Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 24 October 2014

SERIKALI HATARINI KUIPOTEZA BENKI YA NBC


Mwenyekiti wa  Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Rajabu Mbarouk Mohammed (katikati) akizungumza na waandishi wa katika Ofisi Ndogo za Bunge, Dar es Salaam jana. Picha na Rafael Lubava   

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amesema iwapo Serikali itashindwa kulipa deni la Sh22.5 bilioni inayodaiwa na kampuni ya Absa Group Limited ya Afrika Kusini hadi kufikia Machi mwakani, itapoteza asilimia 30 ya hisa zake katika Benki ya Biashara ya NBC.
Alisema endapo Serikali itashindwa kulipa deni hilo, Benki hiyo itakuwa chini ya kampuni ya Absa ambayo ina asilimia 55 ya hisa za NBC. Awali, kampuni hiyo ilikuwa na hisa asilimia 70 za benki hiyo lakini ikauza asilimia 15 ya hisa zake kwa Shirika la Fedha la Kimataifa.
Ili kuinusuru Serikali, Zitto amemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitia mikataba yote ya Serikali na Absa katika NBC ili kubaini kilichojificha.
Serikali ilikopa kiasi hicho cha fedha ili kutekeleza agizo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo mwaka 2012 iliiagiza NBC kuongeza mtaji wa biashara wenye thamani ya Sh75 bilioni, baada ya ule wa awali kushuka kwa asilimia 12.
Jana, katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam, Zitto pamoja na wajumbe wa PAC walimbana Msajili wa Hazina, Domi Malosha wakimtaka atoe maelezo ya kina sababu za Benki ya NBC kudaiwa kiasi kikubwa cha fedha tangu mwaka 2012 na kushindwa kulipa chochote hadi sasa.
Katika maelezo yake, Malosha alisema baada ya NBC kubinafsishwa mwaka 1997, Serikali ilibaki na asilimia 30 ya hisa na Kampuni ya Absa kuchukua asilimia 70 huku akifafanua kuwa mtaji wa NBC ulishuka kati ya mwaka 2010 hadi 2012 baada ya Benki hiyo kutoa mikopo ya magari ya Sh55 bilioni.
“Baada ya mtaji wa NBC kushuka kwa asilimia 12, BoT iliagiza wanahisa wote watatu kuongeza mtaji. Kwa kuwa Serikali haikuwa na fedha za kuongeza katika mtaji, ilikopa Sh22.5 bilioni kwa Absa na kuzitoa kama mtaji kwa makubaliano ya kurejesha deni hilo ndani ya miaka miwili,” alisema Malosha na kuongeza:
“Miaka hiyo miwili inamalizika Machi 2015, hadi sasa deni hilo bado halijalipwa… kila mwanahisa anatakiwa kulipa fedha za kuongeza mtaji kulingana na hisa alizonazo NBC.”
Baada ya maelezo hayo, Zitto alimtaka Malosha kueleza sababu za mtaji wa NBC kushuka kutokana na taarifa za benki hiyo zilizoifikia PAC kutia shaka.
“Sababu ni mikopo. NBC ilikuwa ikitoa mikopo kwa watu kwa ajili ya kununua malori lakini inaonekana kulikuwa na udanganyifu wa kiasi cha mkopo na bei halisi ya malori kutokana na takwimu za (TRA) Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Taarifa zilionyesha kuwa malori yanauzwa Sh200 milioni wakati si kweli. Ukaguzi wa suala hili mpaka sasa unaendelea kwa sababu aliyekuwa akikagua mara ya kwanza aliacha ukaguzi na hakutoa taarifa yoyote, sasa kazi ya ukaguzi amepewa mkaguzi mwingine.”
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, NBC ilikuwa ikitoa mikopo lakini haifiki kwa walengwa na badala yake fedha hizo zilikuwa zikipitia kabla ya kuzipeleka kwa waombaji.
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage alisema kwa takwimu zilizopo, ni wazi kuwa Absa haikulipa kodi serikalini baada ya kuuza asilimia 15 ya hisa zake kwa kampuni ya IFC huku Zitto akimbana Malosha akitaka kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya Absa... “iweje hasara isababishwe na wengine lakini iwajibike Serikali. Hatua gani zimechukuliwa?”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kibiti (CCM), Abdul Marombwa aliyetaka kujua hatua zitakazochukuliwa iwapo mkaguzi wa sasa atashindwa kutoa ripoti mapema kabla ya Machi 2015.
Malosha alisema hatua zitakazochukuliwa zitatolewa baada ya kukamilika kwa ukaguzi wa pili, huku akisisitiza kuwa mkaguzi wa sasa hataondolewa kama wa awali na kama Serikali haitaridhishwa na ukaguzi wake, itamtumia CAG.
Maliasili yaibana Serikali
Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imeibana Serikali baada ya kubaini kwamba inachangia kulikosesha Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) Dola 20 milioni za Marekani kwa mwaka.
