Hayati Baraka Abdallah Kitenge, aliyefahamika kama 'Askari' au 'Zagallo'
Na DANIEL MBEGA
WAPENZI wa kandanda walimwita 'Askari au Zagallo'
wakimfananisha na beki nambari mbili wa Brazil enzi hizo, Mario Jose Lobo
Zagallo, kwa uwezo wake wa kumchunga adui barabara uwanjani. Lakini jina lake halisi
ni Kitenge Abdallah Baraka Said, beki nambari mbili wa zamani wa Young Africans
aliyeichezea timu hiyo kwa miaka mitano.
Mzaliwa wa Tabora, mwaka 1942, Kitenge Baraka alivua jezi
mapema mwaka 1971 baada ya miaka 20 ya uchezaji. Alianza kulisukuma gozi akiwa
na miaka nane na aliendelea na ari ya kuupenda mchezo huo wa kandanda alipoanza
masomo ya msingi shule
Town School
hadi sekondari Kazima Sekondari zote za mjini Tabora.
Alishamiri zaidi kimpira wakati bado akiwa mwanafunzi wa
sekondari huko Kazima. Kwa kipindi cha miaka minne ya sekondari (kuanzia 1961
hadi 1965), pamoja na kuchezea timu ya hapo shuleni, Kitenge Baraka alikuwa
mpenzi na mchezaji wa Young Boys ya Tabora aliyoiwakilisha katika michezo ya
ligi. Wakati huo alikuwa akichezea nafasi ya mshambuliaji nambari 9. Nafasi
nyingine alizowahi kuchezea ni wingi ya kulia (nambari 7), sentahafu (mkoba -
5) na beki nambari mbili, nafasi aliyoichezea hadi alipostaafu.
Mwishoni mwa 1965 baada ya kumaliza kidato cha nne
alikuja mjini Dar es Salaam na kuajiriwa na Shirika la Upakiaji na Upakuaji
Mizigo Bandarini (East African Cargo Handling Services, sasa Tanzania Harbours
Authority). Mara tu alipowasili Dar es
Salaam viongozi wa klabu za soka mjini humo walianza
kumshawishi ajiunge na timu zao, kwani hakuwa mgeni kwao. Walikwisha muona
akishiriki mashindano ya Sunlight Cup (sasa Taifa Cup) akiwa na timu ya mkoa wa
Tabora (Western Province ). Lakini chaguo lake likawa
Yanga, aliyojiunga nayo mwaka 1966.
Mwaka huo huo alichaguliwa kuunda timu mchanganyiko ya
mkoa wa Dar es Salaam
(Mzizima United) kugombea Kombe la Taifa. Pamoja naye walikuwemo wanasoka wengine
mashuhuri wa nyakati hizo, akina Emmanuel Albert Mbele 'Dubwi', Abrahaman
Lukongo, golikipa Kitwana Ramadhan Manara 'Popat' ambaye baadaye alikuja
kubadilisha nafasi na kuwa mshambuliaji hatari wa Yanga na Taifa Stars, Arthur Mambetta, Mustafa Choteka, na
wengineo. Hakuwahi kuachwa katika orodha ya Dar-Kombaini (mara nyingine Pwani)
mpaka alipoamua kutundika njumu ukutani. Anakumbuka mwanandinga huyo katika
mahojiano yaliyofanyika mwaka 1984.
Mwaka 1967 alipata fursa ya kuliwakilisha taifa katika
mashindano ya Kombe la Afrika Mashariki (Kombe la Chalenji) na Kombe la Nchi
Huru za Afrika (sasa Kombe la Mataifa Afrika), Madagascar na hapa nyumbani na
aliendelea kuichezea Taifa Stars kwa miaka mitatu.
"Nilivutiwa sana
na mchezaji Ramadhan Abdallah 'Kitumbo' aliyekuwa mshambuliaji wa timu ya Mkoa
wa Tabora na timu ya Taifa (Tanganyika ),
ambapo sifa zake zilinifanya niwe mwanasoka. Kweli nilifanikiwa," alisema
Kitenge Baraka.
Mchezo mgumu kuliko yote ambayo Kitenge amewahi kucheza
katika historia yake ni baina ya Yanga na Asante Kotoko ya Ghana mwaka
1969 kuwania Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika. Katika mchezo huo wa robo
fainali timu zilikwenda sare baada ya dakika 210 za mchezo ugenini na nyumbani
(Kumasi na Dar es Salaam ). Kwa kuwa
sheria ya penati tano tano ilikuwa haijaanza kutumika, Asante Kotoko, mabingwa
wa Afrika mwaka 1969 na 1970, walipata ushindi wa shilingi. Michezo yote
ilikuwa migumu kwa kuwa timu zote zilicheza mtindo unaofanana.
Akizungumzia kuhusu wacheza wa enzi zake, aliwasifu sana Maulidi Dilunga
'Mtoto wa Mexico '
na Gilbert Mahinya 'Machine', ambao alisema kwamba aliwahusudu kutokana na
bidii yao
uwanjani na uwezo wa kupachika mabao. "Japokuwa Gilbert Mahinya alikuwa
mchezaji wa kiungo, lakini aliweza kucheza mbele na nyuma bila kuchoka na
kufunga mabao ya pembeni sana
(impossible angles) tokea umbali wa mita 30 na zaidi," alisema.
Wachezaji wa miaka ya '80 waliokuwa wakimvutia walikuwa
Athumani Juma 'Chama' mchezaji bora kwa mwaka 1983 na 1984 na Hamisi Ramadhani
'Kinye' golikipa wa Yanga na Taifa Stars.
"Kumekuwa na hali ya kuridhisha katika kabumbu hivi
sasa kutokana na mbinu za kisasa wanazofundishwa wachezaji wetu na walimu
mbalimbali. Isipokuwa wachezaji bado wanashindwa kuzingatia miiko inayotawala
mchezo wa mpira hasa nyakati za mashindano makubwa. Fedha zimetawala mawazo ya
wachezaji wengi, lakini pamoja na tamaa ya baadhi ya wachezaji hali ya soka
imepanda," alisema Kitenge.
Msukuma ndinga huyo wa zamani, ambaye ni baba mzazi wa mtangazaji nguli wa michezo nchini, Maulid Baraka Kitenge 'Mshambuliaji', alifariki dunia Agosti 21, 2013 na kuzikwa jijini Dar es Salaam.
MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALI PEMA. AMEN!
WASIFU WAKE:
Kuzaliwa: 1942
Mahali: Tabora
Kufariki: 21 Agosti, 2013
Jina la utani: Askari au Zagallo
Nafasi uwanjani: Beki 2
Alianza kucheza soka: Akiwa na miaka 8
Klabu: Young Boys (Tabora) 1961 - 1965; Yanga (Dar) 1966 - 1971.
Timu ya Mkoa wa Tabora (Western Province ): 1963 - 1965.
Timu ya Mkoa wa Pwani (Mzizima United): 1966 - 1971.
Mafanikio: Robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika (Yanga) 1969; Ubingwa wa Taifa (Yanga) 1968, 169, 1970, 1971.
Daniel Mbega ni mwandishi mwandamizi nchini ambaye amefanya tafiti mbalimbali kuhusu michezo na muziki katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Makala haya ni sehemu ya muswada wake wa 'UBINGWA WA SOKA TANZANIA' ambao uko kwenye hatua ya uhariri. Anapatikana kwa simu namba +255 656 331 974.
No comments:
Post a Comment