Pages

Pages

Pages

Thursday 4 September 2014

NAWAKUMBUSHA TU: MUUNGANO UKIFA NA CCM ‘KWISHINEI’, NDIYO MAANA WANAPIGANA KUULINDA!


Huko nyuma nimetumia maneno mwelekeo wa Chama bila maelezo. Inafaa sasa nieleze maana yake. Ili kusisitiza umuhimu wake. Kujenga nchi si jambo rahisi. Kujenga Tanganyika tuliyorithi, iwe Taifa moja imara lisingekuwa jambo rahisi. Tulikuwa tumeanza. Na kujenga Zanzibar tuliyorithi, iwe taifa moja imara, isingekuwa kazi rahisi.
Mimi naamini kuwa kutokana na historia yake, ya nyuma na ya karibu, kuifanya Zanzibar kuwa Taifa moja imara, kungekuwa kazi ngumu zaidi kuliko kuijenga Tanganyika na kuyafanya makabila yake kuwa kitu kimoja. Lakini hatukuruhusiwa kujua. Historia haikuturuhusu kujenga Tanganyika kuwa Taifa, wala kujenga Zanzibar kuwa Taifa. Wa Bara tulikuwa raia wa Tanganyika huru tangu tarehe 9 Desemba, 1961 mpaka tarehe 26 Aprili, 1964; muda wa miaka miwili, na miezi minne, na siku kumi na saba, ukiihesabu na siku ya tarehe 26 Aprili, 1964.
Mimi nilikuwa Rais wa Tanganyika kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne na siku 17 hizo hizo. Wala historia haikuturuhusu kujenga Zanzibar iwe Taifa. Uhuru wa kutoka kwa mkoloni ulipatikana tarehe 10 Desemba, 1963: na Mapinduzi ya kung'oa usultani wa Mwarabu yalifanywa tarehe 12, Januari 1964. Hatukujenga nchi mbili. Badala yake tukafanya kitendo cha pekee katika historia nzima ya Afrika huru.
Tanganyika tuliyokomboa kutoka kwa Wakoloni, lakini hatukuiunda, mipaka yake ni ya kurithi; na Zanzibar' tuliyonyakua kutoka kwa Wakoloni na Masultani wa Kiarabu, lakini hatukuiunda, mipaka yake ni matokeo ya unyang'anyi na unyang'au wa Waingereza na Wajerumani, tukaziunganisha zikawa nchi moja. Tan­zania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru. Nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka katika Ukoloni. Tanzania ni ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe, baada ya kukomboa sehemu zake ilivyo kutoka katika ukoloni.
Wako Watanzania wa ajabu kabisa wanaosema kuwa uamuzi huo, au vyombo vilivyotumiwa, au njia iliyotumiwa, au vyote, havikuwa halali. Hao hawana shaka na uhalali wa Tan­ganyika, ambayo iliunganishwa na Wajerumani, na ikamegwa-megwa na Waingereza na wenzao. Kwa hao kama Rwanda na Burundi na Tanganyika zisingetengwa na mabeberu, tukazirithi kama zilivyokuwa chini ya Wajerumani, wasingeushuku uhalali wa nchi Moja hiyo. Lakini kama baada ya uhuru, Rwanda na Burundi na Tanganyika zingeamua kuungana ziwe Nchi Moja, kwa utaratibu wo wote ambao zingekubaliana, "Wazalendo" hawa wangesema muungano huo si halali!
Pwani ya Tanganyika na Zanzibar ya sasa zilikuwa pamoja kwa muda mrefu sana kabla ya kutengwa na Wakoloni Waingereza na Wajerumani.
Kama zingebaki zimetengana, kwa "wazaIendo" hao hiyo ingekuwa ni halaIi, maana zilitengwa kwa hila na mitutu ya bunduki za Mabwana. Lakini uamuzi wa Tanganyika huru na Zanzi­bar huru kuungana, na hivyo kuwaunganisha tena ndugu waliokuwa wametengwa na Mabeberu, tendo hila kuna viongozi wetu wanaosema kuwa halikuwa halali.
Hatukutafuta maoni ya watu kwa njia ya demokrasia wanayoijua wao. Wajerumani na Waingereza walitafuta maoni ya wazee wetu kwa mtutu wa bunduki! Hiyo iIikuwa halali. Nchi walizoziunda kwa njia hizo zilikuwa halali. Tunatakiwa tujivunie Utanganyika na Uzanzibari uliopatikana kwa njia hizo; lakini tuuonee haya Utanzania, tunda la uhuru wetu wenyewe.
Sikuamini kuwa wakoloni walifaulu kiasi hiki katika kuzinywesha kasumba na kuzitawala akili za baadhi yetu!
