Pages

Pages

Pages

Friday 9 May 2014

TUNAUZA VINU, MITWANGIO BURE!

 
Manyoni, Singida

Ndugu zangu,
Vinu ni miongoni mwa zana zilizokuwa zikitumiwa na babu na bibi zetu enzi hizo katika shughuli mbalimbali. Hata kizazi chetu pia kimeendelea kuvitumia kwa ajili ya kukoboa nafaka na hata kuzibadili nafaka hizo kuwa unga.
Binafsi nimevitumia sana enzi zile kwa kukoboa mpunga, mtama na mahindi, lakini pia hata kutwanga mboga za asili hususan mlenda na kalanga.
Na vinu vinatofautiana kwa sura na umbile lake - viko vikubwa lakini viko pia vidogo (kwa ajili ya kutwangia karanga na mlenda na mboga nyinginezo, vikiwemo vitunguu swaumu). Pia vipo vilivyowekwa urembo na kuvutia zaidi, lakini vipo ambavyo vimetengenezwa bila urembo wowote. Vyote kazi ni moja tu.
Kwa siku za karibuni, ambapo tayari kuna maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, tayari tumeshuhudia matumizi ya vinu yakibadilika kutoka yale ya asili. Watu wengi wanapeleka nafaka kwenye mashine za kukoboa na kusaka, zinazotumia mafuta na umeme.
Adha ile ya kupata mabungu mikononi kwa kazi nzito ya kutwanga imepungua, hivyo vinu vinaelekea kukosa nafasi yake ya asili.
Lakini bado zinaendelea kutumiwa huku vijijini kwa shughuli nyinginezo, na ukivikuta mjini, siku hizi vimegeuzwa mapambo na kumbukumbu nzuri kwamba ni mojawapo ya zana asilia zinazoelekeza mabadiliko ya binadamu katika uvumbuzi.
Hata hivyo, kinu lazima kiwe na mtwangio wake. Unapouliza bei kwa muuzaji unasema 'kinu bei gani?' husemi 'mtwangio bei gani?' maana huo atakupatia bure tu ili kukamilisha seti ya kinu.
Mitwangio nayo ina saizi yake kulingana na saizi ya kinu chenyewe, na hawa jamaa wanaochonga vinu ni mafundi kweli kweli. Huwezi kuchukua mtwangio mdogo wakati kinu chako kikubwa, vivyo hivyo huwezi kuchukua mtwangio mkubwa wakati kinu kidogo! Kama huna utaalam unaweza usipate mtwangio unaofaa, lakini ukiwauliza wenyewe watakueleza.
Naam, yote ni mabadiliko ya teknolojia, na tuna kila sababu ya kuwapongeza wazee wetu waliobuni zana hizi ambazo enzi zile zilikuwa bora kabisa kwa kuaidia shughuli mbalimbali.

Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Singida
0656-331974

No comments:

Post a Comment