Serikali inadaiwa kulikosesha fedha hizo Tanapa kutokana na kuchelewa kutangaza bei mpya ya tozo ya kulala mtalii ya Dola 60 za Marekani kwa wenye hoteli ndani ya hifadhi za taifa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli alisema jana kuwa hatua hiyo ni sawa na hujuma dhidi ya Tanapa, hasa ikizingatiwa kwamba ni hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha dhidi ya kesi iliyofunguliwa na wamiliki wa hoteli hizo. Kwa sasa kila mtalii anatozwa Dola 6.
“Ni jambo ambalo linatupa maswali mengi kwani kuna hukumu ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Stella Mugasha, tangu Septemba 12 mwaka huu. Aliitaka Serikali itangaze bei hiyo mpya kwenye gazeti lake ili iwe rasmi na ianze kutumika.”
Tanapa iliiandikia Wizara ya Maliasili na Utalii ili itangaze tozo hiyo lakini hadi sasa, kumekuwa na ukimya usioeleweka, tumemuuliza Waziri, Lazaro Nyalandu leo (jana) hakuwa na jibu, hivyo kamati imeagiza watangaze haraka,” alisema Lembeli.
Alisema pia tozo ya kutembelea hifadhi za Taifa inaikosesha Serikali mamilioni ya fedha, hivyo inapaswa itolewe inayoruhusu mtalii kuingia mara moja, iwapo atatoka na kutaka kurejea siku hiyo anapaswa kulipa nyingine.
“Duniani kote wenzetu ndivyo wanavyofanya lakini sisi tunafikiri ni njama za mawakala wasio waaminifu wanatumia mwanya wa tozo moja kuingiza watalii tofauti wakitumia magari yao, tumewagundua tunataka wizara isimamie jambo hili likomeshwe,” alisema Lembeli.
Kamati hiyo pia imeikataa taarifa ya wizara hiyo inayohusu migogoro inayotokana na mipaka ya hifadhi ya taifa na wananchi iliyowasilishwa na Waziri Nyalandu jana baada ya kubaini kuwa haina vielelezo muhimu.
Ubadhirifu fedha za wafadhili
Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) imesema inahitaji kufanya ukaguzi katika mikoa miwili; uliofanya vizuri na uliofanya vibaya katika taarifa za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Rajabu Mohamed alisema wanahitaji kujua namna Sh256 milioni zilizokosa maelezo kwa taarifa kwamba zilitumiwa katika ununuzi na matumizi ambayo hayajawekwa wazi.
“Tumechagua Mkoa wa Iringa ambao ndiyo uliofanya vizuri na Mkoa wa Mwanza ambao ndiyo uliofanya vibaya ili kuangalia hatua zinazochukuliwa. Tunahitaji kujua chanzo cha ubadhirifu na kukwama kwa miradi ambayo fedha zake zilishatolewa,” alisema.
Alieleza kwamba kiasi hicho ni sehemu ya Sh616 bilioni zilizotolewa kwa halmashauri katika mwaka wa fedha wa 2010/11 kwa ajili ya miradi ya maji, kilimo cha umwagiliaji (SDP) na mingine ya maendeleo.
Alisema katika ukaguzi huo, ilibainika kwamba zaidi ya Sh16 bilioni zimetumika bila kufuata Sheria ya Ununuzi ya mwaka 2004/05, suala ambalo linahitajika kuchukuliwa hatua.
Ripoti ya CAG
Katika ripoti yake inayoishia Juni 30, 2013, iliyotolewa juzi katika Kamati ya PAC, CAG alianika matumizi mabaya ya fedha za umma. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, Tanesco ilinunua transfoma mbili kwa gharama ya Sh7.879 bilioni kwa kushindanisha wazabuni 12 kwa njia ya zabuni maalumu.
Msaidizi wa Mkaguzi Mkuu, Benja Majura Majura alisema baada ya mchakato wa awali wa kupendekeza washindani kumalizika na kamati kuwasilisha ripoti yake, Tanesco iliongeza jina la kampuni ya Shadong Taikai Power Engineering, ambayo haikuwa kwenye orodha ya awali ambayo ilipitishwa na bodi ya zabuni ya shirika kuwa mshindi wa zabuni husika.
Aidha, ripoti hiyo imesema kwamba ukaguzi katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ulibaini kuwa Sh214.5 milioni zilitolewa kwa wanafunzi walioshindwa mitihani na kutoendelea na chuo na wengine walioahirisha masomo ikivitaja vyuo hivyo na kiwango kwenye mabano kuwa ni Algeria na Cuba (Sh132 milioni), Chuo Kikuu cha Dodoma (Sh43.9 milioni), Chuo cha Usimamizi wa Fedha - IFM (Sh28.9 milioni) na Chuo Kikuu cha Urusi (Sh9.6 milioni).
Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa Mgodi wa Southern Paper Mills uliuzwa kwa Kampuni ya Rai Group ya Kenya kwa bei ya Sh1.68 bilioni wakati thamani halisi ni Sh43.68 bilioni.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa Chuo cha Ufundi Mpanda kina mashine zenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni ambazo zimetelekezwa na kwamba menejimenti ya Mamlaka ya Vyuo vya Ufundi Stadi (Veta) ingepaswa kuweka mikakati ya kuhamisha mashine hizo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu jinsi ya kuzitumia kulingana na utandawazi badala ya kuzitelekeza.

Imeandikwa na Fidelis Butahe, Beatrice Moses na Andrew Msechu.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment