Ndugu zangu,
Leo hii sina kingine
cha kusema zaidi ya kwanza kumpa pole za dhati Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Zuberi Kabwe, kwa kuondokewa na mzazi wake mpendwa Mama Shida binti Salum.
Ni msiba mzito kwa
Zitto na wanafamilia. Majonzi yetu sisi katu hayataweza kuyafikia yale ya
walengwa.
Zitto yuko katika
kipindi kigumu, pengine kuliko vyote katika maisha yake, kwa sababu haombolezi
msiba wa mama peke yake, bali anayo mengi na ni fundo kubwa moyoni mwake ambalo
wa kulifungua ni Mungu pekee.
Mama Shida binti Salum
hakuwa mzazi tu, bali alikuwa rafiki kwa Zitto na mshauri wake katika masuala
mbalimbali ya maisha, yakiwemo ya siasa.
Tukumbuke kwamba,
hakuwa tu mwanachama na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, bali pia alikuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata), hivyo alikuwa mtetezi
mkubwa wa walemavu wote nchini.
Mama huyu atakumbukwa
kwa jinsi alivyokuwa akimpa moyo Zitto tangu mwaka 2009 wakati Zitto
alipotangaza nia yake ya kugombea uenyekiti wa Chadema, uamuzi ambao ulimfanya
akatukanwa na wanachama wengi wa chama hicho waliokuwa wakimuunga mkono
mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe.
Ingawa alishauriwa na
watu wengi wenye busara, lakini pengine ushauri wa mama yake aliuzingatia zaidi
na akaamua kujitoa katika kinyang’anyiro kile.
Akahusishwa na kashfa
mbalimbali za kukihujumu chama, kubwa zaidi ni ile kashfa ya mwaka 2013
iliyosababisha Chadema imsimamishe uanachama na kumvua nafasi zote za uongozi
hadi Bungeni.
Kile kilikuwa kipindi
kigumu sana kwa mwanasiasa kijana kama Zitto ambaye bado hajafikisha hata miaka
40. Lakini kwa hekima ya mama yake, mwanasiasa huyu ameendelea kupambana na
kusimama imara kwa kipindi chote hicho.
Maumivu makali zaidi
aliyoyapata Zitto ni katika kipindi anamuuguza mama yake, ambapo siku chache tu
kabla ya mauti kumfika mzazi wake huyo, yeye alizushiwa kashfa Bungeni, tena
kupitia kwenye Hotuba Kivuli ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Vijana,
iliyosomwa na waziri kivuli Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwamba alitafuna mamilioni ya
fedha kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Shirika la Hifadhi
za Taifa (Tanapa) kupitia LekaDutigite na Gombe Advisors.
Nakumbuka
Zitto mwenyewe aliamua kujibu tuhuma hizo kwa majonzi makubwa na uchungu mwingi
akasema, namkunukuu: “Nasikitika kwamba katika hali niliyonayo ya kumwuguza
mama yangu naingizwa kwenye siasa za majitaka. Kampuni ya LekaDutigite
inamilikiwa na wasanii. Gombe Advisors ni kampuni isiyofanya faida (Company
limited by guarantee) na haina maslahi yeyote ya kibiashara.
Wasanii wa Kigoma wamefanya
kazi na TANAPA na NSSF, kazi ambazo zinajulikana na zipo. Leo mpigie simu
mfanyakazi yeyote wa NSSF utasikia kazi ya wasanii hao.Kwa namna yeyote ile hii
ni ishara ya kukosa ubinaadam maana waliyoyasema wanajua sina faida yeyote ya
kifedha, leo wala kesho kwa LekaDutigite na Gombe Advisors.
Kipindi ambacho mama yangu
yupo mahututi, tena mjumbe wa kamati kuu ya chama chao, pole ninayopewa ndiyo
hiyo. Hakuna namna ya kukosa ubinaadamu zaidi ya hivi.
