INNOCENT A.
NDAYANSE (ZAGALLO)
0755 040 520 /
0653 593 546
Judith
anaulizwa swali gumu na Makella aliyeamuru wazazi na ndugu zake wauawe. Lakini anaona
jibu lolote atakalolitoa ama litaokoa maisha yake au litamfanya Makella amuue
na yeye ingawa anadai anampenda. Je, atafanyaje? Ungana na msimulizi wako…
“Hakuna
tatizo,” ni jibu lililomtoka baada ya kuzitafakari kwa kina kauli za Makella.
Na alijibu hivyo huku akijua kuwa ilimpasa kutumia akili katika kufanya lolote
lile la kumtoa katika mikono ya jahili huyo.
Kwamba
ni kipi atakachokifanya katika kujinusuru, hilo lilikuwa ni suala la
kutekelezwa kwa umakini wa hali ya juu. Hakupaswa kuwa na papara, hakutaka
kumfanya Makella agundue mapema kuwa kuna jambo tofauti na matarajio yake.
Lilikuwa
ni jibu lililomfariji na kumsisimua Makella kwa kiwango kikubwa. Papohapo
akamvuta Judith na kumkumbatia, kisha akambusu kwenye paji la uso wake huku mikono
yake iliyokosa uvumilivu ikitalii hapa na pale katika mwili wake mwororo
uliovutia.
Miongoni
mwa mambo ambayo Judith hakuyapenda na yalikuwa ni kero zaidi ya kero, ni
kitendo cha kukumbatiwa-kumbatiwa, kupapaswa, kutomaswa, kupigwa busu au
kufanywa vyovyote vile kwa namna ya kimahaba na mtu, mwanamume asiye mpenzi
wake wa dhati.
Makella
alikuwa ni mmoja wa watu hao, na alimkera! Lakini afanye nini? Hakuwa na budi
kufuata ule usemi wa “mtaka cha uvunguni sharti ainame.”
“Ok, twen’zetu,” Makella alimwambia
Judith huku akimshika mkono na kuanza kutembea tena. Dakika tano baadaye
walikuwa Kiyovu Hotel, wakiwa wamesimama kaunta, na kwa sauti ambayo
haikutofautiana na amri alimwambia mhudumu wa kike aliyekuwa mbele yao: “Chumba
tafadhali.”
“Single au double?”
“Single.”
“Kipo.”
Dakika
chache zilizofuata zilikuwa za
kukamilisha taratibu za upangaji, kisha mhudumu akawapeleka chumbani.
**********
KILIKUWA
ni chumba kilichostahili kuitwa chumba cha daraja la kwanza. Kitanda kikubwa,
zulia zito sakafuni, jokofu lililosheheni vinywaji na televisheni ndogo
iliyoegeshwa ukutani katika kijisanduku cha aina yake zilikuwa ni samani
zilizotosha kukifanya chumba hicho kuwa maridadi. Isitoshe, simu kwa ajili ya
kuwasiliana na utawala wa hoteli ilikuwa juu ya kimeza kidogo kilichokuwa kando
ya sofa mbili.
Mpangaji
hahitaji kuhangaika kuuliza wapi bafu na choo vilipo. Ni kiasi cha mtu kujua
kusoma, ama Kiingereza, Kiswahili, Kinyarwanda au Kifaransa. Milango miwili
yenye maandishi ya lugha hizo, yenye maelekezo kuhusu matumizi ya vyumba hivyo ilikuwa
kulia mwa chumba hicho.
“Karibu..karibu
mpenzi,” Makella alimwambia Judith huku akimtazama kwa namna iliyoashiria hitaji
kamili la starehe ya mapenzi.
Ilikuwa
ni tazama ambayo Judith hakuhitaji mtu wa kumfafanulia kuwa tayari Makella yuko
mbali na yu taabani, uroho wa fisi ukiwa umekwishamtawala. Lakini hakuhofu.
Aliyaepuka macho hayo huku moyoni akisema, tutaona.
Akalifuata sofa moja na kuketi kwa kujiachia kihasarahasara, nusu kaketi, nusu
kalala.
Makella
alimtazama kidogo kisha akaurudisha mlango na kumfuata pale sofani. “ Nakupenda
Judith,” alinong’ona huku akimpapasa katika paja la kulia.
Kwa
Judith, upapaswaji huo haukumletea msisimko wowote. Zaidi, alihisi kupapaswa na
popobawa, kiumbe wa ajabu ambaye miaka kadhaa iliyopita aliviteka vyombo
mbalimbali vya habari hususan yale magazeti pendwa akidaiwa kuwa alikuwa na tabia
ya kuwaingilia wanaume na wanawake kimiujiza
usiku wakiwa wamelala.
Hakuwa
radhi kuuachia mwili wake utumiwe na mtu huyu ambaye hakumtofautisha na shetani,
achilia mbali huyo popobawa. Alimwogopa,
na zaidi alimchukia. Haikumwingia akilini asilani kumwachia Makella apenye
katikati ya miguu yake na kustarehe. Hapana, hakuwa tayari kwa hilo, labda maiti
yake ndiyo inajisiwe.
Hivyo,
wakati Makella akimpapasa huku akimtazama kwa matamanio makubwa, yeye alikuwa
mbali kifikra, akipanga namna ya kujiokoa.
Alishakichunguza
chumba hicho kwa makini. Kumtoroka Makella kwa kupitia dirishani lilikuwa ni
jambo lisilowezekana. Dirisha kubwa lililokuwa kaskazini mwa chumba hicho,
lilisheheni nyavu imara na nondo madhubuti, hivyo isingekuwa rahisi kufanya
chochote katika kujiokoa.
Itaendelea kesho...

No comments:
Post a Comment