Nilitoka nje ya mstari. Narudia: Tulikuwa Nchi Mbili, lakini kwa hiari yetu wenyewe, tukaamua kuwa Nchi Moja. Kwa sabaabu ambazo nimezieleza mara nyingi, na kama hapana budi nitaendelea kuzieleza, tukakubaliana kuwa ni Muungano wa Serikali Mbili. Aidha, tulikuwa na vyama viwili vya ukombozi, TANU na ASP. Na ni vizuri kuendelea kuwakumbusha wale ambao wangependa tusahau, kwamba TANU na ASP vilikuwa yyama vya ukombozi, havikuwa vyama vya uongozi.
Hatua ya pili katika historia ya kuijenga Nchi yetu, tuliichukua tarehe 5 Februari, 1977, miaka 13 baada ya Muungano. TANU na ASP, Vyama vyetu vya Ukombozi, ambavyo vilijua kuwa Umoja ni silaha kubwa ya Ukombozi, viliungana vikawa chama kimoja, Chama Cha Mapinduzi, CCM chama ambacho kina nasaba inayofanana na nasaba ya Tanzania. Tanzania ni Tanganyika na Zanzibar, na CCM ni ASP na TANU.
Sitaki kusema kuwa CCM nayo ni lulu ya Afrika, lakini naeleza tu mwelekeo wa historia ya nchi yetu na vyama vya ukombozi wetu. Tuliokwisha kuunganisha nchi mbili zikawa nchi moja, sasa tukaunganisha vyama viwili vikawa chama kimoja. Hiyo haikuwa hatua ndogo hata kidogo katika kujenga nchi yetu. Kuna nchi gani nyingine zilizofanya hivyo? Vyama tunavyoviona katika Bara letu siku hizi vinashindwa hata kuunganisha mbinu tu, ili viweze kushinda wapinzani wao katika uchaguzi. TANU na ASP vilikuwa vyama viwili na vyote vikitawala. Vikajiua kwa hiari iIi vizae chama kimoja kiongoze na kuendeleza historia ya nchi yetu.
Tumejenga nchi ambayo ilikuwa inaheshimiwa duniani kote, ndani na nje ya Afrika. Mwaka huu tumetimiza umri wa miaka thelathini. Kama si maajabu haya yaliyozushwa bure na viongozi wetu watukufu, ilitupasa kushangilia sana umoja wa nchi yetu, na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha hapa salama.
Tungali na Serikali Mbili, lakini tuna Serikali moja tu ya Muungano. Na nani hawezi kuona kwamba hapo haja ya kubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali Mbili itakapodhihirika, historia ya Nchi yetu na mwelekeo wa chama chetu vitatuongoza kwenye muundo wa Serikali moja? Kitu kimoja ambacho hatuwezi kutazamia ni kwamba siku moja Nchi Moja hii itakuwa nchi mbili, kwa uongozi wa CCM. Lakini hiyo ndiyo shabaha ya kuwa na Serikali ya Tanganyika. Na hata kama wajinga na wapumbavu hawatambui hayo, bado hayo ndiyo yatakayokuwa matokeo ya ujinga wao: ukifufua Tanganyika, utaua Tanza­nia. Kwa uongozi wa CCM?
Ila narudia tena,
Niliyokwisha kunena,
Sera hii, nilisema,
Si ya umma ni ya chama,
Ni Sera ya Viongozi,
Wa Chama Cha Mapinduzi,
Na waungao mkono,
Uvunji wa Muungano.
Chama hiki Mapinduzi,
Kimeleta mageuzi,
Si Chama pekee tena,
Viko aina aina
Na Chama Cha Mapinduzi,
Watambue Viongozi,
Ni Chama cha Muungano,
Si Chama cha Utengano.
Kama mwanachama wake,
Hazipendi sera zake,
Atoke, asichelewe,
Aanze chake mwenyewe.
Kama viongozi wetu,
Hawapendi sera zetu,
Watoke waende zao,
Waanzishe vyama vyao.
Viko vyama bozibozi,
Vyatafuta viongozi,
Waende waviongoze,
Na hiki tukipongeze
WASlTEKE CHAMA NYARA,
WAKILAZIMISHE SERA,
AMBAZO KATU SI ZAKE,
NI ZA WAPINZANI WAKE
HASA KAMA SERA KAMA ZINO
ZA KUVUNJA MUUNGANO

CHAMA CHA MAPINDUZI kitakapobadili sera yake ya Muungano wa Serikali Mbili, sera yake mpya itakuwa sera ya Muungano wa Serikali moja. Chama Cha Mapinduzi chenye wanachama wenye akili, na ukweli, na ujasiri, hakiwezi katu kukubali sera ya serikali tatu, kikijua wazi wazi kwamba matokeo na shabaha ya sera hiyo ni kuiua, na kuizika Tanzania. Chama Cha Mapinduzi kikiwa na msimamo huo, na wala kisiuonee haya, Tanzania itadumu.

REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)

No comments:

Post a Comment