Pages

Pages

Pages

Wednesday 1 October 2014

KINANA AKERWA VIONGOZI KUJIFANYA MIUNGU-WATU

Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana

Na Mary Geofrey
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Abdulrahman Kinana, amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kujifanya miungu watu.

Aidha, amekemea baadhi ya viongozi wa CCM kufanya maamuzi ya Chama kwa kutumia vichwa vyao badala ya katiba ya Chama, kanuni na taratibu.

Kinana alitoa wito huo jana wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani Mlalo mkoani Tanga baada ya kupokea taarifa ya Chama na Serikali.



“Chama hiki kinaongozwa na kanuni na taratibu kwa mujibu wa katiba ya CCM, haruhusiwi kiongozi kutoa mwongozo kutoka kwenye kichwa chake, kujifanya miungu watu na kuamua mambo kienyeji enyeji,” alisema Kinana.

Alisema hakuna kitu kibaya kama kiongozi mwenye mabavu na kiburi kutumia mabavu yake kuwaongoza wananchi.

Kinana alisema lazima viongozi wa CCM wafanye maamuzi na kukiendesha chama hicho kwa kufuata katiba na siyo vichwa vyao huku akikemea wale wanaojifanya miungu watu.
“Sifa ya kiongozi mzuri siyo kuwa mtawala, bali ni kuwaongoza wenzake kwa kutumia kanuni na taratibu,” alisema Kinana.

Sambamba na hilo, pia aliwataka wagombea na viongozi wa CCM, kujiepusha na tabia ya kuahidi  ahadi hewa ambazo zinakuwa kitanzi kwao.

Alisema ni vyema wagombea wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, kujiepusha na ahadi zilizo nje ya uwezo wao. “Acheni kutafuta sifa mbele za watu ili mpigiwe makofi, hakikisha ahadi unayotoa unaweza kuitimiza, achana na sifa ambazo zitakuja kuwa kitanzi siku za mbele,” alisisitiza Kinana.

Alifafanua kuwa matokeo ya ahadi hewa yanasababisha wananchi kukichukia Chama na kukiona kuwa kinatoa ahadi hewa ambazo hazitekelezeki.

“Usione wananchi wanasikiliza ukadhani hawana kumbukumbu, tena kwa sasa wanatumia simu zao kurekodi kila kiongozi jambo ambalo analizungumza,” alisema Kinana.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment