
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP), Hellen Clark akikabidhi moja ya kompyuta mpakato kati ya 60 kwa mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damiani Luvuva, alipokutana na wakuu wa NEC, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) pamoja na mabalozi wa nchi mbali mbali za Ulaya, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka NEC, Julius Malaba. Picha na Emmanuel Herman.
Dar es Salaam. Shirika la Mpango wa Maendeleo la
Umoja wa Mataifa (UNDP) limeeleza nia ya kuisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) ili ifanikishe matumizi ya mashine za kisasa za Biometric Voters Register
(BVR) wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Hellen Clark alitoa ahadi hiyo jana
na kuongeza kuwa hata hivyo, matumizi ya mashine hizo yamechelewa kwani
zilitakiwa zitumike tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, muda uliobaki unahitaji
utekelezaji ili zitumike mwakani.
Clark ambaye pia ni waziri mkuu wa zamani wa New Zealand,
alisema hayo wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ziara yake ya siku nne
nchini.
Alisema alipokuja nchini mwaka 2010 alitembelea NEC na kuziona
kompyuta zilizokuwa zikitumika kusajili wapigakura kuwa zilikuwa zinatumia
mfumo uliopitwa na wakati.
“Natambua kuwa kuna mpango wa kuwenda kwenye mashine za BVR ambazo
zitahusisha uchukuaji wa alama za vidole na mambo mengine, natambua kuwa uamuzi
umeshachukuliwa kuhusu mfumo huo, umechelewa, lakini sasa utekelezaji
unatakiwa,” alisema.
Kauli hiyo imetolewa siku chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda kulitaarifu Bunge mjini Dodoma kuwa NEC inaendelea na maandalizi ya
kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi la kuboresha daftari la kudumu la
wapigakura.
Pinda alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akisoma hotuba kuhusu
mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya
ofisi yake na ofisi ya bunge kwa mwaka 2014/15.
Katika hotuba yake, Pinda alieleza kuwa mfumo wa BVR
utakaotumika ni tofauti na mfumo wa awali wa Optical Mark Recognition (OMR)
ambao ulikabiliwa na changamoto nyingi za utendaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva
akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, alisema kuwa mashine za BVR
zitatumika wakati wa uandikishaji wapigakura pekee yake.
Akizungumza kwa kujiamini, Hellen alisema Tanzania imeshafanya
uchaguzi mara nne kwa mafanikio makubwa.
Alisisitiza kuwa UNDP ipo tayari kutoa msaada wowote wa kiufundi
ingawa mpango huo ni wa kitaifa, lakini mradi wa wa shirika hilo unatoa nafasi
kuisaidia NEC.
Clark ambaye ameshafanya ziara nne nchini, alisema kuwa wadau
mbalimbali wanaoshirikiana na shirika lake wameshatoa dola 22 milioni sawa na
Sh35.2 bilioni kusaidia mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika
mwakani.
“Hali kadhalika, tutashirikiana nanyi katika kuhakikisha
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanashiriki kwenye uchaguzi huo,”
aliongeza.
Hata hivyo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe wakati akiwasilisha taarifa ya kambi yake bungeni kwenye Bunge la bajeti
mwaka jana, alimtaka Waziri Mkuu Pinda kuiamuru NEC kusimamisha maandalizi ya
mfumo wa uchaguzi wa elektroniki hadi hapo itakapowashirikisha wadau.
Mbowe alisema tayari NEC imekiri kuanza maandalizi huku wadau wa
uchaguzi vikiwamo vyama vya siasa hawajashirikishwa.
Ujangili Tanzania
Akieleza masuala aliyozungumza na Rais Jakaya Kikwete, Clark
alisema kuwa alimwelezea changamoto za ujangili na umaskini aliouona
alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kwamba kuna umaskini mkubwa, njaa,
watoto hawapati elimu ya kutosha na kinamama wajawazito wanakufa kwa sababu
zinazoweza kuzuilika.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment