INNOCENT A.
NDAYANSE (ZAGALLO)
0755 040 520 /
0653 593 546
Simulizi
zimemnogea Makella na sasa anaamua kunywa pombe. Anamlazimisha Judith naye
anywe. Kwa woga na hofu, anaamua kunywa pombe kwa mara ya kwanza maishani
mwake. Makella anasimulia mengi na kuwaponda wanawake wa Tanzania. Anajiuona
yuko huru zaidi. Hatimaye anaamua kwenda kuoga. Je, nini kitaendelea hali
Judith naye akiendelea kunywa pombe? Ungana na msimulizi wako…
NJE
ya Kiyovu Hotel, Judith alitembea kwa mwendo uleule wa kawaida huku kwa macho
ya wizi akiwatazama askari watatu wenye silaha waliokuwa wakiilinda hoteli
hiyo. Askari hao hawakumjali wala kumshuku, zaidi walimtazama kwa namna nyingine
kabisa, umbo lake lililotengeneza robota kubwa chini ya nyonga yake likiwa ni
kivutio kikubwa machoni mwa askari hao kiasi cha kujikuta wakitikisa vichwa kwa
matamanio na kutabasamu kisirisiri.
Judith
aliwaona jinsi walivyomtazama. Akaijua sababu ya kufanya hivyo. Hakushangazwa
na macho hayo, wanaume wengi walishamkodolea macho hususan kwenye makalio yake
makubwa pale inapotokea akavaa nguo yoyote iliyomshika vilivyo maungoni. Hawa
askari walikuwa kama hao wanaume wengine wengi waliokwishapita, hivyo hakuwajali.
Akaendelea kutembea taratibu vilevile, kama mtu anayejiamini ilhali ni Mungu tu
aliyejua hali aliyokuwa nayo moyoni mwake.
Muda
mfupi baadaye alikuwa kando ya Barabara ya 17/18. Barabara hiyo ilikuwa
maarufu, yenye kutumiwa na magari mengi, makubwa kwa madogo, kuingia na kutoka
nchini Rwanda. Kwa dakika chache tu, kama mbili alizosimama kando ya barabara
hiyo tayari magari mawili makubwa ya mizigo, yenye nambari za usajili za
Tanzania yalipita.
Akilini
mwake, Judith aliamini kuwa, kwa kutumia magari hayo ya mizigo atafanikiwa
kufika mbali na mkono wa Makella. Hivyo, aliamua kuhakikisha anafikia
makubaliano na mmoja wa madereva wa magari hayo.
Lakini kuna wepesi gani katika
kulifanikisha suala hilo? alijiuliza. Hakuwa zaidi ya hatua mia mbili kutoka
Kiyovu Hotel ambako ametoroka huku kaiba fedha kutoka katika mifuko ya suruali
ya ‘mpenzi’ wake aliyemleta humo.
Hakupenda
kujipa matumaini kuwa Makella atatulia tu pindi atakapogundua kuwa dola zake 2,000
za Marekani zimeibwa. Hatatulia! Judith alilitambua fika hilo jambo.
Atakachofanya Makella ni kulivalia njuga suala hilo. Atawakimbilia wahudumu wa
hoteli ambao nao wataharakisha kuwasiliana na walinzi. Walinzi nao katika
kutaka kuhakikisha kuwa siyo wafanyakazi ‘wachovu’, watahaha huku na kule, nje
na ndani ya hoteli wakimsaka mithili ya msako wa gaidi au haini!
Usingepita
muda mrefu kabla hawajamkuta pale kando
ya barabara na kumsulubu kwa jinsi watakavyo kabla ya hatua yoyote nyingine
kuchukuliwa na labda hatua hiyo ikiwa ni kumchinja kama kuku!
Hakuwa
tayari kutiwa mbaroni na watu hao na kwa kuwa alijua kuwa ana pesa, hakutaka
kusababisha uzembe utakaowafaidisha hao watakaomsaka. Alijua kuwa mbele ya pesa
lolote linawezekana hata kama ni gumu kiasi gani.
Mbele
kidogo, kiasi cha hatua hamsini hivi,
kulikuwa na duka kubwa lililosheheni bidhaa mbalimbali. Lilikuwa wazi, wateja
wakiingia na kutoka. Kando ya duka hilo kulikuwa na teksi kadhaa zilizokuwa
zikiwasubiri wateja. Judith aliichangamsha akili yake katika kufanya kila jambo
kwa haraka na kwa umakini, hivyo aliifuata teksi moja na kuingia haraka.
**********
AWALI
ilimwia vigumu Makella kuamini kuwa Judith hayumo chumbani. Kwa sekunde kadhaa
aliduwaa katika mlango wa bafu akikodoa macho chumbani. Kaenda wapi? Swali hilo lilirandaranda akilini mwake kwa mshangao.
Taratibu
akatoka bafuni humo na kuufunga mlango taratibu vilevile. Akahisi kengele ya
hadhari ikilia kichwani mwake. Nywele zikamsimama, na mara hima akaufuata
mlango mkubwa wa kutokea chumbani humo. Akajaribu kuufungua.
Haukufunguka!
“Umefungwa!”
akaropoka kwa sauti iliyojaa fadhaa na kugeuka huku na kule kama atazamiaye
kuupata ufumbuzi wa tatizo lililojitokeza. Akashusha pumzi ndefu, macho kayatoa
pima!
Akageuka
na kurudi haraka kwenye nguo zake. Akainyanyua suruali iliyokuwa sofani
ili aivae. Lakini jambo jingine
likamshtua; kitambulisho cha uraia kilikuwa sofani huku mifuko ya nyuma
ikiwa ikining’inia nje.
Hakuhitaji
kukisumbua kichwa kufikiria ni kipi kilichomsibu. Ameibiwa! Ndiyo, ameibiwa!
Hilo halikuwa jambo la siri tena. Mmoja wa mifuko ya suruali ulikuwa umehifadhi
pesa nyingi, dola 2,000 za Marekani, pesa alizozipata mchana katika harakati
zake za uwajibikaji dhidi ya Watutsi.
Sasa
hazimo!
“Mungu
wangu!” aliropoka tena. Mara akakurupuka kuitwaa bunduki na kuishika mikononi
mithili ya mtu aliye tayari kuitumia dakika hiyohiyo! Kwa takriban dakika nzima
akabaki kaduwaa, akili imedumaa!
Mara
kama aliyezinduliwa, akaitupa bunduki hiyo pale kitandani. Akili mpya ikamjia.
Akaifuata simu na kubonyeza tarakimu kadhaa, akilenga mapokezi.
“Tukusaidie?”
sauti ya kike ilipenya masikioni mwake baada ya muda mfupi.
“Njooni
mnifungulie!” Makella alibwata simuni. “Njooni haraka nimefungiwa mlango kwa
nje!”
Ulikuwa
ni ujumbe uliomshtua na kumshangaza mhudumu wa mapokezi. “Chumba namba ngapi?”
aliuliza.
“Kumi
na moja!”
Papohapo
mhudumu akautwaa ufunguo wa akiba wa chumba namba 11 na kutoka hima. Akaiona
lifti ya kupandia huko ghorofani ni kama vile itamchelewesha. Akazikwea ngazi
mbili, mbili hadi huko katika ghorofa ya kwanza. Punde akawa ameshaufungua
mlango wa chumba namba 11. Akakutana uso kwa uso na Makella.
“Umemwona
yule malaya?” lilikuwa ni swali lililomtoka Makella kwa jazba, akimtazama
mhudumu huyo kama aliyehusika na kufungiwa kwake.
“Malaya!
Malaya gani?”
“Yule
niliyekuja naye!”
Mhudumu
akatokwa macho pima. Kisha akauliza, “Kwani imekuwaje?”
Makella
akazidi kughadhibika. Akamkwida mhudumu huyo. “Umeshirikiana naye, siyo?”
alimuuliza huku akiendelea kumkwida.
“Kwani
vipi…?”
Kofi
kali lililotua katika shavu lake la kulia lilimkata kauli.
“Sema!
yule malaya yuko wapi?”
“Ametoka!”
binti yule alijibu.
Kofi
la pili!
“Jamani
utaniua bure!” mhudumu huyo alilalamika kwa sauti iliyoashiria kilio.
“Nitakuua
kweli!” Makella aliwaka. “Sema yuko wapi…sema…sema au nakuua!”
“Subiri
nikwambie!” mhudumu alisihi.
Itaendelea kesho...
No comments:
Post a Comment