Pages

Pages

Pages

Wednesday 2 July 2014

COSTA RICA ITALIWEZA SEBENE LA ‘TOTAL FOOTBALL’ YA UHOLANZI?

 

Na Daniel Mbega

TULISHUHUDIA fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 kule Afrika Kusini namna Uholanzi ilivyotandaza kandanda safi hadi fainali, kabla ndoto zake za kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza kuzimwa na Hispania kwa bao 1-0.
Muziki ule unaonekana bado unaendelea na kila timu inayokutana na Wadachi hao inatakiwa kuwa ngangari ili iweze kulimudu sebene la total football ambalo linaonyeshwa na kikosi hicho kinachofunzwa na kocha mzalendo Luis Van Gaal.
Timu hiyo imefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali kwa kushinda mechi zake nne zilizopita katika fainali za mwaka huu nchini Brazil, zikiwemo tatu za Kundi B na moja ya raundi ya pili na sasa inataka kuuendeleza katika robo fainali dhidi ya Costa Rica Jumamosi Julai 5.
Katika michezo yake ya Kundi B Uholanzi ndiyo iliyoipa mkosi bingwa mtetezi Hispania kwa kuikung’uta mabao 5-1, Ikainyuka Australia 3-2 kabla ya kuishindilia Chile 2-0, lakini katika raundi ya pili ikaichapa Mexico 2-1 na kusonga mbele.
Kikosi cha Uholanzi, wakali wa total football, mwaka huu kina wachezaji wengi mahiri na wenye vipaji, kama ilivyokuwa mwaka 2010, wengi wakiwa kwenye umri wa kati wa uchezaji.
Wanaounda kikosi hicho miaka na klabu wanazozichezea kwenye mabano ni walinda mlango Jasper Cillessen (25 – Ajax), Michel Vorm (30 – Swansea City, Wales), na Tim Krul (26 – Newcastle United, England); walinzi ni Ron Vlaar (29 – Aston Villa, England), Stefan de Vrij (22 – Feyenoord), Bruno Martins Indi (22 – Feyenoord), Daley Blind (24 – Ajax), Daryl Janmaat (24 – Feyenoord), Paul Verhaegh (30 - FC Augsburg, Ujerumani), Joël Veltman (22 – Ajax), na Terence Kongolo (20 – Feyenoord).
Viungo ni Nigel de Jong (29 – AC Milan, Italia), Jonathan de Guzmán (26 – Swansea City, Wales), Wesley Sneijder (30 – Galatasaray, Uturuki), Jordy Clasie (22 – Feyenoord), Leroy Fer (24 - Norwich City, England), na Georginio Wijnaldum (23 – PSV). Washambuliaji ni nahodha Robin van Persie (30 – Manchester United, England) Arjen Robben (30 – Bayern Munich, Ujerumani), Dirk Kuyt (33 – Fenerbahçe, Uturuki), Jeremain Lens (26 – Dynamo Kyiv, Ukraine), Klaas-Jan Huntelaar (30 – Schalke 04, Ujerumani), na Memphis Depay (20 – PSV).
Costa Rica ambayo ilikuwa Kundi D iliweza kuongoza kundi hilo kwa kushinda mechi mbili na kutoka sare moja. Kwanza iliitandika Uruguay 3-1, ikaichapa Italia 1-0 kabla ya kutoka suluhu na England, na katika raundi ya pili iliitoa Ugiriki kwa matuta 5-3 baada ya matokeo ya dakika 120 kuwa bao 1-1.
Timu hiyo kutoka Bara la Amerika ya Kati na Kaskazini (CONMEBOL) inanolewa na Jorge Luis Pinto, raia wa Colombia ambapo katika kikosi chake hakuna mchezaji anayevuka miaka 35.
Wanaounda kikosi hicho miaka na klabu zao zikiwa kwenye mabano ni makipa: Keylor Navas (27 – Levante, Hispania), Patrick Pemberton (32 – Alajuelense), Daniel Cambronero (26 – Herediano); walinzi ni: Johnny Acosta (30 – Alajuelense), Giancarlo González (26 – Columbus Crew, Marekani), Michael Umaña (31 – Saprissa), Óscar Duarte (25 – Club Brugge, Ubelgiji), David Myrie (26 – Herediano), Waylon Francis (23 – Columbus Crew, Marekani), Júnior Díaz (30 – Mainz 05, Ujerumani), Cristian Gamboa (24 – Rosenborg, Norway), na Roy Miller (29 – New York Red Bulls, Marekani).
Viungo ni; Celso Borges (26 – AIK, Sweden), Christian Bolaños (30 – Copenhagen, Denmark), Michael Barrantes (30 – Aalesund, Norway), Esteban Granados (28 – Herediano), José Miguel Cubero (27 – Herediano), Yeltsin Tejeda (22 – Saprissa), na Diego Calvo (23 – Vålerenga, Norway). Washambuliaji: Randall Brenes (30 – Cartaginés), Marco Ureña (24 – Kuban Krasnodar, Russia), Joel Campbell (21 – Olympiacos, Ugiriki), na nahodha Bryan Ruiz (28 – PSV, Uholanzi).

Rekodi zao
Timu hizi mbili zinakutana kwa mara ya kwanza katika historia ya soka duniani, na historia inaweza ikawa tofauti na mambo ya uwanjani kulingana na hali halisi ya timu husika.
Kati ya mechi 748 za kimataifa ambazo Uholanzi imecheza tangu Aprili 30, 1905, haijawahi kucheza na timu hii ingawa imecheza mara 13 na timu za shirikisho la soka la CONMEBOL na kushinda mechi 10, kutoka sare mara moja na kufungwa mbili, ikifunga mabao 32 na kufungwa 11.
Uholanzi imecheza mara sita na Mexico, ikishinda mara nne na kufungwa mbili, imecheza na Marekani mara nne na kushinda zote, imecheza na Dutch Antilles mara mbili, ikashinda mara moja na kutoka sare mara moja, na imecheza na Canada mara moja na kushinda.
Kwa upande mwingine Costa Rica nayo ingawa haijacheza na Uholanzi, lakini imecheza mara 30 na timu za Ulaya (UEFA) ambapo kati ya mechi hizo imeshinda 7, sare tano na kufungwa 18, huku ikipachika mabao 20 na kufungwa 38.
Costa Rica imecheza na Italia mara tatu na kushinda mbili ikipoteza moja; imecheza na Poland mara tatu na kufungwa zote; imecheza na Slovakia mara mbili ikatoka sare na kushinda moja; imecheza na Finland mara mbili ikishinda moja na kufungwa moja; imecheza mara mbili na Sweden ikashinda mmoja na kupoteza mmoja; ikacheza mara mbili na Austria na kufungwa mmoja na kutoka sare; na pia imecheza mara mbili na Norway ikitoka suluhu mmoja na kupoteza mwingine. Michezo mingine iliyoshinda ni dhidi ya Scotland na Ugiriki.
Timu hiyo imefungwa na Urusi, Czechoslovakia, Wales, Ubelgiji, Ufaransa, Ukraine, Jamhuri ya Czech, Ujerumani, Uswisi na Yugoslavia. Ilitoka sare na England pia mwaka huu katika mashindano ya Kombe la Dunia.



No comments:

Post a Comment