Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 20 November 2014

DK. SLAA AMVAA KIKWETE MAUAJI KITETO

Dk. Slaa amvaa JK mauaji Kiteto
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbroad Slaa, amezungumzia migogoro ya ardhi inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha mauaji ya kutisha, akisema italiweka pabaya taifa na hivyo kumshauri Rais Jakaya Kikwete, amfukuze kazi Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, vinginevyo wananchi wanaoona damu ikimwagika hawawezi kumwelewa.

Dk. Slaa pia aliwataka Watanzania wote hususani jamii za wakulima na wafugaji kuacha kupigana na kuuana wakigombea ardhi badala yake waiwajibishe Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa migogoro hiyo ni matokeo ya serikali hiyo kushindwa kuwajibika ipasavyo hasa katika kuweka mipango mizuri ya matumizi ya ardhi ambayo ni majukumu ya Serikali za Mitaa.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara ya chama hicho iliyopewa jina la ‘Operesheni Delete CCM’ akimpokea Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyezunguka mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma na Morogoro.
Alisema kuwa migogoro ya ardhi inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha umwagaji damu za Watanzania na uharibifu mkubwa wa mali ni matokeo ya kushindwa kwa sera, mipango na mikakati ya CCM, hivyo akawataka wananchi kujiandaa kukipumzisha chama hicho kutoka madarakani.
Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza kijijini Mvuha, kati ya mikutano mitano kwenye vijiji mbalimbali vya majimbo ya Morogoro Kusini, Morogoro Kaskazini na Kilosa, Dk. Slaa alisema kuwa umwagikaji wa damu huo usipodhibitiwa na migogoro hiyo kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, serikali itakuwa imeshindwa moja ya majukumu yake ya msingi ya kulinda raia wake.
“Ndugu zangu, ziara hii itanifikisha katika maeneo ambayo mnajua yamekuwa na migogoro ya ardhi…kumekuwepo na migogoro hata huku kwenu isiyokwisha ya wakulima na wafugaji kugombea ardhi…Mkoa wa Morogoro baraka ya ardhi na utajiri wa rutuba mliopewa umekuwa ukigeuka laana kiasi cha damu za watu kumwagika.
“Yanatokea sana huko Mvomero, Kilosa hata hapa kwenu (Mvuha) nimeambiwa migogoro ipo. Tunavyozungumza hivi sasa kuna matukio ya kutisha yametokea huko Kiteto, Siha, Malinyi na kwingine. Ndugu zangu, wakulima na wafugaji…ninyi wote ni Watanzania. Nawaomba sana muendelee kuishi kama ndugu kama ilivyokuwa huko nyuma,” alisema.
Dk. Slaa aliongeza kuwa hayo ni matokeo ya serikali kushindwa majukumu yake na vile vile kushindwa kwa sera za CCM, mipango na matumizi mazuri ya ardhi.
Alisema kuwa ili ardhi ya mifugo na kilimo ijulikane na matumizi mengine ni kazi za Serikali za Mitaa kupitia halmashauri, hivyo akawasihi wananchi kuwa huko kote sera za CCM zimeshindwa, kwamba ndio maana wanasema ‘delete CCM’.
“Kupitia mkutano wangu huu leo tunaitaka serikali ya Kikwete ichukue hatua za haraka sana kuzuia umwagaji wa damu unaoendelea na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ya ardhi nchini. Vinginevyo wanazidi kudhihirisha kuwa wamechoka na watakiwa kupumzishwa.
“Kwa Kiteto mojawapo ya chanzo cha mauaji yanayoendelea huko ni wanasiasa wanaoongoza wilayani humo, akiwemo Mkuu wa Wilaya, yuko Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, yupo mbunge wa jimbo ambaye amewahi kuwa waziri…mgawanyo wa ardhi ni jukumu la serikali. Hatuwezi kuangalia tu damu ya Watanzania inamwagika kama kuku. Hatuwezi. Tunamtaka Kikwete amfukuze kazi huyo DC,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa iwapo viongozi walioko madarakani sasa hawataona thamani za damu zinazomwagika kwa sababu ya wao kushindwa kutekeleza wajibu wao, iko siku watailipa kwa gharama kubwa endapo wananchi wataendelea kupoteza matumaini huku haki ikiwa haipatikani, huku akisisitiza kuwa hayo yataanza kuonekana kuanzia uchaguzi wa Desemba 14 mwaka huu.
Dk. Slaa ambaye jana alifanya mikutano katika vijiji vya Mvuha, Kisika, Ludewa, Magubike na akimaliza mkoa wa Morogoro akiingia mkoani Dodoma leo, aliwataka Watanzania katika jamii zao, zikiwemo za wakulima na wafugaji, kuacha kuuana wao kwa wao, badala yake wajue namna ya kushughulikia chanzo cha migogoro yao.
IGP aongeza nguvu Kiteto
IGP aongeza nguvu KitetoMkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu ameahidi kuongeza idadi ya askari katika kijiji cha Chekanao, Kata ya Kiperesa wilayani Kiteto mkoani Manyara kufuatia wananchi katika kijiji hicho kujitolea nyumba kwa ajili ya kuishi askari kwa lengo la kuimarisha usalama katika maeneo yao kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi inayosababisha kutokea kwa mauaji.
IGP Mangu aliyasema hayo jana wakati alipokuwa katika ziara wilayani humo ya kujionea uharibifu uliojitokeza pamoja na kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo iliyopelekea kutokea kwa vifo vya wakulima na wafugaji hivi karibuni ambapo watu kadhaa wanashikiliwa kutokana na vurugu hizo.
Alisema kufuatia kuwepo kwa umbali mrefu wa kituo cha Polisi na kijiji hicho, atahakikisha askari wa kudumu wanakuwepo ili kushirikiana na wananchi katika kuwabaini wahalifu wanaofanya vurugu na kuendeleza migogoro hiyo ambapo wananchi nao waliahidi kujenga kituo cha polisi.
Mtendaji wa Kijiji cha Chekanao, Omar Ndee alisema wamekuwa wakipata shida kutokana na umbali mrefu wa kituo cha Polisi jambo ambalo limekuwa likifanya kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu vinavyochangiwa na migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kiteto.
Watu 16 mbaroni
Katika hatua nyingine, watu 16 wamekamatwa na Jeshi la Polisi kufuatia vurugu kubwa zilizozuka za kugombea eneo la malisho katika kijiji cha Miti Mirefu, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, baina ya jamii ya kifugaji ya Kimaasai na mwekezaji wa shamba la Ndarakwai.
Akithibitisha tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema waliokamatwa jana kufuatia oparesheni ya jeshi la polisi ni jamii ya wafugaji.
Gama alisema kati yao wanaume ni 11 na wanawake watano waliokutwa na vifaa vya mwekezaji kama kompyuta mpakato (laptop), magodoro, vitanda, meza na vitu vingine vya thamani.
Mwishoni mwa wiki iliyopita watu wanaodaiwa kuwa jamii ya kifugaji, walilivamia shamba la mwekezaji huyo, ambaye pia anafanya utalii wa picha, kambi za watalii na kufuga wanyama na kusababisha vurugu ambazo zilizuka baada ya mifugo zaidi ya 300 ya jamii ya wafugaji wa Kimaasai kutoka wilaya ya Longido na nchi jirani ya Kenya, kudaiwa kuingiza mifugo yao kwenye shamba la mwekezaji huyo baada ya kukosa eneo la malisho ya mifugo yao ambapo magari na nyumba viliteketezwa kwa moto.
CREDIT: TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment