HOTUBA YA MHESHIMIWA WAZIRI WA FEDHA, SAADA MKUYA SALUM (MB)
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA KWA
MWAKA 2014/15
UTANGULIZI:
1.
Mheshimiwa Spika, kufuatia
taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, naomba kutoa hoja kwamba Bunge
lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2014/15.
2.
Mheshimiwa Spika,
awali
ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa
kuniwezesha kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya mwaka 2014/15. Aidha,
natoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Ninaahidi kwamba
nitatekeleza jukumu hili kwa weledi na uadilifu. Vile vile, nawapongeza Mhe.
Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Mhe. Adam Kighoma Ali Malima (Mb) kwa kuteuliwa
kuwa Naibu Mawaziri wa Wizara ya Fedha. Kadhalika, namshukuru pia aliyekuwa
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janeth Zebedayo Mbene (Mb) kwa utendaji kazi wake
mahiri na tunamuombea Mwenyezi
Mungu ampe nguvu na afya njema katika kazi zake mpya Wizara ya Viwanda na
Biashara. Nichukue pia fursa hii kumpongeza Bw. Rished M. Bade kwa kuteuliwa
kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
3.
Mheshimiwa Spika, napenda
kukupongeza wewe mwenyewe, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa
Bunge kwa kuongoza vyema majadiliano ya Bunge la Bajeti.
4.
Mheshimiwa Spika, naomba
nitumie nafasi hii kuishukuru kwa namna ya pekee Kamati ya Kudumu
ya Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Luhaga Joelson
Mpina (Mbunge wa Kisesa) na Makamu wake Mhe. Dunstan Luka Kitandula (Mbunge wa
Mkinga) kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa
kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Aidha, nachukua nafasi hii
kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti Mhe. Andrew John Chenge
(Mbunge wa Bariadi Magharibi) pamoja na Kamati nzima kwa ushauri wao. Katika
uandaaji wa hotuba hii, Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati
hizo pamoja na ushauri na maoni ya hoja mbalimbali zilizotolewa wakati wa mjadala wa bajeti
ya Wizara kwa mwaka 2013/14.
5.
Mheshimiwa Spika, kama
unavyofahamu, Wizara ilipata pigo kwa kuondokewa na kiongozi wetu
mkuu Marehemu Dkt. William Augustao Mgimwa. Tunawashukuru Viongozi wa Serikali,
Waheshimiwa Wabunge, Washirika wa Maendeleo, Taasisi mbalimbali pamoja na
wananchi kwa ushirikiano waliotupa kipindi chote cha msiba. Tumeendelea kuenzi
misingi imara aliyotujengea marehemu katika kutekeleza majukumu ya Wizara.
Aidha, tunapenda kutoa pole kwa ndugu na jamaa kufuatia kifo cha aliyekuwa
Mbunge wa Chalinze Marehemu Saidi Ramadhani Bwanamdogo. Vile vile, napenda
kutoa pole kwa Mheshimiwa Zuberi Zitto Kabwe kwa msiba wa mama yake mzazi
aliyefariki tarehe 01 mwezi Juni, 2014. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu
mahali pema peponi. Amina.
6.
Mheshimiwa Spika, tarehe
27 mwezi Mei 2014, Wizara ya Fedha ilipata pigo tena baada ya
kifo cha mke wa Katibu Mkuu - Hazina. Kwa namna ya kipekee naomba nitumie tena
fursa hii kutoa pole kwa Dkt. Servacius Likwelile kwa kufiwa na mkewe.
Hata hivyo Dr. Likwelile ameendelea kutekeleza majukumu yake katika kipindi
chote cha msiba.Wizara inatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia yake
kwa msiba wa mpendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho ya marehemu
mahali pema peponi. Amina.
7.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuwapongeza, Mhe. Yusuf Salim Hussein Mbunge wa Chambani, Mhe.
Godfrey William Mgimwa (Mbunge wa Kalenga) na Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete
(Mbunge wa Chalinze) kwa kuchaguliwa kwao.
8.
Mheshimiwa Spika,
kwa
namna ya kipekee napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mhe.
Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge
wa Mpanda Mashariki kwa hotuba yake nzuri ambayo imetoa mwelekeo wa shughuli za
Serikali kwa mwaka 2014/15.
9.
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba yangu nitaanza kuelezea mapitio ya utekelezaji wa mipango
ya Wizara katika mwaka 2013/14. Nitaelezea pia mikakati mbalimbali ambayo Wizara
imeweka kwa mwaka 2014/15 ili kuendelea kuboresha utekelezaji wa majukumu yake
ya msingi yakiwemo: usimamizi wa Bajeti ya Serikali; ukusanyaji mapato ya
Serikali; usimamizi wa misaada na mikopo; ulipaji wa Deni la Taifa; usimamizi
wa matumizi ya fedha za umma; usimamizi na udhibiti wa ununuzi wa umma;
usimamizi wa utekelezaji wa MKUKUTA; na usimamizi wa mashirika na taasisi za
umma.
10.
Mheshimiwa Spika, mwisho
nitawasilisha bajeti ya mwaka 2014/15 kwa mafungu saba ya wizara
ya fedha ambayo ni fungu 7, 10, 13, 21, 22, 23 na fungu 50 pamoja na fungu 45
la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
11.
Mheshimiwa Spika, naomba
sasa uniruhusu nisome maelezo haya kwa muhtasari na hotuba yote
kama inavyoonekana kwenye vitabu vya hotuba iingie kwenye Hansard.
MAPITIO
YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2013/14 NA MALENGO YA
MWAKA 2014/15
12. Mheshimiwa
Spika, malengo
yaliyozingatiwa katika
utekelezaji
wa majukumu ya wizara pamoja na utekelezaji wake kwa mwaka 2013/14 ni kama
unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa nne na wa tano.
Mfumo wa Tekeleza
Sasa kwa Matokeo Makubwa
13.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, kupitia Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, Wizara
ya Fedha katika maabara ya utafutaji wa rasilimali fedha iliwekewa malengo
yafuatayo: kuongeza mapato mapya ya kodi ya shilingi trilioni 1.16; kuongeza
mapato mapya yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 96.7; kudhibiti matumizi; na
kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi ya Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa
katika sekta zinazotekeleza miradi hiyo.
