Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 20 October 2014

HALIMA MDEE AMSHUKIA CHENGE

Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee

Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (Bawacha), limemshukia aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum la Katiba (BMK), Andrew Chenge, kwamba hakuwa na sifa za kusimamia uandishi wa Katiba iliyopendekezwa na Bunge hilo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, ambaye pia ni Mbunge wa Kawe ambapo alisema Chenge na wenzake, wamechakachua maoni ya wananchi na kupenyeza maoni yao ili kulinda maslahi yao.

Mdee aliyasema hayo juzi jioni wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara kwenye uwanja wa Furahisha ikiwa ni sehemu ya ziara ya Bawacha katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Magharibi ya kuwaelimisha wananchi kuhusu mchakato wa Katiba mpya na kuwashawishi waikatae Katiba iliyopendekezwa na BMK kwa kuipigia kura ya hapana kwa kuwa imeacha maoni ya wananchi.

Katika mkutano huo ambao wakazi wengi wa Jiji la Mwanza walijitokeza, Mdee alisema lilikuwa ni kosa kubwa kumpa Chenge jukumu kuandika Katiba kwa kuwa rekodi yake ya utumishi wa umma inaonyesha kwamba anakabiliwa na tuhuma za kukosa uadilifu, hivyo asingeweza kukubali maoni ya wananchi ya kuwadhibiti viongozi wanaokwenda kinyume cha maadili.

Mdee alisema kuwa Chenge alichukua jukumu la kuongoza Kamati ya Uandishi ili kuzima maoni yaliyotolewa na wananchi kupitia Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba, ambayo pamoja na mambo mengine, ilipendekeza kuwabana vigogo kufungua akaunti nje ya nchi.

“Lilikuwa kosa kubwa sana kumpa jukumu hilo, kama mzee wa vijisenti isingekuwa rahisi kuacha kama yalivyo maoni yaliyokuwa yamependekezwa na wananchi kwa kuwa anajua yangewabana katika kufanikisha mambo yao,” alisema Mdee.

“Chenge  na wenzake wamechakachua maoni ya wananchi na kupenyeza ya kwao pamoja na kumpa Rais madaraka makubwa ili kufanikisha mambo yao, waliogopa kwamba wangeacha maoni ya wananchi ya kupunguza madaraka ya Rais ya kuteua viongozi mambo yao yasingefanikiwa,” alisema Mdee.

Aliongeza kuwa Chenge hawezi kutenganishwa na mikataba mibovu ambayo Tanzania imeingia na kuisababishia athari kubwa kwa kuwa alihusika kuisaini akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwamba alipoulizwa kuhusiana na fedha kiasi cha Dola za Marekani milioni moja zilizokutwa ughaibuni zilizotokana na mkataba wa ununuzi wa rada ya kijeshi kutoka Uingereza katika akaunti yake, alisema kuwa ni vijisenti.

“Watanzania hawatakubali kuona Katiba yao inachakachuliwa,” alisema huku kundi kubwa la wananchi waliokuwa katika mkutano huo wakinyoosha mikono ya kupinga Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba.

Aliongeza: “Hawa wanataka kuendesha nchi kihunihuni kama wanavyotaka wao, na sisi hatutakubali, tutaenda nao hivyo hivyo kihunihuni.”
Kadhalika, alisema wamempatia madaraka makubwa Rais ya kuteua viongozi ili kulinda maslahi yao.

Rasimu ya Jaji Warioba ilipendekeza Rais apunguziwe madaraka ya kuteua viongozi kwa kupendekezwa kuwa baadhi ya taasisi zitumike kupendekeza majina ya viongozi kabla ya kuteuliwa pamoja na Bunge kupewa madaraka ya kuthibitisha uteuzi wa viongozi waandamizi wa serikali.

Hata hivyo, BMK lilipindua mapendekezo hayo na kupendekeza kwamba viongozi ambao uteuzi wao utapaswa kuendelea kuthibitishwa na Bunge ni Waziri Mkuu na Makamu wa Rais aliyechaguliwa na Rais (Running Mate) pale ambapo atapoteza sifa ya kuendelea na wadhifa wake na kuteuliwa mwingine.

Viongozi ambao Tume ya Warioba ilipendekeza uteuzi wake uthibitishwe na Bunge ni mawaziri na manaibu mawaziri, katibu mkuu kiongozi, mwanasheria mkuu wa serikali, jaji mkuu na naibu wake, mtendaji mkuu wa mahakama, katibu wa tume ya utumishi wa umma, mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na makamu wake, msajili wa vyama vya siasa, mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali na mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu na makamu wake.

Chenge alipotafutwa kwa simu jana hakupatikana baada ya simu yake kuita bila majibu.

Katibu Mkuu wa Bawacha, Grace Tendega, alisema wako tayari kuzunguka nchi nzima kuwaelimisha wananchi kuhakikisha hawaipitishi Katiba hiyo.

Alisema Bawacha watahakikisha wanapambana kukomesha uchakachuaji wa maoni ya wananchi kwa kushirikisha nguvu kubwa ya Watanzania milioni 40 wanaowaunga mkono.

“Haijalishi kwamba wabunge wetu katika Bunge la Katiba walikuwa wachache na CCM wakatumia nafasi hiyo kuchakachua maoni ya wananchi, nataka niwaambie kwamba sisi hatujali hiyo kwa kuwa tunao Watanzania wengi wanaotuunga mkono ambao hawajafurahishwa na uchakachuaji huo, tutakaoungana nao kuhakikisha katiba hiyo haipiti,” alisema Tendega.

Ziara hiyo ya viongozi wa Bawacha ililitetemesha Jiji la Mwanza baada ya wakazi wa Jiji hilo juzi jioni kulazimika kusimamisha shughuli zao kwa zaidi ya saa moja kupisha msafara mkubwa uliosindikiza viongozi hao waliokuwa wakielekea katika ofisi za Kanda za Chadema baada ya mkutano huo huku wakiimba nyimbo mbalimbali na kusababisha daladala na magari yaliyokuwa yakitumia barabara ya kuelekea Uwanja wa Ndege kusimama kwa muda.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment