Naibu Katibu Mkuu toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma HAB Mkwizu (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma yanayotarajiwa kuanza Juni 16, katikati ni Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Bi. Roxana Kijazi toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma na mwisho kulia ni Mkrugenzi Msaidizi Idara ya Uchumi na Ushauri Kazi Bw. Hassan Kitenge.
Naibu Katibu Mkuu toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma HAB Mkwizu (kulia) akisistiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema hii leo jijini Dar es Salaam juu ya maadhimisho ya siku ya utumishi wa umma yanayotarajia kuanza tarehe16 Juni, kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Habari assah Mwambene.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Naibu Katibu Mkuu toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.HAB Mkwizu (hayupo pichani) wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma yanayotarajiwa kuanza Juni 16 jijini Dar es Salaam. Picha zote na Eliphace Marwa – MAELEZO
……………………………………….
Na Eliphace Marwa -MAELEZO
Zaidi ya Taasisi 30 za Serikali hapa nchini zinatarajia kushiriki katika maonesho ya wiki moja ya utumishi wa Umma yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. HAB Mkwizu wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kukamilika kwa maandalizi hayo.
Mkwizu alisema maadhimisho hayo ambayo huratibiwa na ofisi yake yatafunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Hawa Ghasia na kuambatana na uoneshaji wa kazi mbalimbali za Taasisi za Serikali wanazozifanya kila mwaka kwa lengo la kutathmini kazi zinazofanywa na sekta hiyo katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Kuadhimisha siku hii kutakuwa na kongamano la siku mbili litakalojadili miaka hamsini ya Muungano katika Utumishi wa Umma ambalo litafanyika kuanzia tarehe 19 hadi 20 Juni katika Kituo cha Mikutano cha kimataifa cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na kusimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue”, alisema Bw. Mkwizu
Aidha Bw. Mkwizu pia alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mnazi mmoja ili kupata huduma na kutoa maoni juu ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi za Serikali.
Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni ‶Mkataba wa Msingi na Kanuni za Utumishi wa Umma Barani Afrika ni Chachu ya kuimarisha utawala bora na Uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa Uwazi″
Kilele cha Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka tarehe 23 Juni kama ilivyokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) mwaka 1994 katika mkutano wa Mawaziri wa Utumishi wa Umma barani Afrika uliofanyika nchini Morroco.
CHANZO FULL
SHANGWE

No comments:
Post a Comment