14.
Mheshimiwa Spika, hadi
mwezi Aprili 2014, ukusanyaji
wa mapato kutoka
vyanzo vilivyoibuliwa chini ya BRN umefikia shilingi
bilioni 338 sawa na asilimia 29.14 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni
1.16. Matokeo yasiyoridhisha yalisababishwa na baadhi ya mapendekezo ya BRN
kutokutekelezwa katika mwaka 2013/14. Mapendekezo hayo ni kubadilisha mfumo wa
ushuru wa bidhaa zisizo za petroli kutoka specific kwenda advalorem (makisio
shilingi bilioni 386) na kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia tano kwenye bidhaa
zinazotoka nje ya nchi (makisio shilingi bilioni 225.6). Kwa vile ukusanyaji wa
mapato ndio msingi wa kufanikiwa kwa BRN, Serikali inachambua vyanzo mbadala
vya kufidia mapato haya ili kuhakikisha lengo kuu la kuongeza mapato kwa
shilingi trilioni 3.48 linafikiwa ifikapo mwaka 2015/16.
Mwenendo wa Uchumi
15. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara
kupitia
Benki Kuu iliendelea na jukumu la kuandaa, kusimamia na kutathmini utekelezaji
wa sera ya fedha inayolenga kuwa na kiwango kidogo cha mfumuko wa bei kwa ajili
ya kuhakikisha gharama za maisha haziongezeki. Kutokana na juhudi hizi, mfumuko
wa bei umeshuka kutoka wastani wa asilimia 16 mwaka
2012 hadi kufikia wastani wa asilimia 7.9 mwaka 2013. Katika kipindi hiki
uchumi umeendelea kuimarika huku ukuaji halisi wa Pato la Taifa ukiongezeka kwa
asilimia 7.0 katika kipindi cha mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 6.9
katika mwaka 2012. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kiasi kikubwa ni pamoja
na mawasiliano asilimia 22.8, huduma za kifedha asilimia 12.2, ujenzi asilimia
8.6, na uuzaji bidhaa wa jumla na rejareja asilimia 8.3. Katika mwaka 2014/15,
Wizara kupitia Benki Kuu itaendelea kushirikiana na wadau wote katika
kuhakikisha kwamba lengo la msingi la utulivu wa bei na ukuaji wa uchumi
linadumishwa.
Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa
Bajeti ya Serikali
16.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara
imeratibu
uandaaji wa Mwongozo wa Mpango na Bajeti kwa kipindi cha 2014/15 – 2016/17 kwa
Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na
kusambaza kwa wadau mwezi Desemba kama ilivyopangwa. Aidha, Wizara imeandaa na
kuchapisha vitabu vya bajeti ya Serikali
vya mwaka 2014/15 (Volume I, II, III na IV) kama vilivyowasilishwa Bungeni kwa
ajili ya mjadala wa Bunge la Bajeti la mwaka 2014/15 unaoendelea; kitabu cha
tafsiri rahisi ya bajeti ya Serikali (Citizen’s Budget) kwa mwaka 2013/14; na
Kitabu cha Budget
Background and Medium Term Framework –
2013/14 – 2015/16.
17. Mheshimiwa
Spika, utekelezaji
zaidi na malengo kwa
mwaka
2014/15 ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ukurasa wa saba mpaka
ukurasa wa tisa.
Usimamizi wa Misaada
na Mikopo
18. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14,
Wizara ilifanikisha kusainiwa kwa
mikataba 18 kwa ajili ya misaada na mikopo nafuu yenye thamani ya jumla ya
shilingi bilioni 958.027 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Aidha, Wizara
imeendelea kuratibu ukamilishaji wa Mwongozo mpya wa Ushirikiano wa Maendeleo -
Development Cooperation Framework ambao utachukua nafasi ya
Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA). Mwongozo huu una lengo
la kusimamia
ushirikiano wa maendeleo baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo na kuendeleza
mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa MPAMITA. Lengo la ujumla ni
kupatikana ufanisi katika misaada kutoka kwa Washirika wa maendeleo na
kubainisha wajibu wa kila mdau wa maendeleo wakiwemo raia, wabunge, asasi
zisizo za kiserikali na sekta ya habari.
19. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara
imepanga
kufanya yafuatayo: kuzindua Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo na kuandaa
mpango kazi wake pamoja na kuhamasisha matumizi yake kwa Washirika wa
Maendeleo, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Serikali za Mitaa, Taasisi Binafsi na
Waheshimiwa Wabunge; kutathmini utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali
inayotekelezwa kwa fedha toka Washirika wa Maendeleo kwa nia ya kuhakikisha
kwamba thamani ya fedha inapatikana katika miradi hiyo; kushiriki kwenye majadiliano
na Jumuiya za kikanda na kimataifa; na kuendelea kutafuta fedha za misaada na
mikopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na Misaada ya Kiufundi kutoka kwa Mashirika
ya Kimataifa na nchi wahisani.
Ulipaji wa Deni la
Taifa
20.
Mheshimiwa Spika, Deni
la Taifa limeendelea kusimamiwa na Sheria ya Madeni ya mwaka 1974
na marekebisho yake ya mwaka 2004. Wizara imeendelea kutoa kipaumbele katika
ulipaji wa madeni kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya riba. Katika kipindi
cha Julai, 2013 hadi Aprili, 2014 malipo ya deni la ndani yalifikia shilingi
bilioni 1,694.53 ambapo kati ya malipo hayo riba ni shilingi bilioni 581.20 na
Mtaji (principal rollover) ni shilingi bilioni 1,113.33. Aidha, deni la nje
limelipwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 340.22, kati ya kiasi hicho malipo ya
riba ni shilingi bilioni 201.52 na deni halisi principal ni shilingi
bilioni 138.70.
21.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kulipa madeni ya ndani na nje
kwa wakati ikiwa ni pamoja na kulipa kwa wakati madeni mbalimbali ambayo serikali
imeingia mikataba (Contractual Liabilities) na madai ya dharura (Contingent
Liabilities) pindi yanapotokea.
Usimamizi wa
Matumizi ya Fedha za Umma
22.
Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kujenga uwezo wa usimamizi wa matumizi ya fedha za umma
kwa kudhamini mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 313 wa kada ya uhasibu, ugavi
na kompyuta kutoka kwenye wizara, idara za serikali, sekretariati za mikoa,
manispaa, halmashauri za miji na wilaya waliopo vyuoni na watumishi 218
walipewa mafunzo ya muda mfupi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi
wa matumizi ya fedha za umma. Aidha, Wizara imeendelea kusambaza Mfumo wa
Malipo wa Kielektroniki -TISS. Mikoa hiyo ipo katika kitabu cha hotuba
ya bajeti ukurasa wa 11.
23.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji
zaidi na malengo ya mwaka 2014/15 upo katika kitabu cha hotuba ya
bajeti ukurasa wa 12 na 13.
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha
za Umma - Public Finance Management Reform Programme (PFMRP)
24. Mheshimiwa
Spika, Wizara
kupitia Programu ya
Maboresho
ya Usimamizi wa Fedha za Umma imekamilisha utafiti wa mfumo wa kupeleka fedha
kwenye Serikali za Mitaa, mpango wa utekelezaji wa utafiti huo umeandaliwa na
utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2014/15. Aidha, utafiti juu ya mifumo
ya fedha inayotumiwa na Serikali kwa lengo la kuiunganisha mifumo hiyo ili
kuboresha usimamizi wake umekamilika. Vile vile, Wahasibu 522 kutoka Wizara
mbalimbali, hazina ndogo na sekretarieti za mikoa walipata mafunzo juu ya
Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Hesabu katika Sekta ya Umma na
watumishi wengine 34 ambao wanasimamia programu hii kutoka katika wizara na
taasisi walipata mafunzo ya kusimamia Mabadiliko na Kuandaa Mipango Mkakati -Change
Management and Strategic Planning.
Mafunzo haya yalilenga kuwajengea uwezo wa
kuandaa mipango na bajeti inayolenga katika kutekeleza maboresho ya usimamizi
wa fedha za umma.
25.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara
itaendelea
kuboresha usimamizi wa fedha za umma kwa kuendelea na utekelezaji wa Awamu ya
Nne ya Programu ya PFMRP kwa kufanya yafuatayo: kupitia na kuboresha mifumo ya
kifedha na kuangalia njia bora ya kuiunganisha baada ya utafiti kukamilika; na
kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani katika wizara, idara, wakala za Serikali na
halmashauri za Serikali za Mitaa juu ya ukaguzi wa mifumo ya fedha, usimamizi
na ukaguzi wa vihatarishi, ukaguzi wa bajeti na mishahara, na ukaguzi wa miradi.
Sera ya Ununuzi wa
Umma
26. Mheshimiwa
Spika, utekelezaji
wa sera na udhibiti wa
ununuzi
wa umma, rufaa za zabuni za umma na huduma ya ununuzi serikalini ni kama unavyooneshwa
katika kitabu changu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 14 hadi ukurasa wa 18.
Usimamizi wa Mali ya
Serikali
27. Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara iliendelea kuandaa Sera ya
Mali ya Umma. Lengo la sera hii ni kusimamia na kutoa miongozo ya udhibiti wa
mali ya umma. Aidha, Wizara ilifanya uthamini wa mali ya Serikali katika mikoa
mitano na wizara mbili, hivyo kufanya wizara, idara zinazojitegemea na wakala
wa Serikali zilizofanyiwa uthamini kufikia 42. Katika kipindi hicho, usimikaji
wa mfumo wa uhakiki wa mali ya umma ulikamilika. Vile vile, Wizara iliendelea
na zoezi la kuondosha mali chakavu katika wizara na idara za Serikali ambapo
jumla ya shilingi bilioni 1.58 zilikusanywa kutokana na mauzo ya vifaa hivyo na
shilingi milioni 12.83 kutokana na utoaji wa leseni za udalali. Utekelezaji
zaidi na malengo kwa mwaka 2014/15 ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha
hotuba ya bajeti ukurasa wa 18.
Mpango
wa Millenium Challenge Account – Tanzania (MCA-T)
28. Mheshimiwa
Spika, Programu
ya Millenium Challenge Account Tanzania iliendelea
na ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji,
nishati ya umeme na maji. Miradi yote ya barabara imekamilika isipokuwa sehemu
ya Laela- Sumbawanga katika barabara ya Tunduma-Sumbwanga ambayo inatarajiwa
kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka 2014. Miradi ya umeme na maji imekamilika
na ipo katika kipindi cha uangalizi. Aidha, kutokana na utekelezaji wa
kuridhisha, Tanzania imekidhi vigezo na hivyo itanufaika na awamu ya pili ya
msaada wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Changamoto za Milenia
(MCC). Katika awamu ya pili, miradi itakayofadhiliwa ni ya umeme na barabara za
vijijini Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Ukaguzi wa Ndani
29. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara
imetekeleza
yafuatayo: kutoa Mwongozo wa Kamati za Ukaguzi katika Sekta ya Umma kwa lengo
la kuhakikisha utendaji wenye tija kwa Kamati zote za Ukaguzi; kutoa mafunzo ya
kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani 458, wajumbe wa Kamati za Ukaguzi na wadau
wa ukaguzi wa ndani wapatao 567; kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo 11;
ukaguzi wa orodha ya malipo ya mishahara; na kuhakiki madai mbalimbali
yaliyowasilishwa wizarani kabla ya kulipwa.
30. Mheshimiwa
Spika, wizara
kwa kushirikiana na Taasisi za
Serikali
itaendelea kuimarisha ofisi za Mkaguzi Mkuu wa ndani kwa lengo la kusimamia
matumizi ya fedha. Utekelezaji zaidi na malengo ya mwaka 2014/15 upo ukurasa wa
20 na 21 wa kitabu cha hotuba ya bajeti.
Ukaguzi wa Hesabu za
Serikali
31.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imetekeleza kazi zake
kwa mujibu wa sheria. Ofisi imeendelea kuwa mshirika katika Bodi ya Ukaguzi ya
Umoja wa Mataifa katika kukagua taasisi za Umoja wa Mataifa. Aidha, Ofisi
imeendesha mafunzo kwa Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali na
Kamati ya Bajeti kwa lengo la kuzijengea uwezo wa kuimarisha uwajibikaji na
utawala bora. Vile vile, ukaguzi wa mapato na matumizi ya vyama vya siasa
vyenye usajili wa kudumu unaendelea.
