Jacqueline Mkindi, Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA
Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha
WAJASIRIAMALI zaidi ya 250 kutoka Kanda ya Kaskazini wanakutana jijini Arusha kwenye maonyesho ya kuwaelimisha kuhusu bidhaa zinazopatikana nchini.
Maonyesho hayo yameandaliwa na Shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO) na Asasi kilele ya Sekta binafsi yenye lengo la kuhamasisha maendeleo ya kilimo cha mazao ya Horticulture nchini (TAHA).
Akizungumzia kufanyika kwa maonyesho hayo Meneja SIDO Mkoa wa Arusha Isidori Kiyenze alisema, yatawashirikisha wajasiriamali wadogo na wakati kutoka Mkoa wa Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Kiyenze alisema, mbali na wajasiriamali hao wamewaalika pia wajasiriamali wengine kutoka sehemu mbalimbali nchini ili wafike na kuonyesha bidhaa zinazotengenezwa nchini.
“Lengo kubwa la maonyesho haya ni kuelimisha wananchi kuwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ni bora zaidi kuliko zinazotoka nje ya nchi,” alisema Kiyenze na kuongeza:
“Lakini pia tunalenga kuimarisha soko la ndani la bidhaa hizi zinazozalishwa nchini kwasababu lengo si kuzalisha tu bali kuuza bidhaa zinazozalishwa,” alisema.
Alisema maonyesho hayo yanawalenga wajasiriamali wenye bidhaa za uhandisi, usindikaji wa vyakula, bidhaa za ngozi na mazao yake, uzalishaji sabuni na bidhaa mbalimbali .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA Jacqueline Mkindi alisema, wamewalenga wadau wao hasa wakulima wazalishaji, wasindikaji wa mazao ya Holticultural na watoa huduma.
Alisema katika eneo la usindikaji washirika wao wakubwa ni SIDO kwani wameendeleza ushirikiano huo hasa katika masuala ya kuwajengea uwezo wadau katika sekta yao.
“Lengo letu la kuwaleta hapa wajasiriamali katika sekta yetu ya Horticultural ni kuwajegea uwezo kwa masuala ya usindikaji ili waweze kuzalishaji na kuwa na bidhaa zinye viwango,” alisema Mkindi na kuongeza:
“Kubwa pia ni kuwaleta pamoja ili waone wenzao wanafanya nini katika sekta hiyo pia kupata fursa ya kuelezana changamoto zao kwao na Serikali ili washiriki katika kuzitatua,” alisema.
Mbali na maonyesho hayo pia waandaji hao wameandaa mafunzo yatakayotolewa bure yatakayohusu masuala ya masoko na jinsi ya kujipanga kuingia kwenye ushindani na mafunzo kuhusu suala la viwango.

No comments:
Post a Comment