Kijana akipanga nyanya kwenye matenga tayari kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.
Hili ni soko lisilo rasmi kando ya Mto Mlowa unaotenganisha vijiji vya Iyayi na Uhominyi katika Kata ya Image wilayani Kilolo. (Picha zote na Daniel Mbega).
Lori aina ya Fuso likipakia matenga ya nyanya kupeleka Dar es Salaam. Wakulima wengi mkoani Iringa wamekuwa wakilalamikia tabia ya kulanguliwa na wafanyabiashara huku nyanya nyingi zikipotea kwa kuharibika tangu zikiwa shambani kutokana na kukosa masoko ya uhakika.
Kujengwa kwa kiwanda kipya cha kusindika bidhaa zitokanazo na mboga mboga mkoani Iringa kutawanufaisha wakulima wengi ambao sasa wanatakiwa kuongeza uzalishaji.
Na Daniel Mbega, Iringa
KILIO cha wakulima wa nyanya mkoani Iringa cha ukosefu wa
masoko ya zao hili sasa kinaonekana kupata ufumbuzi kufuatia ujenzi wa kiwanda
cha kusindika bidhaa za mbogamboga kukaribia kukamilika.
Kiwanda hicho kipya ambacho kipo chini ya kampuni ya Darsh
Industries Limited inayozalisha bidhaa maarufu nchini za Redgold kinajengwa
katika Kijiji cha Ugwachanya, Kata ya Mseke, takriban kilometa 12 kutoka Iringa
mjini.
Kwa mujibu wa mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo
anayeshughulikia masuala ya ujenzi huo, Pratap, kiwanda hicho kinatarajiwa
kuanza uzalishaji Julai mwaka huu.
Pratap alisema kwamba, uzalishaji utakapoanza kiwanda hicho
kitahitaji jumla ya tani 200 (kilogramu 200,000) za nyanya kwa siku, sawa na
kreti 4,500 au magari 20 aina ya Fuso yenye uwezo wa kubeba wa tani 10 kila
moja.
“Tunahitaji tani 200 kwa siku, ndio uwezo wa kiwanda, na
tunawahakikishia wakulima kwamba soko la uhakika litapatikana wala wasiwe na
hofu,” alisema Pratap.
Ofisa huyo alisema kwamba, kiwanda kitanunua nyanya za
maharaja yote bila kubagua, hivyo hakutakuwa na ‘masalo’ yatakayomwagwa na
wakulima wawe na imani kwamba watapata tija kutokana na kilimo hicho.
Aliongeza kusema kwamba, watapeleka makreti ya kubebea
nyanya kwenye vituo vyote vya kukusanyia zao hilo ambavyo vitateuliwa na kwamba
wakulima hawatagharamia usafiri wa kupeleka kiwandani.
“Wakulima kazi yao itakuwa kupeleka nyanya kwenye vituo
ambako tutakuwa tumepeleka makreti ya kubebea, usafiri utakuwa ni juu ya
kiwanda,” alifafanua.
Aidha, alisema kwamba, pamoja na kununua nyanya kwa
wakulima, ambayo ni malighafi ya kiwanda hicho, lakini uongozi utatoa huduma za
ugani kwa wakulima ukishirikiana na Mradi wa Tanzania Agricultural Productivity
(TAPP) pamoja na maofisa ugani wa vijiji na kata husika linakolimwa zao hilo.
Pratap amewataka wakulima kuongeza uzalishaji wa nyanya ili
kukidhi mahitaji ya kiwanda pamoja na kujiongezea kipato.
Nyanya, ambalo ndilo zao kuu la biashara mkoani Iringa
ukiacha mbao zinazotokana na kilimo cha ambacho ni cha muda mrefu, limekuwa na
changamoto kubwa ya masoko, hali inayowafanya wakulima wengi kukata tamaa.
Brotherdanny5.blogspot iliwahi kutembelea Tarafa ya Mazombe,
hususan Kijiji cha Image ambako kilimo cha nyanya kimeshamiri na kujionea malundo
makubwa ya zao hilo yakiwa yametupwa pembeni kutokana na kutofaa kusafirishwa
na kwenda kuuzwa.
“Hii ni hasara kubwa, nimekuja na matenga hamsini, lakini
inaonekana yametoka thelathini tu, haya malundo yote ni nyanya zilizolainika
(masalo) ambazo haziwezi kwenda mahali popote,” alisema Jacob Kamota, mkulima
wa nyanya kutoka Kijiji cha Iyayi, Kata ya Image wilayani Kilolo.
Wakati huo Jacob alikuwa ameacha malundo ya nyanya zisizofaa
kusafirishwa, ingawa zinafaa kwa matumizi ya nyumbani au hata kwa kusindikwa,
hali ambayo alisema inamtia umaskini kwani kungekuwepo na kiwanda walau
angepata chochote na kurudisha gharama zake za kilimo.
Mkulima huyo alisema, gharama za shamba lake lenye ukubwa wa
ekari moja zilikuwa Sh. 1 milioni na kwamba alipovuna alipata jumla ya matenga
80, lakini matenga 30 yalionekana yameharibika tangu shambani huku mengine 20
yakiharibika wakati alipozifikisha nyanya hizo kwenye soko dogo kando ya Mto Mlowa
unaotenganisha kijiji cha Iyayi na Uhominyi katika Kata ya Image.
