Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 23 May 2014

WWF YAWAWEZESHA WAKULIMA WA MPUNGA PAWAGA, IDODI

 


Na Daniel Mbega, Iringa

MFUKO wa Kimataifa wa Kuhifadhi Mazingira (WWF) mkoani Iringa umetoa mafunzo na vifaa kwa wakulima wa mpunga wa Kata za Pawaga na Idodi wilayani Iringa katika kuhamasisha kilimo shadidi.
Vifaa 12 vilivyotolewa, ambavyo vinatarajiwa kukabidhiwa kesho Jumamosi vitakavyosaidia kupalilia pamoja na kuvunia ambavyo vina thamani ya Shs. 960,000, vitawanufaisha wakulima wa mpunga wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mlenge, Pawaga kutoka vijiji vya Kinyika, Isele, Kisanga na Magombwe.
Vijiji vya Kata ya Idodi vitakavyonufaika ni Idodi, Tungamalenga, Mapogoro na Makifu ambavyo vipo katika Skimu ya Magozi.
Mbali ya vifaa hivyo, WWF pia imegharamia mafunzo hasa katika vijiji vya Kata ya Pawaga, mafunzo ambayo yanaendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la Rural Urban Development Initiative (RUDI) la mjini Iringa.
Ofisa wa WWF mkoani Iringa, Bi. Martha Sanga, amesema wanashirikiana na Idara ya Kilimo ya Wilaya ya Iringa katika mpango huo ili kuwawezesha wakulima wapate tija katika shughuli zao na kuwakomboa katika umaskini.
Mafunzo na vifaa hivyo, pamoja na gharama nyingine za uendeshaji, vimegharimu Shs. 8 milioni, ambazo ndizo zilizoombwa na Idara ya Kilimo kufanikisha zoezi hilo.
“Tuliwafuata Idara ya Kilimo Wilaya na kuwaambia kwamba tunataka kuwasaidia wakulima wa mpunga, lakini wilaya ikatuambia kwamba kwa kuwa nao wanafanya kazi katika maeneo hayo, basi ni vyema watueleza wapi walipopungukiwa ili tuwasaidie.
“Walisema wanahitaji kusaidiwa katika mafunzo na vifaa vya palizi, jambo ambalo nasi tumeona linafaa hasa kwa kuzingatia kwamba tulikuwa tumechelewa msimu wa kupanda, lakini mafunzo waliyoyapata yatawasadia wakulima kwa msimu ujao,” alisema Bi. Martha.
Katika mafunzo hayo, wakulima wanaelekezwa namna ya kushiriki katika kilimo bora chenye tija kwa uchaua mbegu bora kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo shadidi na kupanda kwa nafasi ya 25sm mstari kwa mstari na mche kwa mche.
Mbegu zinazopendekezwa kwa kilimo chenye tija ni aina ya Saro 5 (TXD 306) ambayo imeonekana bora zaidi, hairefuki, inatoa machipukizi mengi, ina uwezo wa kutoa mavuno mengi kutoka magunia 30 hadi 40 kwa ekari moja ambazo zina ujazo wa 80kg.
Inaelezwa kwamba, mbegu hiyo tayari imeanza kuonyesha matunda mazuri hasa kwa wakulima wa Skimu ya Tungamalenga ambao tayari wamekwishapatiwa mafunzo na shirika hilo la RUDI tangu mwaka 2013.
Shirika la WWF limejikita katika kuhamasisha shughuli za utunzaji wa mazingira pamoja na maendeleo ya jamii, ikiwemo kilimo, ambapo limekuwa likishiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu na vifaa kwa wanajamii.
Mwaka 2013 lilianzisha kampeni ya utunzaji wa mazingira katika ngazi ya shule kwa kutoa mafunzo kwa washiriki zaidi ya 60 kwenye Kijiji cha Ifunda mkoani Iringa ambapo pia walitoa vifaa mbalimbali vilivyogharimu Shs. 1.2 milioni kwa shule za Kibaoni, Ifunda Tech, Ifunda Girls na Lyandembera sekondari katika harakati za kuuokoa Mto Ruaha Mkuu ambao unakabiliwa na hatari ya kutoweka kutokana na shughuli za kibinadamu.
“Hii ni kampeni ya kuhifadhi mazingira, hasa katika eneo bonde la Mto Mbarali na Ndembera inayomwaga maji yao kwenye Mto Ruaha,” alisema wakati huo Ofisa Elimu ya Mazingira wa WWF, Mwamini Masanja.
Mto Ruaha unamwaga maji katika mabwawa ya Mtera, Kihansi na Kidatu ambayo yanategemewa sana katika uzalishaji wa umeme, hivyo kukauka kwake kunamaanisha kwamba uzalishaji huo utapungua na kuwa janga kwa taifa.
Hali ya baadaye ya Mto Ruaha Mkuu inaonekana kuwa mashakani huku jitihada za serikali na wadau wa uhifadhi mazingira zikionekana kugonga mwamba baada ya mto huo kukauka kwa kasi hivyo kutishia maisha ya binadamu, wanyama na viumbehai vingine hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Pamoja na serikali kuwafukuza wafugaji waliokuwa wamevamia mabonde ya Usangu na Ihefu na kuwahamishia Kilombero, lakini shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika mashamba makubwa ya mpunga huko Mbarali, Kapunga, Madibira, Pawaga na Idodi yamefanya maji mengi kuishia mashambani na hivyo kutishia pia uwepo wa Bwawa la Mtera ambalo nalo linakauka.



1 comment: