Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 10 August 2014

NARUDIA TENA, WAZANZIBARI WALIUKATAA MUUNGANO MWAKA 1992, SERIKALI YA MKATABA NI GERESHA TU

Mwalimu Julius Nyerere (kushoto) na Sheikh Abeid Amani Karume wakibadilishana Hati za Muungano mwaka 1964


Na Daniel Mbega

WAJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba wako Dodoma, wanatumia mabilioni ya fedha za walipa kodi kwa matarajio ya Watanzania wengi kupata Katiba Mpya.
Hata hivyo, mvutano wa muundo wa serikali ndiyo changamoto kubwa inayowakabili kiasi cha kushuhudia wajumbe kutoka vyama vya upinzani kuamua kujitoa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Tangu walipoondoka katika awamu ya kwanza, mpaka sasa bado wameshikilia msimamo wao huo kwamba hawatakwenda Bungeni kwa kuwa wanaamini CCM inataka kuchakachua Rasimu ya Katiba mpya na kupitisha mfumo wa serikali mbili badala ya tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Warioba.
Lakini ndani ya msuguano huo, kuna hawa Wazanzibari ambao tangu wakati wa vuguvugu la kukusanya maoni, walikwishasema kwamba wao wanaitaka Tanganyika iwepo ndani ya Muungano ili wajue nchi waliyoungana nayo, kwa sababu katika muungano wa sasa haitajwi kabisa.
Wazanzibari wamekuwa vinara wa kuwasemea Watanganyika katika kuidai Tanganyika. Lakini wanakwenda mbali kuhusu Muungano ambapo wamependekeza uwe muungano wa mkataba na siyo kama ulivyo sasa kwa sababu unawaminya wao na kuwakandamiza. Kwamba hauna ridhaa ya walio wengi.
Ukiingia kwa undani sana unagundua kwamba, kelele zao za kuwapigania Watanganyika waipate Tanganyika yao – jambo ambalo ni jema kabisa katika kurejesha utaifa wa Watanganyika – lakini utagundua kwamba kuna mbinu chafu nyuma yake kwamba mara tu Tanganyika itakapopatikana ama kurejeshwa, basi hoja yao ya kuukataa muungano itakuwa na nguvu zaidi hasa kwa vile serikali ya muungano haitakuwa na nguvu zozote zaidi ya kuwasikiliza washirika wa muungano huo.
Tuseme ukweli kwamba Wazanzibari hawautaki kabisa muungano, bali wanalazimishwa. Kitendo cha wanaosaidikiwa Waislamu kuchoma makanisa mjini Unguja kinadhihirisha kwamba upande huo wa Jamhuri ya Tanzania hauutaki kabisa Muungano, ingawa visingizio vyao ni kwamba, hauwasaidii chochote.
Wazanzibari wanasema Muungano hauwasaidii, lakini kule hakuna mashamba makubwa ya mchele, mahindi wala viazi, achilia mbali umeme wa uhakika ambao wanautoa Tanzania Bara wanakodai kwamba kunawakandamiza na kuwanyima uhuru wao.
Lakini Watanganyika wanaung’ang’ania Muungano huo ambao kwa kiasi kikubwa hauna msaada kwao, pengine kama kuna sababu za kiusalama, kwa sababu hakuna chochote ambacho Tanzania Bara inakipata kutoka huko.
Wazanzibari wameonyesha dhahiri kwamba wao ni ‘wachoyo’ hasa baada ya kuwepo kwa tetesi kwamba kuna mafuta huko, wakaona hawawezi kuwagawia na wenzao wa Bara huku wakisahau kwamba kwa miaka 50 ya Muungano tangu uliposainiwa, wamekuwa wakinufaika nao.
Lakini kwa upande mwingine, najiuliza bila kupata majibu, kwamba Watanzania wanawashangaa vipi Wazanzibari wanaposema hawautaki Muungano? Au inakuwaje Wazanzibari waanze kuchoma makanisa sasa wakidai hawautaki Muungano?
Wazanzibari wanasema kwa kipindi chote hicho wameshindwa kufanya jambo lolote kwa maendeleo yao kutokana na kivuli cha Muungano na kila wanalotaka kulifanya lazima wahojiwe.
Watanganyika nao wanasema rasilmali nyingi za Bara zimekuwa zikiwanufaisha bure Wazanzibari katika kile kinachoonekana kama kujipendekeza kwa Serikali ya CCM kulinda kwa nguvu ili Muungano usivunjike.
Kilicho dhahiri ni kwamba, Wazanzibari wanawakumbusha tu Watanzania kwamba wao walikwishauvunja kitambo Muungano ambao muasisi wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliupigania kwa juhudi hadi mauti yalipomfika.
Kimantiki, Wazanzibari waliuvunja Muungano huu mwaka 1992, wakati walipoamua kujiunga na Shirikisho la Nchi za Kiislamu Duniani (Organization of Islamic Countries - OIC). Hapa ndipo hasa 'Chunusi' wa Muungano alipoingia.

