Mwaka 2010 tulikuchagua uwe mwakilishi wetu tukijua kuwa utatusaidia kutuwakilishia kero zetu, mara kwa mara umekuwa ukifanya chokochoko kwa viongozi wakuu wa kitaifa huoni kama hilo ni tatizo?
Jibu: Ahmed Istambul, napenda ujue kuwa hizo unazoziita ni chokocho ndizo zimefanya mambo mengi yafanyike hapa Iringa Mjini, wazungu wanasema gurudumu linalopiga kelele ndilo linawekewa grisi, hapa Iringa tunasema mtoto anayelia halali njaa. Hizo unazoziita chokochoko ndizo zimefanya baadhi ya kero kuondoka, mfano sasa hatuna shida ya maji, barabara nyingi tumepasua, na maeneo mengi tumeweka lami. Serikali inawajibika kufanya hayo maendeleo kwani wananchi wanatoa kodi, sihitaji kujipendekeza na kuwa mnafiki kwa waziri au Rais ili Serikali itimize wajibu wake.
3. Ali Simba:
Wakati wa kampeni ulitoa ahadi mbalimbali kwa wananchi wako, mimi nataka kujua tangu uingie madarakani hadi sasa ni miaka minne umefanya kitu gani? Ni ahadi ngapi umetekelezaji na kama zipo ambazo hujatekeleza ni zipi na ni lini utazikamilisha?
Jibu. Kwanza muuliza swali hajasema ni ahadi gani nilitoa, nadhani angeuliza kwa mifano, ingekuwa bora zaidi. Lakini nimkumbushe kuwa ahadi zangu zilikuwa tano tu ambazo ni kubadilisha mtazamo kutoka hasi kuwa chanya na kufuta dhana kuwa mbunge ndio mtatua matatizo ya watu. Nilisema mimi sitatoa samaki nitafundisha watu kuvua samaki. Pia niliahidi kuweka mwanasheria ofisini kwangu na nimetimiza. Pia niliahidi kusaidia wananchi ili waweze kukopesheka. Katika michezo niliahidi kutoa hamasa katika utekelezaji nikaanzisha Msigwa Cup. Niliahidi kuboresha huduma za jamii kwa ujumla japo baadhi hazijatekelezwa asilimia mia, nitajitahidi muda uliobaki kuzimalizia.
4. Haruna Mbata, mkazi wa Kigamboni:
Ninavyojua mimi, kiongozi ni mtu mwenye dhamana aliyopewa na wananchi ili awatumikie, wewe kama mbunge uliyechaguliwa na watu wa Iringa Mjini ili uwatumikie, unaweza kunieleza kwa kifupi namna ulivyowasaidia watu wenye ulemavu?
Jibu. Kama mbunge natambua mazingira ambayo siyo rafiki kwa watu wenye ulemavu, ndio maana hivi karibuni nilianda chakula cha pamoja kuendelea kukusanya kero zao na hilo lilikuwa jambo la kihistoria katika jimbo letu. Napigania huduma kwao ziweze kuwa rafiki, kwa mfano kwenye vituo vya mabasi, hospitalini, mabenki na vyuoni. Mambo mengine nitajitahidi kusaidia katika kipindi kilichobaki.
5. Isike Yakuti Mkazi wa Ngeleli:
Swali: Wakati wa kampeni mwaka 2010 uliahidi kuwa iwapo ungechaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini ungepunguza tatizo la ajira kwa vijana  katika jimbo lako, Je, unatuambia nini wakazi wa Iringa husuani tuliokuchagua?
Jibu: Hii haikuwa sehemu ya ahadi zangu, nimesema ahadi, zilikuwa tano, suala la ajira ni la kisera. Kwa sera ya CCM ya kuua viwanda ni vigumu mno vijana kupata ajira, dawa pekee kwa vijana tushirikiane kuwatosa CCM uchaguzi ujao.
6.   Samsoni  Mponzi Mkazi wa Mtaa wa Kihodombi:
Tulikuchagua uwe mwakilishi wetu kwa sababu tuliamini utatuwakilisha, lakini kwa bahati mbaya vikao vingi vya Bunge umekuwa ukitoka nje, Je, huoni kama kitendo hicho kimepunguza uwakilishi wako kwa wananchi bungeni?
Jibu: Kutoka nje ya Bunge ni sehemu ya uwakilishi, nikitoka nje maana yake sijaridhika na ubabe uliokuwa unaendelea ndani ya Bunge, kwa hiyo kutoka nje ni sehemu ya kanuni za bunge. Bunge la Katiba kulikuwa na usanii mkubwa na mimi kama mcha Mungu nisingeweza kuvumilia uovu ule ukiendelea kufanywa mbele yangu, walikuwa wanajenga nyumba kwa matofali ya barafu. Hakuna Katiba pale.
7.   Seif Rashid, mkazi wa Kibwabwa:
Wakazi wa Jimbo la Iringa Mjini walio wengi ni wakulima, kama mbunge umefanya jitihada gani kuhakikisha mazao yao yanapanda thamani na kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya mkoa wa Iringa?
Jibu. Asilimia arobaini ya wakazi wa Iringa ni wakulima, ingawa ni kilimo kidogo siyo cha kibishara sana. Japokuwa tatizo la soko ni la Serikali ambayo imekuwa ikiwazuia wakulima kuuza mazao yao wanakotaka, nikiwa bungeni nimeishauri Serikali iache kuwatia umaskini wananchi kuuza mazao nchi za nje na jitihada hizo zinaendelea.
8.   Zablon Philimoni, mkazi wa Miyomboni: 
Ulituahidi sisi wafanyabiashara ndogondogo (machinga)kuwa utatuondolea kero ya kutembeza  bidhaa kwa kututengea eneo lililopo katikati ya mji. Je, nini matarajio yako?
 Jibu: Nashukuru kwa kuona juhudi zangu za kuwatetea wamachinga ambazo zimefanya mpaka sasa niendelee kuwa na kesi mahakamani kwa ajili yenu. Kwa sababu madiwani wa CCM hawataki mfanye biashara pale mjini. Kwa muda uliobaki wanatuzidi kwa wingi wao. Ninachoweza kusema mpango wangu ni kuwa uchaguzi wa mwakani tupeni madiwani wa kutosha ili tuchukue halmashauri wamachinga wote mtafanya biashara mara mbili kwa wiki katikati ya mji yaani Jumamosi na Jumapili, Tutachagua barabara za kuzifunga.
9. Josephat  Chengula:
Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kama mbunge nini msaada wako kwa wananchi kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na uchaguzi huu?
Jibu. sidhani Kama Serikali inachukulia suala hili kwa uzito unaostahili. Ingawa mimi binafsi nimeongea kwa nguvu sana kupitia redioni na mikutano ya hadhara kuhusu umuhimu wa uchaguzi huu na kuwasihii wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la makazi.
10. Modesta Mkini:
Mheshimiwa Mbunge, Agosti 30, mwaka huu ulikutana  na sisi watu wenye ulemavu katika ukumbi wa kijamii wa manispaa ya Iringa, katika mkutano huo ulikusanya kero mbalimbali zinazoikabili jamii ya watu wenye ulemavu, je,  ni lini utaanza kutimiza ahadi hiyo ukizingatia umebakiza mwaka mmoja  kumaliza muda wako wa uwakilishi?
Jibu: Nashukuru kwa kukumbuka kuwa nilikutana nanyi, naomba muwe na subira nitafanyia kazi yote tuliyokubaliana, tukimaliza vikao vya Bunge nitaanza kushugulikia.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment