Pages

Pages

Pages

Friday 18 July 2014

RIWAYA TAMU: JUDITH…JUDITH…! - 21


INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)

0755 040 520 / 0653 593 546 

ILIPOISHIA:
Makella amefumaniwa laivu na Ramadhani akiwa amemkumbatia Jamilla. Ramadhani anamlenga kwa bastola akiwa na dhamira moja tu ya kuua, maneno yanamkauka Makella ambaye ghafla anahisi kitu kikipenya mwilini na hatimaye kupitiwa na usingizi mzito usio na kikomo. Judith naye anapagawa na sura Edson na kujikuta akitamka haraka kwamba hajaolewa. Hatmaye anatoroka kwenye gesti aliyofikia na kuhamia pengine ili awe na fursa ya kukutana na Edson. Mapenzi yao yanazaa uchumba na hatimaye ndoa. Lakini siku moja akipita madukani Judith anayavutia macho ya kijana mmoja mhudumu. Je, ni nani na anataka nini? Endelea na sehemu hii ya mwisho ya hadithi yetu …

Yule mhudumu alimtazama kidogo Judith kisha akageukia kwenye rundo la nguo zilizotundikwa mbele ya wateja. Akaisogelea blauzi moja na kuigusa huku akimuuliza, “Hii hapa?”
“Hiyohiyo. Ni bei gani?”
Mhudumu hakujibu, aliitoa blauzi hiyo na kumletea Judith huku akisema, “Itazame kwanza, dada.”
Ni wakati mhudumu huyo akimpatia blauzi hiyo ndipo macho yao yalipogongana. Mhudumu yule alishtuka kidogo na kumkodolea macho zaidi Judith. Judith naye akamtazama kwa mshangao huku akiipokea blauzi.
“Ni bei gani?” Judith aliuliza tena.
“Shilingi elfu kumi tu.”
Judith alilipa na kuamua kuondoka. Tazama ya mhudumu huyo ilimshangaza, na zaidi, ilimkera. Akaamua kwenda duka jingine. Ilikuwa ni wakati amevuka maduka mengine mawili tu mara akasikia akiguswa bega. Akageuka na kukutana na yule mhudumu wa duka la kwanza.
“Samahani dada, sijui kama nimekufananisha au sijakufananisha,” kijana yule alisema kwa sauti ya upole. Kisha akaongeza, “Naomba kukuuliza.”
Judith alisimama na kumtazama kwa makini kijana huyo ambaye macho yake yalionyesha ujasiri uliofichika moyoni. “Unasemaje?” hatimaye alimuuliza.
“Naitwa Rwagasore. Je, wewe ni Judith  mtoto wa marehemu mzee Ndayishimiye?”
Moyo wa Judith ulipiga paa! Katika nchi hii ya Tanzania, yeye akiwa ni mgeni, hakutarajia kuwa kuna mtu ambaye angeweza kumfahamu. Akashusha pumzi ndefu na kumkodolea macho zaidi kijana huyo. Kisha, badala ya kujibu, naye akauliza, “ Kwani vipi?”
“Sina nia mbaya, dadangu. Nauliza tu.”
“Na kama ndiye au siye wewe unataka nini?”
“Basi, dada kama nimekuudhi niwie radhi,” Rwagasore alisema huku akionyesha kuanza kuondoka.
“Subiri,” Judith alimzuia kwa kumshika mkono.
Rwagasore akatii.
“Mimi ndiye Judith, mtoto wa marehemu mzee Ndayishimiye, enhe, unasemaje?” Judith aliamua kutoboa ukweli huo akiwa ameamua kuwa liwalo na liwe.
“Ni kweli dada?” kijana yule alionekana kutomwamini Judith.
“Ni kweli! Enhe, kwani vipi? Unasemaje?”
“Pole sana, dada,” Rwagasore alisema kwa unyonge huku akimtazama kutoka juu hadi chini. “Pole kwa matatizo yaliyokukuta. Mimi nilikuwa mtoto wa mzee Nsanze, nyumba ya tatu toka kwenu. Hata mimi wazazi wangu waliuawa. Mimi nilijificha kwenye migomba nje ya nyumba, ndiyo maana nilinusurika. Lakini nilisikia kuwa wewe ulitekwa na Makella. Habari hizo zilienea sana baada ya vurugu ile. Tukasikia kuwa Makella alipania kukuoa kwa nguvu. Baadaye tukasikia kuwa ulimtoroka. Ni kweli dada?”
Judith hakujibu, akaendelea kumtazama Rwagasore kwa namna ya kumpa nafasi ya kuendelea kuongea.
“Tukasikia kuwa Makella alikuwa akikusaka, na alidai kuwa akikupata lazima akuue, eti ulimwibia pesa zake!” Rwagasore aliendelea. “Lakini Mungu mkubwa, dada Judith. Siku chache tu baada ya wewe kupotea, Makella alifumwa kwa mke wa askari mwenzake. Akauawa kwa kupigwa risasi kifuani!”
“Nini? Makella kauawa?!” Judith alibwata huku macho kayatoa pima.
“Ndiyo dada! Alikufa kifo kibaya sana! Baada ya kupigwa risasi, yule askari mwenye mke alimkata sehemu za siri na kumchinja shingo, kichwa kule kiwiliwili kule! Akamtumbua tumbo lote, maini, utumbo na kila kitu nje! Nakwambia, Makella alibaki ni maiti isiyotazamwa mara mbili!”
Judith alitwaa leso ndani ya mkoba na kufuta jasho usoni. Kisha akainua mikono juu na kusema, “Ee, Mungu, ushukuriwe. Nikulipe nini Mungu wangu?”
Mara akahisi machozi yakimlengalenga. Hakujua kama yalikuwa machozi ya furaha au majonzi. Taarifa hii njema ya kifo cha Makella ilizirejesha kumbukumbu kichwani mwake, kumbukumbu ya siku baba, mama na wadogo zake watatu walipouawa mbele yake na kundi la watu watatu wenye silaha, Makella akiwa miongoni mwao.
Kwa kutumia leso ileile aliyafuta machozi hayo kisha akamshika mkono Rwagasore na kusema, “Asante kaka’ngu kwa taarifa hiyo.”
Akafungua pochi na kuchomoa noti moja ya shilingi 10,000. Akampatia.
Kisha akaondoka huku akimtupia tabasamu hafifu, moyoni akijisikia kujawa na faraja ya aina yake. kwa sauti ya chini sana ambayo haikuweza kuyafikia masikio ya mtu mwingine, alitamka, “Mungu uhimidiwe! Jina lako litukuzwe!”

TAMATI

Kwa maoni na ushauri wasiliana na mtunzi kwa simu na. 0653 593 546, 0755 040 520 au baruapepe: lubulilubuli@yahoo.co.uk 


ZILIZOPITA:

No comments:

Post a Comment