32.
Mheshimiwa Spika, malengo
ya Ofisi ya Taifa Taifa ya Ukaguzi kwa mwaka 2014/15 yanapatikana
katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 21 na 22
Uratibu wa
Utekelezaji wa MKUKUTA
33. Mheshimiwa
Spika, Wizara
imeendelea kuratibu
utekelezaji
wa MKUKUTA II kwa kufanya ufuatiliaji, tafiti, na tathmini na kuandaa taarifa
ya utekelezaji na hali ya Umaskini nchini ili kuwezesha maamuzi ya kisera,
kibajeti na
kiutekelezaji. Kazi
ya uandaaji wa
Taarifa ya Mwaka
ya Utekelezaji
wa MKUKUTA II imekamilika na kuwekwa katika tovuti ya Wizara. Aidha, Wizara
inaendelea kukamilisha Taarifa ya Maendeleo ya Malengo ya Milenia. Taarifa ya
awali inaonesha kuwa umaskini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania Bara ni
asilimia 28.2 ambapo kwa Dar es Salaam ni asilimia 4.2, maeneo mengine ya mjini
ni asilimia 21.7 na maeneo ya vijijini ni asilimia 33.3. Umaskini wa chakula ni
asilimia 9.7 ambapo kwa Dar es Salaam ni asilimia 1.0, maeneo mengine ya mjini
ni asilimia 8.7 na maeneo ya vijijini ni asilimia 11.3.
34. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara
imepanga
kutekeleza yafuatayo: kukusanya na kuchambua taarifa mbalimbali kutoka katika
Wizara, Idara na Wakala za Serikali ili kuandaa Taarifa ya mwaka ya Utekelezaji
wa MKUKUTA II; kuandaa taarifa ya mwisho ya kutathimini utekelezaji wa Malengo
ya Maendeleo ya Milenia; kufanya mapitio ya MKUKUTA II; kukamilisha Mpango wa
Utekelezaji wa Kinga ya Jamii pamoja na kuainisha viashiria vya upimaji juhudi
za kinga ya jamii; na kuratibu mkutano wa kitaifa wa kujadili sera za kupambana
na umaskini nchini. Pia Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaandaa
mapendekezo ya hatua
zitakazofuata baada ya MKUKUTA II kufikia kikomo mwezi Juni, 2015.
35.
Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia Mradi wa SELF II imeendelea kutoa mikopo kwa
wajasiriamali ambapo hadi kufikia Aprili 2014, mikopo yenye thamani ya shilingi
bilioni 8.6 ilikopeshwa kwa wajasiriamali 4,943 kupitia Asasi ndogo 103. Kati
ya waliokopeshwa, wanawake ni 2,040 sawa na asilimia 41 na wanaume ni 2,903
sawa na asilimia 59. Kwa wastani, urejeshwaji wa Mikopo ya Mradi wa SELF
umeendelea kuwa wa ufanisi mzuri katika kiwango cha asilimia 90 hivyo kuwezesha
fedha za mkopo kuzunguka na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
36.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji
zaidi kwa mradi wa SELF pamoja na malengo ya mradi huu kwa mwaka
2014/15 yanapatikana katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 24.
Sheria na Miswada ya
Fedha
37. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara kwa
kushirikiana
na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilifanya marekebisho
ya Sheria mbalimbali za Fedha kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 - The
Finance Act, 2013. Lengo la marekebisho hayo ni kuweka usimamizi mzuri wa
kodi na fedha za umma. Aidha, Sheria mbalimbali zilizopitishwa na Bunge ni
pamoja na Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu ya mwaka 2013 -
The GEPF Retirement Benefit Fund Act, 2013 na marekebisho ya
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa ya mwaka 2013 - The Excise (Management and
Tariff) (Amendment) Act, 2013 yaliyopitishwa na Bunge katika Mkutano
wa 13 mwezi Desemba, 2013 yaliyolenga kuondoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwenye Sim
Card.
38. Mheshimiwa
Spika, utekelezaji
zaidi wa sheria na
miswada
ya fedha pamoja na Ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ni kama
unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 25 hadi ukurasa wa
27.
Ubia kati ya Sekta
ya Umma na Sekta Binafsi – PPP
39. Mheshimiwa
Spika, Wizara
imeendelea kupokea na
kuchambua
maandiko ya miradi inayokusudiwa kutekelezwa kwa
utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Katika mwaka 2013/14,
Wizara imepokea na kuchambua miradi minne ya PPP. Katika uchambuzi wa miradi
imebainika kwamba kuna upungufu katika upembuzi yakinifu pamoja na ukosefu wa
Wataalam wa kufanya upembuzi huo. Aidha, Wizara imeshiriki kutoa mapendekezo ya
kurekebisha Sheria ya Ubia Na. 18 ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake kwa lengo
la kuweka usimamizi mzuri wa ubia.
40.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2014/15 Wizara
imetenga
fedha za kuanzisha Mfuko wa Kuwezesha Utekelezaji wa Miradi ya Ubia -PPP
Facilitation Fund.
Udhibiti wa Fedha
Haramu na Ufadhili wa Ugaidi
41.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara
kupitia
Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu imepokea na kuchambua taarifa 46 za
miamala shuku inayohusu fedha haramu na ufadhili wa ugaidi na taarifa 14 za
kiintelijensia zimewasilishwa kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa
sheria. Aidha, mafunzo ya kudhibiti fedha haramu na ufadhili
wa ugaidi yametolewa kwa watoa taarifa 135 na washiriki 86 kutoka katika vyombo
vinavyosimamia utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu na Mali
Athirika. Vile vile, mafunzo hayo yametolewa kwa washiriki 49 kutoka Mamlaka za
Udhibiti. Kadhalika, masuala yanayohusiana na utoroshaji wa fedha nje ya nchi
yanaratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Kamati iliyoundwa
na Serikali, na taarifa ya Kamati hiyo itapatikana baada ya kazi hiyo
kukamilika.
42. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara
kupitia
Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu itatekeleza yafuatayo: kupokea na kuchambua
taarifa za miamala shuku inayohusu utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa
ugaidi; kutoa mafunzo kwa vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria na kwa
watoa taarifa; kutoa miongozo ya kudhibiti fedha haramu na ufadhili wa ugaidi
kwa watoa taarifa; kuratibu zoezi la kutathmini mianya na viashiria vya fedha
haramu na ufadhili wa ugaidi katika sekta mbalimbali nchini; na kuendelea na
hatua za kujiunga na Umoja wa Kupambana na Biashara ya Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi Duniani - EGMONT
Group of Financial Intelligence Units.
Tume ya Pamoja ya
Fedha
43.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara kupitia Tume ya Pamoja ya Fedha
imekamilisha Stadi ya Kubainisha Mfumo Bora wa Kodi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, pamoja na kuendelea na Uchambuzi wa Uhusiano wa Mwenendo wa Uchumi na
Mapato ya Muungano.
44.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara kupitia Tume ya Pamoja ya Fedha inatarajia
kukamilisha Stadi ya Kubainisha Mwenendo wa Uchumi na Mapato ya Muungano wa
Tanzania, na kufanya Stadi ya Uwekezaji katika Mambo ya Muungano. Aidha, Tume
inatarajia kuhuisha Takwimu mbalimbali za Stadi zilizofanywa na Tume.
Habari, Elimu na
Mawasiliano kwa Umma
45. Mheshimiwa
Spika, utekelezaji
wa wizara juu ya habari,
elimu
na mawasiliano kwa umma pamoja na masuala ya watumishi yanapatikana katika
kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa 28 hadi ukurasa wa 30.
Usimamizi wa
Mashirika na Taasisi za Umma
46. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara
kupitia
Ofisi ya Msajili wa Hazina imechambua na kutangaza katika Gazeti la Serikali
mashirika 10 ambayo yanatakiwa kuchangia asilimia 10 ya mapato ghafi katika
Mfuko Mkuu wa Serikali. Hadi kufikia Aprili 2014, kiasi cha shilingi bilioni
25.0 kimekusanywa ikiwa ni asilimia 69.4 ya makadirio ya kukusanya shilingi
bilioni 36 kwa mwaka 2013/14. Aidha, katika kutekeleza zoezi la kuingia
mikataba ya utendaji na Bodi za Mashirika ya Umma, Wizara inakamilisha
majadiliano na Bodi za Mashirika ya Umma. Vile vile, zoezi la kumpata Msajili
wa Hazina limefikia hatua za mwisho. Matarajio ni kwamba uteuzi utafanyika
kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.
47.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara inatarajia kutekeleza yafuatayo: kusimamia
utendaji wa Bodi za Wakurugenzi wa mashirika na taasisi za umma na kuingia
mikataba ya utendaji na Bodi za mashirika ya umma; kusimamia mikakati ya
kurekebisha mashirika ya umma na kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mashirika
ya umma yaliyobinafsishwa; na kuimarisha usimamizi wa mashirika na taasisi za
umma ili kuongeza mapato ya Serikali.
48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Shirika Hodhi la Mali za Umma (CHC) imeendelea na zoezi la ubinafsishaji na urekebishaji wa mashirika ya Umma. Wizara inaendelea na zoezi la tathmini ya utendaji wa mashirika mengine yaliyobinafsishwa kwa lengo la kufahamu kama makubaliano ya mikataba ya mauzo yanazingatiwa na kuchukua hatua stahiki.Mafao ya Wastaafu na Mirathi49. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha kumbukumbu za Wastaafu, kulipa mafao na michango ya kisheria kwa wakati. Hadi Aprili 2014, kumbukumbu za wastaafu 142,014 zimehifadhiwa kwenye mfumo wa kompyuta (SAPERION) na shilingi bilioni 220.79 sawa na asilimia 87 ya makadirio kimelipwa kama mafao ya wastaafu wanaolipwa pensheni na Hazina. Aidha, Wizara imefanya uhakiki wa wastaafu walio kwenye daftari la Hazina katika mikoa tisa. Vile vile, shilingi bilioni 522.86 sawa na asilimia 76 ya makadirio ya mwaka kimelipwa kama michango ya mwajiri kwa watumishi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa wanaochangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na michango ya Bima ya Afya.50. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia na kuratibu shughuli za Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa PPF na Mfuko wa Mafao ya Kustaafu (GEPF). Utekelezaji kwa mwaka 2013/14 ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 31 hadi ukurasa wa 34.Mamlaka ya Mapato Tanzania51. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2014, mapato halisi ya kodi yalifikia shilingi bilioni 7,771.5 sawa na asilimia 75 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 10,395.4. Kodi zilizochangia zaidi ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani, Kodi ya Kampuni na Kodi ya Mapato ya Ajira ambazo kwa pamoja zilichangia zaidi ya asilimia 80 ya mapato hayo.52. Mheshimiwa Spika, licha ya hatua mbali mbali ambazo zimechukuliwa katika kipindi cha mwaka 2013/14, kumekuwa na changamoto katika kufikia lengo la makusanyo ya mapato. Sababu zilizochangia kutofikia malengo ni pamoja na: mapato pungufu ya Kodi ya Kampuni kuliko ilivyotarajiwa kutoka kwenye baadhi ya kampuni za madini; na kushuka kwa makusanyo hususan Kodi ya Zuio kutokana na kupungua kwa makusanyo kwenye shughuli za utafiti wa gesi na mafuta. Sababu nyingine ni pamoja na kufutwa kwa Tozo ya Kadi za Simu - SIMcard levy na makusanyo hafifu kutoka kwenye Ushuru wa Bidhaa wa Huduma za Uhawilisho wa Fedha - Money Transfers. Kwa upande wa Forodha sababu zilizochangia kutofikiwa kwa lengo la makusanyo ni ukuaji mdogo wa uingizwaji wa bidhaa kutoka nje, na ongezeko la kuingiza bidhaa kupitia njia zisizo rasmi(panya roads) na bandari bubu..Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kudhibiti ukwepaji kodi, wizara kupitia TRA inachukua hatua kadhaa za kudhibiti upotevu wa mapato kupitia bandari bubu na panya roads, kwa kufanya upelelezi ili kuzigundua njia hizo na kuzidhibiti kwa kutumia Kikosi Kazi cha Kuzuia Magendo (Flexible Anti-Smuggling Team). Aidha, elimu kwa wafanyabiashara na wananchi wanaozunguka eneo la Pwani imeendelea kutolewa, ushirikiano na vyombo vingine vya udhibiti yaani Polisi Uhamiaji na Usalama wa Taifa umeanzishwa; na kufanya doria katika maeneo hayo.53. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuimarisha makusanyo ya kodi, Mamlaka imeendelea kufanya yafuatayo: kuimarisha matumizi ya Mashine za Kieletroniki za kutoa Risiti -Electronic Fiscal Devices (EFDs) ambapo kwa sasa inakamilisha zoezi la kuwaingiza wafanyabiashara wote wanaostahili kuanza kutumia mashine hizo; kuanzisha Mfumo wa Uthamini wa Mizigo ya Forodha - Tanzania Customs Integrated System (TANCIS) ambao umeanza kutumika mwezi Aprili 2014 pamoja matumizi ya mfumo wa kuthamini magari chakavu; na kuanzisha Kitengo cha Kodi ya Kampuni za Kimataifa - International Tax Unit kwa lengo la kubaini na kudhibiti mianya ya kupotea kwa kodi inayolipwa na kampuni za kimataifa zilizowekeza nchini.54. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania imeanza kutekeleza makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuweka mazingira ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory - SCT) kuanzia Januari, 2014. Ili kuhakikisha kwamba mizigo ya nchi jirani haiuzwi nchini kinyume na utaratibu wa forodha, mfumo wa ki-eletroniki wa ufuatiliaji wa mizigo inayosafirishwa utatumika. Kupitia mfumo huu, mizigo na ama vyombo vya usafirishaji hufungwa lakili ya ki-eletroniki (electronic seal) na kifaa cha mawasilaino ambavyo huunganishwa na mfumo mkuu ili kuonesha mwenendo mzima wa usafiri hadi mzigo husika utakapovuka mpaka wa nchi. Aidha, mbinu nyingine za udhibiti saidizi kama doria, usuluhishi wa taarifa (reconciliation) na ukaguzi zitatumika ili kuongeza udhibiti.Rufaa za Kodi55. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa rufaa za kodi ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 35 na 36.Huduma za KibenkiBenki Kuu ya Tanzania
56. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Benki Kuu imeendelea kusimamia Sekta ya Kibenki ambapo kati ya kipindi cha Machi 2013 na Machi 2014, idadi ya benki na taasisi za fedha imeongezeka kutoka 51 na matawi 585 hadi 53 na matawi 625 kote nchini. Jumla ya mali ya sekta ya kibenki imekua kutoka shilingi trilioni 17.9 hadi shilingi trilioni 21.1. Kiwango cha mitaji kilifikia wastani wa asilimia 18.5 ikilinganishwa na kiwango cha asilimia 10 kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, Mfumo wa Taarifa za Wakopaji - Credit Reference Bureau unaendelea vyema, ambapo hadi sasa kampuni mbili zimepewa leseni ambazo ni: kampuni ya Creditinfo Tanzania Limited iliyoanza kazi Juni 2013 na kampuni ya Dun & Bradstreet Credit Bureau(T) Limited iliyoanza kazi Septemba 2013. Kampuni nyingine kwa jina la Transunion, nayo hivi karibuni imepewa leseni ya muda na inajiandaa kuanza kufanya kazi.
57.
Mheshimiwa Spika, Kampuni
hizi kwa sasazinaandaa taarifa za wateja kutoka kwenye kumbukumbu
ambazo zinahifadhiwa Benki Kuu. Taarifa hizi bado zinafanyiwa uhakiki kabla ya
kuanza kutumika rasmi. Mara baada ya data bank hiyo kukamilika, makampuni haya
ya Credit Reference yataanza kufanya kazi hiyo kikamilifu na kwa usahihi. Benki
Kuu inaendelea kuyahimiza mabenki ambayo bado hayajawasilisha taarifa kufanya
hivyo.
58.
Mheshimiwa Spika, Tarehe
30 Novemba 2013, Marais wa Afrika Mashariki walitia sahihi
Itifaki ya Umoja wa Fedha ya Afrika Mashariki. Tukio hili, ndilo
limeanzisha safari yetu ya kwenda kwenye hatua ya kuwa na sarafu moja ifikapo
mwaka 2024. Chini ya Itifaki hii, tumekubaliana vigezo ambavyo tutatakiwa
tufikie kabla ya kuingia kwenye umoja huo na road map ya miaka 10
ambayo itaanza kutekelezwa mara tu baada ya nchi zote kuridhia
utekelezaji wake. Katika mpango huo, mambo muhimu ni; kukamilisha utekelezaji
wa Umoja wa forodha na Itifaki ya soko la pamoja; kuoanisha mifumo ya kifedh, sera
za ubadilishaji wa fedha za kigeni, sera za bajeti, na mifumo ya malipo;
uhuisha mifumo ya takwimu na; kuhuisha sheria zote zinazohusiana na uanzishwaji
wa umoja wa kifedha
Benki ya Maendeleo
TIB
59. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14, TIB Development Bank (zamani
Benki ya Rasilimali) iliendelea na marekebisho ya ndani ambapo shughuli
za Benki zimegawanywa katika kampuni mbili ambazo ni TIB Development
Bank Limited inayohusika na shughuli za maendeleo
na TIB Corporate Finance Limited inayohusika na shughuli za biashara.
60. Mheshimiwa
Spika, maelezo ya utekelezaji wa majukumu ya Benki ya Maendeleo TIB,
Benki ya Maendeleo ya Kilimo, Twiga Bancorp na Benki ya Posta kwa mwaka 2013/14
ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 37 hadi
ukurasa 40.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo -
TADB
61. Mheshimiwa
Spika, kufuatia
uamuzi wa Serikali
kuanzisha
Benki ya Kilimo, Wizara imetekeleza yafuatayo: kuzindua Bodi ya Wakurugenzi wa
Benki; kukamilisha zoezi la upatikanaji wa Mtendaji Mkuu na Wakuu wa Idara;
kuandaa Muundo wa Benki na Muundo wa Utumishi; kuandaa majukumu ya wafanyakazi;
kuandaa rasimu ya Mpango wa Biashara; na kupatikana kwa ofisi za Benki. Mwaka
2014/15, Benki ya Maendeleo ya Kilimo inatarajia
kupata leseni ya biashara, kuajiri wafanyakazi na kuanza kutoa huduma.
