Pages

Pages

Pages

Thursday 24 July 2014

TANZANIA YAONGEZA UWEZO WA KUKOPESHEKA

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Website :www.ikulu.go.tz              
Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,      
STATE HOUSE,              
1 BARACK OBAMA ROAD,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania imepandishwa hadhi katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na sasa inaweza kupata mikopo mikubwa zaidi na yenye hadhi kubwa zaidi kuliko huko nyuma. Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo katika Tanzania, Bi. Tonia Kandiero ametangaza hayo, Julai 23, 2014.Bi.
Kandiero amesema kuwa miaka yote tokea Tanzania kuwa mwanachama wa AfDB, imekuwa inapata mikopo ya hadhi ya chini zaidi na midogo zaidi ya maendeleo kutokana na uwezo na nguvu za uchumi wake.Amesema kuwa hadhi ya Tanzania ndani ya Benki hiyo imepanda kutokana na kukua kwa uchumi wa Tanzania, kuongezeka kwa uwezo wa kukopesheka na uwezo wa kulipa na kutimiza masharti yanayokwenda na mabadiliko hayo ya hadhi.
Bi. Kandiero ametangaza mabadiliko hayo katika hadhi ya Tanzania ndani ya Benki hiyo wakati alipozungumza katika sherehe kubwa ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Mangaka-Mtambaswala kwa kiwango cha lami na kufungua Barabara ya Masasi-Mangaka ambayo imekamilika kwa kiwango cha lami. Barabara  zote ziko katika mkoa wa Mtwara na mgeni rasmi katika sherehe hiyo kubwa iliyofanyika mjini Mangaka, mji mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, MheshimiwaJakaya Mrisho Kikwete, ambaye ameingia Mkoani Mtwara jana  kwa ziara ya siku mbili.
Ameingia Mtwara akitokea Ruvuma ambako alifanya ziara ya siku sita.Bi. Kandiero amemwambia Rais Kikwete na mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe hiyo kuwa kabla ya kupandishwa hadhi, Tanzania ilikuwa na sifa za kukopa ndani ya benki hiyo mikopo kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo na siyo mikopo mikubwa ya maendeleo.
Bi. Kandiero amesema kuwa tokea Tanzania kujiunga na AfDB imepata kiasi cha mikopo ya thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni moja.
AfDB ni moja ya wafadhili wa barabara hizo mbili ambazo sherehe zake za uzinduzi na jiwe la msingi zimefanyika jana kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Serikali ya Tanzania. 

AfDB na JICA zinashirikiana na Serikali ya Tanzania kugharimia ujenzi wa barabara hizo chini ya Mradi wa kuendeleza Barabara nchini. Chini ya ushirikiano huo, AfDB inatoa asilimia 64.79 kugarimia ujenzi wa barabara hizo,  JICA inatoa asilimia 31.83 na Serikali ya Tanzania inatoa asilimia 2.39.Barabaraba ya Mangaka-Mtambaswala, mpakani mwa Tanzania na Mozambique, ina urefu wa kilomita 65.5, inajengwa na kampuni ya Jamhuri ya Watu wa China kwa gharama ya shilingi bilioni 59.66 na ujenzi utakuchukua miezi 28.
Nayo Barabara ya Mangaka-Masasi yenye urefu wa kilomita 55.1 ilikamilika mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kuwekewa jiwe la msingi la ujenzi wake na Rais Kikwete Agosti 21, 2009. Barabara hiyo, ilijengwa na kampuni kutoka Japan kwa awamu tatu na kwa gharama ya shilingi  bilioni 54.8.  Barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Masasi-Mangaka-Tunduru.

No comments:

Post a Comment