Bei ya soko ambayo aliikuta kwa siku hiyo ilikuwa Sh. 5,000
tu kwa tenga moja, hivyo kujikuta akiambulia Sh. 150,000 kwa matenga yake 30
ambayo yalionekana yanafaa kusafirishwa.
Jacob ni miongoni mwa wakulima wengi wa Mkoa wa Iringa
wanaojishughulisha na zao la nyanya ambao wamekuwa wakipata hasara kila mwaka
kutokana na ukosefu wa soko la uhakika.
Inaelezwa kwamba, zaidi ya asilimia 70 ya zao hilo la nyanya
inaharibika kutokana na ukosefu wa soko na miundombinu bora, hasa barabara.
Wakulima ndio wanaoathirika zaidi licha ya kutumia gharama
kubwa katika kilimo.
Hali hiyo imewafanya wakulima wengi kuendelea kuogelea
katika lindi la umaskini, huku wengine wakipunguza ukubwa wa mashamba yao ama
kutolima kabisa kutokana na kukosa uwezo wa kuyahudumia.
Maulid Kiboma ‘Papara’, mfanyabiashara wa nyanya, aliiambia
blogu hii kwamba nyanya inayoharibika ni kiasi kikubwa zaidi kuliko inayofika
sokoni.
“Nyanya ikifika hapa sokoni kutoka shambani kiasi kikubwa
inakuwa masalo, hivyo inabidi ichaguliwe na iliyo bora ndiyo inayosafirishwa.
“Kabla ya kufika hapa sokoni mkulima anakuwa ameichambua na
kuyaacha masalo shambani, lakini ikishachambuliwa tena hapa, hata kama ana
matenga 10, anaweza kujikuta amebaki na manne tu ambayo ndiyo yananunuliwa na
sisi wafanyabiashara,” alisema Papara.
Papara alisema, wafanyabiashara pia wanapoifikisha nyanya
hiyo kwenye masoko makubwa, hasa Dar es Salaam, wanalazimika kuichambua, hivyo
kiasi kinachobakia kwa ajili ya matumizi kinakuwa kidogo zaidi ya
kilichozalishwa.
Aliongeza kwamba, wakati mwingine bei katika soko la Dar es
Salaam inaporomoka kiasi kwamba hata wafanyabiashara wenyewe huamua kutonunua
zao hilo kwa ajili ya kusafirisha kwa kuhofia kupata hasara.
“Mwaka huu bei ya tenga moja kwa huku vijijini ilifikia hadi
Sh. 2,000, lakini wakati huo soko la Dar es Salaam linakuwa limeshuka hadi Sh.
10,000, bei ambayo ni hasara kwetu,” alisema.
Mfanyabiashara huyo alisema, bei inaposhuka katika masoko
makubwa inakuwa hasara zaidi kwao wafanyabiashara wa kati, ambapo hata wakipewa
nyanya hizo bure na wakulima hawawezi kuchukua.
“Gharama ya kusafirisha tenga moja, kabla ya manunuzi, ni
Sh. 10,000, sasa nikinunua hapa tenga moja kwa Sh. 5,000 na nikakuta bei ya
sokoni ni Sh. 15,000 nakuwa nimekula hasara, lakini inakuwa hasara zaidi kwa
mkulima ambaye hana mahali pa kupeleka,” aliongeza.
Papara alisema, suluhisho pekee litakalomkomboa mkulima ni
kujenga kiwanda cha kusindika matunda na mboga mboga ili wakulima waweze kuuza
nyanya zote na kukuza kipato chao.
Alisema kiwanda pekee cha Dabaga kilichoko Iringa mjini
hakitoshelezi, hivyo kuitaka serikali na wadau wengine wa maendeleo kufikiria
namna ya kuwakomboa wakulima hao.
Masoud Said, mfanyabiashara wa nyanya kutoka Dar es Salaam,
alisema serikali, pamoja na kufikiria kujenga kiwanda, lakini pia ijenge masoko
ya uhakika vijijini ambayo yatawafanya wakulima wawe na mahali pa kupeleka
bidhaa zao.
Martin Kazingumu Kutika, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Image, akizungumzia
changamoto ya soko la nyanya, alisema inawatesa wakulima wengi, ingawa juhudi
mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali kuboresha mazingira ya soko hilo.
“Nyanya nyingi zinaharibika japokuwa wafanyabiashara wanakuja
huku kuzifuata. Bei nayo inapanda na kushuka kiasi kwamba ni vigumu kwa mkulima
kunufaika moja kwa moja,” alisema.
Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2013, inaelezwa
kwamba Tarafa ya Mazombe, inayoundwa na Kata za Ilula, Image, Irole,
Uhambingeto, Nyalumbu, Lugalo, Mlafu na Ibumu, ilizalisha zaidi ya tani 10,000
za nyanya.
Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni, aliwahi
kukaririwa akisema uzalishaji wa nyanya umeongezeka mkoani humo, ambapo kwa msimu
wa 2011/2012, jumla ya hekta 6,817 zililimwa kwa umwagiliaji na tani 115,514
zilivunwa.
Hata hivyo, alisema changamoto ya masoko inaendelea kupatiwa
ufumbuzi kwa kujenga masoko madogo vijijini kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wa maendeleo kama mashirika ya Techno Save (ambalo sasa halipo),
Muvi na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).
No comments:
Post a Comment