Sera ya Taifa ya
Huduma Ndogo za Kifedha
62. Mheshimiwa
Spika, Wizara
imeanza kufanya mapitio ya
Sera
ya Taifa ya Huduma Ndogo za Kifedha - National Microfinance Policy,
2000 ili kuondoa mapungufu ya kisheria yaliyojitokeza katika
utekelezaji wake kwa lengo la kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi na kijamii
pamoja na kuweka mazingira mazuri katika ukuaji wa sekta hiyo. Aidha, katika
mwaka 2014/15, Wizara itakamilisha maandalizi ya Sera ya Taifa ya Taasisi Ndogo
za Huduma za fedha pamoja na kutunga Sheria ya Taasisi ndogo za huduma za
kifedha - Microfinance Act.
Huduma za Bima
Mamlaka ya Usimamizi
wa Shughuli za Bima – TIRA
63. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara
kupitia
Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima imekamilisha na kutoa Mkakati wa
Kuendeleza Bima ya Watu wa Kipato cha Chini - National Micro Insurance
Strategy 2014-2017. Aidha, hadi kufikia Aprili 2014, kampuni 30, madalali 100
na mawakala 500 wa bima walisajiliwa. Vile vile, mauzo ya bima yaliongezeka kwa
asilimia 18.5 hadi kufikia shilingi bilioni 481.7 ukilinganisha na shilingi
bilioni 406.7 ambazo ni mauzo ya mwaka uliopita.
64. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2014/15, TIRA
inatarajia
kutekeleza yafuatayo: kuendelea na maandalizi ya kufungua ofisi nyingine za
kanda; kuendelea na utaratibu wa uoanishaji (harmonise) sheria na kanuni za
soko la bima katika eneo la Afrika Mashariki na lile la nchi za SADC; kuendelea
na tafiti za bima ya kilimo, mifugo, pamoja na bima za watu wa kipato cha chini
(micro – insurance); na kukamilisha taratibu za kuanzisha bima ya Takaful.
Shirika la Bima la
Taifa – NIC
65. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara
ilikamilisha
urekebishaji wa Shirika la Bima la Taifa na usimikaji wa mfumo wa TEHAMA kwa
lengo la kuongeza ufanisi. Utendaji wa Shirika kibiashara uliendelea kuimarika
ambapo mapato ya bima yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 27.38 mwaka 2012, hadi
kufikia shilingi bilioni 31.53 mwaka 2013, ongezeko hilo ni sawa na asilimia
15. Mapato haya yalitokana na makusanyo ya bima za mtawanyo, vitega uchumi na
mapato mengine. Utekelezaji zaidi na malengo kwa mwaka 2014/15 yapo ukurasa wa
41 wa kitabu cha hotuba ya bajeti.
Masoko ya Mitaji na
Dhamana
66.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji
wa majukumu ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Soko la
Hisa Dar es Salaam na Dhamana ya Uwekezaji Tanzania pamoja na malengo kwa mwaka
2014/15 ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 42
hadi ukurasa wa 46.
67.
Mheshimiwa Spika, kuhusu
credit rating, wizara iko katika hatua za mwisho za kupata
taasisi mbili zitakazoendesha zoezi la tathmini ya kupima uwezo wa nchi wa
kukopa na kulipa madeni yake. Mwezi Februari 2014, Wizara iliziandikia kampuni
za Fitch, Moody’s Investment Services na Standard and poors kuwasilisha fomu
zao za mikataba kwa hatua za uchambuzi.
Tayari kampuni
ya Fitch na
Moody’s zimewasilisha fomu
za mikataba
kupitia kwa mshauri mwelekezi Citi Group. Aidha, kuchelewa kwa zoezi hili
kulitokana na kampuni hizi za upimaji (Rating Agencies) kutokukubaliana na aina
ya fomu za mikataba zinazoandaliwa na serikali pamoja na kuleta nyongeza ya
gharama nje ya makubaliano yaliyosainiwa awali.
Taasisi
za Kitaalam na Huduma Nyinginezo
68. Mheshimiwa
Spika, utekelezaji
wa majukumu kwa
mwaka
2013/14 pamoja na mipango kwa mwaka 2014/15 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bodi
ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu, Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na
Ugavi, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha pamoja na taasisi za mafunzo za Taasisi
ya Uhasibu Arusha, Chuo cha Usimamizi wa Fedha, Taasisi ya Uhasibu Tanzania,
Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika
ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti kuanzia ukurasa wa 46
hadi ukurasa wa 52.
CHANGAMOTO
69. Mheshimiwa
Spika, katika
kutekeleza majukumu yake,
Wizara
ilikabiliwa na changamoto zifuatazo:
i.
Kuongeza mapato ya ndani ya Serikali ili
kukidhi mahitaji ya matumizi ya maendeleo na ya kawaida;
ii. Mabadiliko ya hali ya uchumi na uongozi
katika nchi za washirika wa maendeleo ambapo zimepelekea kushindwa kutimizwa
kwa baadhi ya miadi;
iii. Uwezo wa kusimamia mikataba katika
kutekeleza baadhi ya miradi na programu za maendeleo; na
iv. Upatikanaji wa mikopo ya kibiashara kwa
wakati kunakotokana na kubadilika kwa masharti kutoka kwa wakopeshaji.
70.
Mheshimiwa Spika, katika
kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imeendelea kuchukua hatua
mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
i.
Kubuni vyanzo vipya vya mapato na kudhibiti
matumizi pamoja na kupunguza upotevu wa mapato;
ii.
Kuboresha ushirikiano na washirika wa
maendeleo yenye lengo la kuwa na uelewa sawa kuhusu masuala mbali mbali katika
ushirikiano wetu;
iii.
Kuendelea kuzijengea uwezo Wizara, Taasisi
na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kusimamia na kutekeleza mikataba ya
miradi na programu za maendeleo;
iv.