SUALA LA UTAIFA:
Tangu mwaka 1992 katika jaribio la Dk. Salmin Amour Juma kuiongoza Zanzibar kujiunga na OIC, ilionekana dhahiri lengo la SMZ lilikuwa kuifanya Zanzibar Taifa la Kiislam wakati alifahamu suala kama hilo lilipaswa kuingizwa kwenye Muungano na kujadiliwa kabla ya kuchukua uamuzi mzito kama huo.
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, hasa kutoka Tanzania Bara, waliona wamesalitiwa na kiongozi huyo wa Zanzibar ambaye pia kikatiba, ndiye Makamu Mwenyekiti wa chama kwa upande wa Visiwani na alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Lakini uamuzi huo ukawa umewasha moto kwa Wabunge wa CCM kutoka Bara, ambao waliona kuwepo kwa serikali mbili ndani ya Muungano kulikuwa kunawapa kiburi Wazanzibari kiasi cha kufanya lolote wanalotaka bila kusubiri baraka za upande mwingine.
Haikushangaza wakati wa Kikao cha Bunge la Bajeti la mwaka 1993, aliyekuwa Mbunge wa Chunya, Njelu Kasaka, alipowasilisha hoja binafsi kudai Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano ili kutoa uwiano sawa.
Tuliokuwepo wakati huo tuliuona mjadala huo pale Karimjee jinsi ulivyopamba moto na kushuhudia Wabunge 55 wa Bara (maarufu kama G55) wakiunga mkono kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Wabunge hao na Watanzania wa Bara walikuwa na haki ya kulizungumza hilo, ingawa muasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere, aliingilia kati na kuwaita Waziri Mkuu wa wakati huo, John Malecela, na Katibu Mkuu wa CCM wa wakati huo, Horace Kolimba, kwamba ni wahuni na walevi. Hakuishia hapo, ndipo akaamua kutunga kitabu cha ‘Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania’.
Leo hii nitashangaa ikiwa wale waliokuwa wanaiunga mkono hoja ya Tanganyika ndani ya Muungano kama wataikana, ingawa mtoa hoja, Njelu Kasaka, hataki kabisa kuulizwa swali lolote kuhusiana na Serikali ya Tanganyika.
Ninawakumbuka wabunge wote waliounga mkono hoja hiyo, akina Jenerali Twaha Ulimwengu, Mateo Qaresi, Edward Oyombe Ayila, Shashu Lugeye, Dk. Mganga Kipuyo, John Mwanga, Dk. Deogratius Mwita, Abel Mwanga, Patrick Qorro, Dk. Ndembwela Ngunangwa, Richard Koillah, Paschal Mabiti, Luteni Lepilal Ole Molloimet, Lumuli  Alipipi Kasyupa, Profesa Aaron Massawe, Arcado Ntagazwa.
Walikuwemo pia, Phineas Nnko, Paschal Degera, Mussa Nkhangaa, Halimenshi Mayonga, Said Abdallah Nakuwa, Mosi Tambwe, Luteni Kanali John Mhina, Charles Kagonji, Kisyeri Werema Chambiri, Tobi Tajiri Mweri, Aidan Livigha, Philip Marmo, Erasto Lossioki, Shamin Khan, Raphael Shempemba, Mussa Massomo, Jared Ghachocha na Mariam Kamm.

MAMBO WALIYOYATAKA:
Kinachojadiliwa sasa kwa kiasi kikubwa kilikwishaelezwa huko nyuma, kwa sababu mambo ambayo akina Njelu Kasaka waliyataka ni mabadiliko katika Katiba ya Muungano, ambao walisema ulizaliwa bila kupata baraka za wananchi na hivyo kuwa na upungufu.
Wakaeleza kwamba, kwa wakati huo ilikuwa lazima muungano huo ufanywe haraka haraka ili kulinda mapinduzi ya kumwaga damu ya ndugu zetu wa Visiwani; Unguja na Pemba, kwamba Sultani Jamshid angeweza kurejea tena kwa msaada wa kutoka kokote kule duniani. Kwa hiyo, nchi hizo ziliungana tu kwa sababu za kiulinzi na kiusalama zaidi.
Kwa upande mwingine, mambo yanayoelezwa na Wazanzibari wa leo wanaochoma makanisa yaliwahi kuelezwa na Aboud Jumbe Mwinyi na ndiyo yaliyomgharimu mwaka 1984 wakati alipovuliwa madaraka yote ndani ya SMZ, Muungano na CCM.
Wazanzibari hawako tayari hata kusikia kunakuwepo na muundo wa Serikali Moja. Watanganyika wanaendelea kujipendekeza tu huku wakiwa wamepoteza utaifa wao wakati ndani ya Katiba hiyo Zanzibar inatajwa na ina serikali yake.
Wazanzibari wanadai eti wakati Muungano unafanyika wao walikuwa na serikali yao kamili! Huu ni upuuzi kwa sababu hata Tanganyika ilikuwa na serikali yake na ndiyo iliyotangulia kujikomboa. Vinginevyo, muungano huo ungetokea vipi kama Zanzibar haikuwa taifa kamili?
Pengine tufike mahali tuwaache Wazanzibari waendelee na mambo yao, kwa sababu walikwishauvunja Muungano miaka mingi iliyopita.
Sisi tuijadili na kuirekebisha Katiba yetu, itufae maishani, hao wamekwishatuulia mwana mwingine wa Mwalimu Nyerere kama walivyomuua ‘Azimio la Arusha’ huko huko Zanzibar mwaka 1992.


1 comment:

  1. If Zanzibar don't like unitary state then they should park and go! 43milion Tanzanians can do without 1.5 million Isle!

    ReplyDelete