Hata hivyo, ni vema CAG
afanye ukaguzi haraka sana na Mimi binafsi nitawajibika iwapo itaonekana kwa
namna yeyote ile nina maslahi ya kifedha katika LekaDutigite na gombe
advisors..
Ni ushetani. Ni roho mbaya.
There are limits to political attacks.” Mwisho wa kunukuu.
Haya
yalikuwa maneno mazito mno ya Zitto, na kwa hakika siku mbili tu baada ya
kuyasema hayo, yaani Juni 2, mama yake akakata roho.
Yapo
mengi yaliyosemwa kuhusiana na msiba huo, sikuwepo mimi lakini nawanukuu
wanaosema, kwamba wakati Shida binti Salum akiwa mahututi, hakuna hata kiongozi
yeyote wa Chadema – ngazi ya juu – ambaye alikwenda kumjulia hali. Lakini
tulimuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
‘Mtu wa Watu’, akimtembelea mama huyo Mei 28 pale hospitali ya Ami.
Tumesikia
pia kwamba, hata katika mazishi ya mama huyo, hakuna kiongozi yeyote wa juu wa
Chadema aliyekwenda kushiriki! Pengine mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu
Mkuu Dk. Wilbrod Slaa wanayo maelezo ya kutosha.
Binafsi
hili la viongozi hawa wa juu kutohudhuria msiba wa Shida binti Salum
haliniingii akilini kabisa hasa kwa kuwa alikuwa ni mwanachama wao na mjumbe wa
Kamati Kuu ya chama hicho. Tunafahamu Chadema ina mgogoro na Zitto, lakini
hatujui kama kumbe ilikuwa na mgogoro na mama yake pia ndiyo maana hata kwenye
msiba viongozi hao wakuu hawakwenda.
Najiuliza
tu jambo moja, kwamba mwaka 2012 baada ya mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa
Habari Mkoa wa Iringa (IPC) Daudi Mwangosi, kuuawa kwa bomu pale Nyororo kwenye
mkutano wao, hawa jamaa walikuja mbio na wakataka ‘kuuteka’ msiba huo. Busara
zaidi ilitumika.
Wakatoa
ahadi nyingi za kuwasomesha watoto wa marehemu ambazo sidhani kama
zimetekelezwa, japo kwa uchache wake.
Wakati
wa kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Mwangosi Septemba 2, 2013, Chadema
wakateka suala la kujenga mnara wa kumbukumbu pale Nyororo, licha ya Umoja wa
Klabu za Wanahabari Tanzania (UTPC) kugoma.
Sasa
ilikuwaje wakalivalia njuga suala la Mwangosi ambaye hata katika vikao vya
chama alikuwa haingii lakini wakamtelekeza mtu aliyekuwa akitetea na kuzinadi
sera za chama hicho?!
Walikuwa
na maslahi gani kwa Mwangosi? Au walitaka kutumia kivuli cha kwamba alikuwa
mwandishi wa habari ili waandikwe sana na vyombo vya habari na kupongezwa?
Ndiyo.
Siyo lazima kufanya kazi za misiba kama watu wengine wanavyosema kupitia
mitandao ya kijamii, lakini sidhani kama ni busara kulala kiyoyozi wakati
unaposikia mwanao ameanguka na kuvunjika mkono, achilia mbali kufariki!
Nichukue
fursa hii tena kukupa pole nyingi Zitto Kabwe na kushauri kwamba rehema ya
Mungu iwe juu yake, akupe ujasiri wa kukabiliana na magumu yote katika kipindi
hiki, akujaalie hekima na busara ili uweze kuyakabili hata yale ambayo ulikuwa
huwezi peke yako.
Mungu
ni mwema, na hakika atampumzisha kwa amani Shida Binti Salum. Japo wengine
hatukuhudhuria msiba huo, lakini sote tumeguswa na msiba huo. Amen!
Daniel Mbega
Iringa - Tanzania
0656-331974



No comments:
Post a Comment