Pages

Pages

Pages

Friday 15 August 2014

SERIKALI YA TANGANYIKA HAIWEZI KUWADHIBITI VIONGOZI WANAOKIUKA KATIBA



Masuala mawili hayo,
(i) Msimamo wa Zanzibar kuhusu utaratibu wa kuchagua Makamu wa Jamhuri ya Muungano, na
(ii) Zanzibar kuingia katika OIC ndiyo yaliyokuwa sababu ya ujumbe wa mara kwa mara kati yangu na Rais wa Jamhuri ya Muungano; na ndiyo Rais na mimi tulikuwa tukiyazungumza Butiama, tarehe 2 Agosti, 1993. Baada ya kuyazungumza kwa muda mrefu na kuelewana nini la kufanya, Rais akanifahamisha kwamba Waziri Mkuu kamletea habari kwamba:
(a) Wabunge 44 wamejiandikisha kupeleka bungeni hoja ya kudai Selikali ya Tanganyika;
(b) Kwa maoni yake hoja hiyo ikijadiliwa bungeni, baadhi ya mawaziri wataiunga mkono na yeye atapata tatizo la kuipinga au kuiunga mkono.
(c) Anapendekeza ifanywe semina ya wabunge wote na viongozi wa Zanzibar, ikiwamo Serikali na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ili hoja hiyo izungumzwe na ipingwe nje ya Bunge na
(d) Rais aniombe nikubali kushiriki katika Semina hiyo. Nilimwambia Rais kwamba niko tayari kushiriki katika semina iliyopendekezwa na Waziri Mkuu;

Lakini kwa kuwa tunakubaliana kwamba hoja ya wabunge ni matokeo ya msimamo wa Zanzibar kuhusu masuala mawili hayo, itafaa “tuyamalize" kabla ya kukabiliana na wabunge.

Sikusema kuwa tusipoyamaliza vema; sitapinga hoja ya wabunge; nilisema, nadhani kwa kusisitiza, kwamba hoja hiyo kwa vyo vyote mimi nitaipinga; lakini "hali ya hewa" itakuwa ni tofauti kama hoja inapingwa baada ya Zanzibar kukubali, au kukataa kubadili msimamo wake, na Selikali ya Muungano itakuwa imeonyesha msimamo gani katika masuala hayo.

DAR ES SALAAM 5:8:1993
Kikao tulichofanya Dar es Salaam kuendeleza mazungumzo haya tulikuwa na Rais na Makamu wake wote, na Waziri Kiongozi na viongozi wengine wa Zanzibar, na Manaibu wa Katibu Mkuu wa CCM. Katibu Mkuu, hakuwepo. Pamoja na kwamba mazungumzo haya yalikuwa magumu, lakini tulikubaliana katika kikao hicho:
(i) Zanzibar itoke katika IOC;
(ii) Tukubali mapendekezo ya Kamati ya Bomani kuhusu utaratibu mpya wa kuchagua Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano;
(iii) Hoja ya Serikali Tatu ipingwe, na mimi nisaidie kuipinga; na
(iv) Kamati Kuu iitwe ili itoe uamuzi wake rasmi kuhusu masuala haya.
Siku hiyo baadhi ya wabunge, viongozi wa hoja ya Serikali Tatu, waliomba kuja kuonana nami Msasani.
Tulizungumza kwa muda mrefu; na wote walisema; wakieleza sababu zao za kudai Serikali ya Tanganyika. Nilisisitiza kwao kwamba zote zilikuwa ni sababu za kuwataka wawadhibiti viongozi wetu na kuwataka watuongoze kwa kufuata sheria na, Katiba ya Nchi yetu.
Hapakuwa na sababu hata moja ya kuwafanya wadai Serikali ya Tangan­yika, maana hata ukiwa na Serikali ya Tanganyika bado viongozi wetu wanaweza kukiuka sheria na Katiba ya Nchi, na dawa haitakuwa ni kuigawa nchi tena na kuongeza serikali.
Bali ni kuwadhibiti viongozi wahalifu. Baadaye hoja hizi nilizirudia bungeni.