Kuendelea kutekeleza Programu ya Maboresho
ya Usimamizi wa Fedha za Umma - “Public Financial Management Reform Programme
(PFMRP)”; na
v.
Kushauri Wizara, Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuzingatia vipaumbele wakati wa kupanga na utekelezaji
kulingana na bajeti iliyotengwa.
vi.
Kuanza mazungumzo mapema na wakopeshaji wa
mikopo ya kibiashara.
Mapitio
ya Mapato na Matumizi ya Mafungu ya Wizara kwa Mwaka 2013/14
71. Mheshimiwa
Spika, mapitio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/14 ya
mafungu ya wizara ya fedha ambayo ni fungu 7,10,13,21,22,23 na 50 pamoja na
fungu 45 ni kama inavyooneshwa
katika kitabu cha hotuba kuanzia ukurasa wa 52 hadi ukurasa wa 56.
MAKADIRIO
YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15
Mapato
72. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara ya
Fedha
Fungu 50 inakadiria kukusanya mapato yasiyo ya kodi yapatayo shilingi 126,188,104,000
(bilioni 126.19)
Maombi ya Fedha
Fungu 50 – Wizara ya
Fedha.
73. Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa
fedha
2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a) Matumizi ya kawaida Shilingi 66,239,790,000
(bilioni 66.23). Kati ya hizo mishahara ni shilingi shilingi 5,620,668,000
(bilioni 5.62) na matumizi mengineyo shilingi 60,619,122,000
(bilioni 60.61).
(b) Miradi ya Maendeleo Shilingi 29,803,232,000
(bilioni 29.71).Kati ya hizo:
(i) Fedha
za Ndani - Shilingi 19,350,000,000 (bilioni 19.35).
(ii) Fedha za
Nje - Shilingi
10,453,232,000 (bilioni 10.45).
Fungu 23 – Idara ya
Mhasibu Mkuu wa Serikali:
74.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa
fedha
2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)
Matumizi ya kawaida - Shilingi 82,170,024,000
(bilioni 82.17). Kati ya hizo mishahara shilingi 5,012,762,000
(bilioni 5.01) na matumizi mengineyo shilingi 77,157,262,000
(bilioni 77.16).
(b) Miradi ya Maendeleo –
Shilingi 7,950,000,000 (bilioni 7.95) Kati ya hizo:
(i) Fedha za
Ndani -Shilingi 4,800,000,000 (bilioni 4.80).
(ii) Fedha za
Nje -Shilingi 3,150,000,000 (bilioni 3.15).
Fungu 22- Deni la
Taifa
75.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa
fedha
2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 4,354,865,076,000
(bilioni 4,354.86). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 10,341,136,000
(bilioni 10.34), Deni la Taifa shilingi 3,650,612,000,000 (bilioni
3,650.61) na matumizi mengineyo ni shilingi 693,911,940,000
(bilioni 693.91).
Fungu 21 - HAZINA
76.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa
fedha
2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a) Matumizi ya kawaida Shilingi 790,325,216,000
(bilioni 790.32). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 4,015,511,000 (bilioni 4.01) na
matumizi mengineyo shilingi 786,309,705,000 (bilioni 786.31)
ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya Idara na Taasisi zilizo chini ya Fungu hili,
nyongeza ya mishahara ya Watumishi wa Serikali na matumizi maalum.
(b)
Miradi ya maendeleo ni shilingi 57,417,015,000
(bilioni 57.42). Kati ya hizo;
(i) Fedha
za Ndani- Shilingi 17,000,000,000 (bilioni 17.0)
(ii) Fedha za
Nje- Shilingi 40,417,015,000 (bilioni 40.42)
Fungu 13 – Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu:
77.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa
fedha
2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a) Matumizi
ya kawaida - Shilingi 2,000,000,000
(bilioni 2.0).
(b) Miradi ya Maendeleo,
fedha za nje Shilingi 195,000,000 (bilioni
0.19).
Fungu 10 – Tume ya
Pamoja ya Fedha:
78. Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa
fedha
2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 2,318,661,000 (bilioni 2.32) kwa
matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, shilingi 318,661,000
(bilioni 0.32) ni kwa ajili
|
ya mishahara na
shilingi 2,000,000,000 (bilioni
|
2.0) ni
|
|
matumizi
mengineyo.
|
|
Fungu 7 – Ofisi ya
Msajili wa Hazina:
79.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa
fedha
2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a) Matumizi ya kawaida - Shilingi 88,455,278,000 (bilioni 88.45).
Kati ya hizo shilingi 670,328,000 (bilioni 0.67) ni
kwa ajili ya
mishahara na shilingi 87,784,950,000 (bilioni 87.78) ni
matumizi mengineyo.
(b) Miradi ya Maendeleo – Shilingi 1,943,000,000
(bilioni 1.94) Kati ya hizo:
(i) Fedha za
Ndani –Shilingi 650,000,000 (bilioni 0.65).
(ii) Fedha za
Nje -Shilingi 1,293,000,000 (bilioni
1.29).
Fungu 45 - Ofisi ya
Taifa ya Ukaguzi
80.
Mheshimiwa
Spika, katika
fungu hili kwa mwaka wa
fedha
2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a)
Matumizi ya kawaida shilingi 69,843,825,000
(bilioni 69.84). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 10,408,402,000 (bilioni 10.41) na
matumizi mengineyo shilingi 59,435,423,000 (bilioni 59.43).
(b)
Miradi ya maendeleo shilingi 13,011,432,000
(bilioni 13.01), kati ya hizo:
(i)
Fedha za
ndani shilingi 8,000,000,000 (bilioni
8.0).
(ii) Fedha
za nje shilingi 5,011,432,000 (bilioni
5.01).
HITIMISHO
81. Mheshimiwa
Spika, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Wakuu wa Idara na
Vitengo, Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha
wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Servacius B. Likwelile na Naibu Makatibu Wakuu
Ndugu Elizabeth J. Nyambibo, Prof. Adolf F. Mkenda na Ndugu Doroth S. Mwanyika
kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Vile vile,
napenda kuwashukuru Wakuu wa Taasisi na Wakala wa Serikali chini ya Wizara kwa
michango yao katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
82.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii
pia inapatikana katika tovuti ya Wizara ( www.mof.go.tz)
83. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:
Post a Comment