Siku iliyofuata, tarehe 6:8:1993, mimi niliondoka kwenda Brussels, Ubelgiji, kumwakilisha Rais katika mazishi ya Mfalme wa nchi hiyo. Huku nyuma Kamati Kuu iliitwa. Niliporudi tarehe 9:8:1993 Kamati hiyo ilikuwa inakutana Dares Salaam. llipokwisha kufikia uamuzi wake, viongozi waliotumiwa kuja kunieleza uamuzi huo walikuwa ni Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa CCM, na Waziri Kiongozi. Msemaji wao alikuwa Katibu Mkuu.

UAMUZI WA KAMATI KUU: 10:8:1993
(i) OIC: Zanzibar itoke;
(ii) MAKAMU WA RAIS: Mapendekezo ya Kamati ya Bomani yakubaliwe;
(iii) HOJA YA SERIKALI TATU: Ipingwe;
(iv) SEMINA: Isifanyike; badala yake mazungumzo yafanyike katika kamati ya Chama ya Bunge.

Baadaye Rais alinifahamisha kwa simu kwamba yeye sasa alikuwa hakusudii kwenda kusema na wabunge, lakini akanitaka mimi niende. lnaelekea kuwa baadhi ya viongozi waliona kuwa Rais akienda kusema atawazuia wabunge wenye hoja kutoa dukuduku zao bila hofu.

Kwa kuwa nilikuwa nafahamu kwamba baadhi ya viongozi wa Chama na Selikali walikuwa na maoni hayo hayo kuhusu kushiriki kwangu, nilimwambia Rais kwamba hata na mimi nisiende kusema bungeni. Na kwa vyo vyote vile kushiriki kwangu kulitegemea kushiriki kwake; lakini kama yeye haendi kusema na wabunge, mimi nitakwenda kama nani na kutafuta nini? Kwa hiyo yafaa wote wawili tusiende. Tukakubaliana hivyo.

NYUMBANI KWA RAIS: 13:8:1993
Baadaye Rais akanipigia simu tena na kuniambia kuwa Waziri Mkuu alipoelezwa makubaliano yetu ya kutokwenda kusema na wabunge amechachamaa. Nikamwomba Rais amwambie Waziri Mkuu asiondoke ili niende wote watatu tuzungumze la kufanya. Nikaenda; tukazungumza kwa muda mrefu. Waziri Mkuu akanisihi sana sana, niende bungeni, nikasaidie kupinga hoja ya Serikali Tatu. Nikakubali, nikasisitiza mambo mawili:
(i) Rais awe ndiye msemaji mkuu na mimi niwe msaidizi tu; na
(ii) Uamuzi wa Zanzibar kutoka katika OIC; na wa kukubali utaratibu wa kuchagua Makarnu uwe umekwisha kutangazwa.
Nilisiliitiza kwamba itafaa uamuzi wa Zanzibar kutoka katika OIC uelezwe wazi wazi, na bila kuvungavunga, ili makali ya wabunge, kama ikiwezekana, yawe yamepunguzwa kabla hatujapinga hoja ya Selikali Tatu,

Tulipokwisha kukubaliana hivyo Waziri Mkuu alifurahi sana na kusema kwa Kiingereza: "I could not take No for an answer! Nisingekubali jibu la Hapana! Tukaachana.

BUNGENI: 14:8:1993
Kesho yake tarehe 14:8: 1993 tulikwenda bungeni.
(i) Nadhani jana yake Waziri Mkuu alikuwa amekwisha kutanga uamuzi wa Zanzibar kutoka katika OIC, na wakubali mapendekezo ya Kamati ya Bomani kuhusu utaratibu wa kuchagua Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Na kwa upande wa Zanzibar Rais wa Zanzibar alikuwa amekwisha kufanya hivyo. Bungeni Waziri Mkuu alieleza sababu za kutuomba tuseme na wabunge.
(ii) Rais alieleza historia ya kisa cha OIC na uamuzi wa Zanzibar kujitoa. Akapinga hoja ya Serikali tatu.
(iii) Mimi nilieleza kwa kirefu sana ile migogoro miwili ya awali. Pia kupinga hoja ya Serikali Tatu. Katika kufanya hivyo nilieleza historia ya Muungano wa Serikali Mbili, badala ya serikali moja au shirikisho la serilali tatu.


REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA

No comments:

Post a Comment